RIPOTA PANORAMA
MBUNGE wa Kisesa na waziri wa zamani wa mifugo na uvuvi, Luhaga Joelson Mpina ametakiwa kutii na kuheshimu amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro iliyomnyang’anya umiliki wa ekari 700 za ardhi na kuzirudisha kwa wananchi.
Hayo yameelezwa na wananchi wa Kijiji cha Dala hivi karibuni walipokuwa wakiwasilisha kilio chao kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa kuhusu kudhulumiwa mashamba yao na Mpina na pia kumtuhumu kuharibu mazao yao.
Nsemwa akiwa njiani pamoja na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya yake kwenda kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi wa vijiji vya Dala, Kongwa na Mbwade, msafara wake ulisimamishwa na wananchi hao na kumuomba kufikisha kilio chao kwa Rais Samia Suluhu Hassan cha kuporwa ardhi yao Mpina waliyedai pia haheshimu amri ya mahakama iliyomtaka kurejesha ardhi aliyopora kwa wananchi hao.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo iliyosomwa Agosti 23, 2018 na Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Morogoro, M. Khasim inawatamka wakulima 15 waliomshataki Mpina kuwa ndiyo wamiliki halali wa eneo la ekari 700 ambazo Mpina kupitia Kampuni yake ya MPSON”S alizivamia na kuharibu mazao.
Ni hukumu ya shauri namba 54 lililofunguliwa mwaka 2018 na wakulima hao 15 wa Kijiji cha Dala dhidi ya Kampuni ya MPSON’S, mali ya Mpina iliyomtia hatiani kwa kuvamia ardhi na kuharibu mazao.
Hukumu inamtaja mdaiwa kwamba ni mvamizi katika eneo hilo na ilitoa zuio la kudumu kwake kutojishughulisha na eneo lenye mgogoro ikiwa ni pamoja na kuingia au kulima.
Aidha, mdaiwa Kampuni ya MPSON’S ya Mpina imeelekezwa kuwalipa wakilima hao fidia ya uharibifu wa mazao alioufanya kupitia taarifa ya tathmini ya mtalaamu huku gharama za shauri zikitolewa.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebecca Nsemwa
Anaeleza kuwa waombaji walifungua madai wakiomba baraza litamke kwamba wao ni wamiliki halali wa eneo lenye mgogoro, baraza litoe zuio la kudumu dhidi ya mdaiwa, wafanyakzi wake au mtu yoyote anayefanya kazi au mwenye uhusiano naye kutoingia au kujishughulisha na eneo lenye mgogoro kwa namna yoyote ile.
Pia waombaji waliomba baraza litamke kwamba hasara ya jumla ya Shilingi 100,000 itolewa, gharama za shauri na nafuu zozote ambazo baraza hilo litaona zinafaa kutolewa.
Hukumu inaeleza kuwa katika shauri hilo, wadai ambao ni wakulima wa mpunga walidai kwamba katika msimu wa mwaka 2017/28, mdaiwa alivamia maeneo yao na kuharibu mazao yaliyokuwa shambani akidai kuwa eneo hilo ni mali ya kampuni yake.
Kwa mujibu wa hukumu, mdaiwa akiwakilishwa na Wakili Malimi Juma, alipinga madai ya waombaji waliokuwa wakiwakilishwa na Wakili Asifiwe Alinanuswe kwa kuwasilisha utetezi wa maandishi barazani hapo na shauri hilo lilianza kusikilizwa upande mmoja baada ya mdaiwa na wakili wake kuacha kuhudhuria mahakamani.
Hukumu huyo ambayo Tanzania PANORAMA imeiona anaeleza upande wa waombaji ulikuwa na mashahidi tisa na baraza lilijiwekea viini vitatu kabla ya kuanza kusikiliza shauri hilo; ambavyo ni kama waombaji ndiyo wamiliki halali wa eneo lenye mgogoro, kama mdaiwa kupitia wafanyakazi wake wamevamia eneo la waombaji na nafuu zozote ambazo wadai wanastahili kupata.
Shahidi wa kwanza anayetajwa kwenye hukumu hiyo kutoa ushahidi wake ni Juma Sume ambaye aliiambia mahakama kuwa yeye mkulima mwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 30 lililopo eneo la Kivumba alilopatiwa na Serikali ya kijiji lakini mwaka 2017, mdaiwa alilivamia na kuharibu mazao yake ambayo ni mpunga.
Wa pili anayetajwa kwenye hukumu ni Consolata Mchuma aliyeieleza mahakama hiyo kuwa anamiliki shamba lenye ukubwa wa ekari 20 alilopewa na Serikali ya kijiji na kwamba lilivamiwa na mdaiwa mwaka 2017 na kumzuia asilime. Katika uvamizi huo aliharibu mazao yake yaliyokuwa shambani kwake.

Consolata Mchuma
Shahidi Zuberi Muhundogwa yeye aliieleza mahakama kuwa mdaiwa alivamia adhi yake iliyokuwa na mazao na kuyaharibu na Mohamed Kilima Sinde, yeye aliieleza mahakama kwamba ni mkulima na Mwenyekiti wa Kijiji cha Dala.
Alisema mdaiwa ambaye mmiliki wake ni Luhaga Mpina alikuwa analima ekari 300 katika Kijiji cha Dala tangu mwaka 2003 lakini baadaye viongozi wa Serikali ya kijiji walimpa ekari 700 bila idhini ya wanakijiji hivyo wanakijiji walipeleka malalamiko yao kwa Waziri Mkuu ambaye alituma watu wake kuchunguza mgogoro huo.
Sinde aliendelea kuieleza mahakama kuwa Julai, 2019 viongozi wa mkoa na wilaya na Mpina walikwenda kwenye eneo lenye mgogoro ambako ulifanyika mkutano na kubainika viongozi wa kijiji walikosea kutoa ardhi bila idhini ya wanakijiji na Mpina aliahidi kulipa fidia kwa wananchi aliovamia ardhi yao lakini baadaye alisema atamlipa kila mmoja Shilingi 400,000 bila kujali ukubwa wa eneo lake na hapo ndipo maelewano yakakosekana.
Shahidi David Augustine Bihita, yeye aliieleza mahakama kuwa ni Afisa Mtendaji (VEO) wa kijiji na kwa wadhfa wake aliitisha mkutano uliowashirikisha pia mkuu wa Mmkoa, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri baada ya mdaiwa kuvamia eneo la wadai.
Alisema mdaiwa aliueleza mkutano huo kuwa alipewa ekari 300 mwaka 2009, baadaye aliomba ekari 700 na maombi yake yalijadiliwa na Serikali ya kijiji, eneo aliloomba lilitembelewa kwa gharama zake lakini wakati anasubiri majibu, akapewa taarifa za kuwepo kwa kesi hiyo.
Bihita alisema mkutano uliazimia mdaiwa afuate utaratibu wa kuomba ardhi ya kijiji na atatue mgogoro uliopo lakini kulitokea kutokuelewa kuhusu kiasi cha malipo ya fidia na mdaiwa aliendelea kutumia eneo lenye mgogoro.
Donald Joseph Kipondya, Afisa Mtendaji Kata ya Mvuha yeye aliieleza mahakama kuwa Mpina amechukua eneo la wakulima na katika mkutano uliofanyika Julai, 2019 iligundulika alivamia eneo hilo.
Mashahidi wengine wa upande wa wadai katika kesi hiyo walikuwa Keikei Masanja Singu na MarryStella Chamlungu ambao ushahidi wao haukutofautina na ushahidi uliotolewa awali lakini shahidi Philemon Matungwa Kawamala alisema mdaiwa alivamia eneo lake na kuharibu mazao yake hivyo amfidie.
Hukumu inaeleza kuwa baraza limejiridhisha wadai ni wamiliki halali wa eneo lenye mgogoro baada ya kuthibitishwa na wao wenyewe pamoja na viongozi wao na kwamba mdaiwa alivamia maeneo ya wakulima hao na kuharibu mazao yao.
Hukumu inasomeka; “baraza hili baada ya kupitia majibu ya mdaiwa na vielelezo vyote ambavyo havikutolewa kama ushahidi kwa kuwa mdaiwa hakuhudhuria na kesi imesikilizwa upande mmoja. Baraza limejiuliza Halmashauri ya Serikali ya Kijiji yenye watu 25 iliopata wapi mamlaka ya kugawa ardhi yenye ukubwa wa ekari 700.
“Kiutaratibu, halmashauri ya kijiji ina uwezo wa kugawa ekari tano na endapo ekari zikifika 50 lazima wanakijiji waridhie na zikizidi ekari 50 lazima uongozi wa juu ushirikishwe. Halmashauri hii ya Kijiji cha Dala ilipata wapi mamlaka ya kugawa ekari 700?.”
Aidha, inasema kuwa shauri lilianza kusikilizwa baraza likiwa na wajumbe wawili lakini mmoja alifariki kabla ya kumalizwa kwa usikilizwaji na mjumbe mmoja aliyebakia, Jane Mngazija katika maoni yake alisema kutokana na ushahidi uliokusanywa, mdaiwa atamkwe ni mmiliki halali wa eneo bishaniwa kwa sababu alifuata utaratibu na amepewa eneo hilo na Halmashauri ya Kijiji cha Dala.
Inasema baraza lilipitia maoni ya mjumbe ambayo yanaheshimiwa lakini hayakukubaliwa kwa sababu utaratibu wa ugawaji eneo la nyongeza la ekari 700 haukuzingatia matakwa ya sheria na hivyo ugawaji uliofanyika ni batili.