Thursday, July 17, 2025
spot_img

TANZANIA KUTOA TAMKO UN-HABITAT KESHO

RIPOTA PANORAMA

Nairobi, Kenya

TANZANIA, kesho itatoa tamko kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT) kuhusu hatua inazochukua kukabiliana na changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya malengo ya milenia ambayo kila nchi duniani inatekeleza.

Tamko hilo litatolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula ambaye anamuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo uliofunguliwa leo na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dk. William Samoe Ruto ukiwa na wawakilishi kutoka pembe zote za dunia.

Waziri Mabula atatoa tamko hilo mbele ya washiriki zaidi ya 5,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani wakati dunia ikingali inakabiliwa na changamoto mbalimbali za makazi zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO 19, mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kivita iliyoongeza hali ya umaskini, huduma hafifu za makazi, njaa na mafuriko katika maeneo kadhaa ya dunia. 

Jana, Waziri Mabula aliongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano wa Baraza la Mawaziri duniani wanaohusika na uendelezaji wa miji na makazi.

Mkutano huo ulitangulia Mkutano Mkuu wa Shirika la Makazi Duniani ulioanza leo jijini Nairobi ambao kauli mbiu yake ni “hatma ya miji endelevu kupitia ushirikishwaji na uwepo wa mifumo ya mahusiano ya kimataifa.”

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN- Habitat) Maimunah Mohd Sharif amesema ifikapo mwaka 2030, watu bilioni tatu, ambayo ni asilimia 40 ya idadi ya watu duniani watakuwa wakiishi mijini katika makazi yasiyo salama na yasiyokuwa na huduma muhimu. 

Maimunah ameyasema hayo alipokuwa akitoa hotuba ya utangulizi ya kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Kenya, Ruto kufungua mkutano huo. 

Amesema ili kukabiliana na hali hiyo, nchi zote duniani zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto zitakazotokana na kuongezeka kwa idadi ya watu. 

Maimunah amesema changamoto hizo zinahitaji Serikali zote za dunia kushiriki kikamilifu kukabiliana nazo ili kufikia malengo ya milenia ya kuwa na miji endelevu, salama na jamii imara. 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula (katikati) Meneja Habari na Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa, Muungano Saguya (Kulia) na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze (kushoto) wakishiriki mkutano wa Baraza Kuu la Shirika la Makazi la Umoja wa Matifa (UN-HABITAT) ulioanza leo jijini Nairobi, Kenya.

Akifungua Mkutano huo wa Baraza Kuu la Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa, Rais Ruto amesema dunia ipo katika wakati mgumu wa kuwapatia watu wake makazi bora kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, machafuko ya kisiasa na kukosekana kwa uwezo wa kuwapatia wananchi makazi bora na salama. 

Amesema Afrika inakabiliwa zaidi na changamoto hizo ambapo asilimia 68 ya watu wake waishio mijini wanakaa katika makazi holela.

Rais Ruto amesema kama nchi za dunia, hususan Bara la Afrika hazitachukuwa hatua madhubuti kuondoa hali hiyo, nchi hizo ambazo idadi ya watu wake inakua kwa kasi zitashindwa kufikia maendeleo endelevu na kutekeleza malengo ya milenia ya ujenzi wa miji salama na endelevu. 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula akishiriki majadiliano kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika Mkutano wa Baraza Kuu la Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-HABITAT), ulioanza leo jijini Nairobi Kenya.

Amesema  kwa kutambua kuwa Afrika inakabiliwa na changamoto hizo, nchi yake imekubali kuandaa Mkutano wa Nchi za Afrika, mwezi Septemba, 2023 utakaojadili na kukubaliana namna bora ya kutatua changamoto za makazi na mabadiliko ya tabianchi. 

Aidha, Rais Ruto ametaka wajumbe wa mkutano huo kuibua majawabu yatakayosaidia dunia kukabiliana na changamoto za makazi zinazokabili dunia hivi sasa, kwa kuja na mikakati na sera imara. 

Amebainisha kuwa Serikali yake imekuja na mkakati wa “nyumba kwa kila Mkenya” utakaowaletea wakenya maisha bora ambao utashirikisha sekta binafsi na wakenya kwa ujumla. Mkakati huo unakusudia pia kuongeza wigo wa mikopo ya nyumba, kuongeza ajira na pia unalenga kuwezesha upandaji miti milioni 60 kila mwaka ili kuwa na Kenya ya Kijani.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya