RIPOTA PANORAMA
BENKI ya National Microfinance (NMB), imeanza kuchunguza tuhuma za wizi wa fedha za wateja wake unaodaiwa kufanywa na wafanyakazi wa benki hiyo.
Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog zimeeleza kuwa tayari Polisi wa Benki ya NMB kutoka makao makuu, Dar es Salaam ametumwa kwenda NMB Tawi la Mafinga kuchunguza madai yaliyotolewa na mteja wa benki hiyo, Habakuki Stefano Nsyenge ya kuibiwa fedha zake na wafanyakazi wa benki hiyo.
Imeelezwa kuwa polisi huyo wa benki tayari amekwishamuhoji Nsyenge kuhusu hilo na pia amewahoji maofisa wa benki hiyo wa Tawi la Mafinga ambao inadawa wamekanusha baadhi ya madai ya Nsyenge.
Nsyenge mwenyewe ameithibitishia Tanzania PANORAMA kuhojiwa na polisi huyo wa benki na kueleza kuwa amempa taarifa zote alizozihitaji, ikiwemo barua alizoiandikia benki kueleza jinsi fedha zake zilivyoibiwa na maafisa wa Benki ya NMB Mafinga lakini wao wamekanusha kuzipokea.

Habakuki Nsyenge
Vyanzo vya habari vya Tanzania PANORAMA vimeeleza kuwa maafisa wa NMB Mafinga wamekanusha kupokea barua yoyote kutoka Nsyenge inayolalamikia kuibiwa pesa zake ikiwa ni pamoja na barua zilizokuwa zikieleza nia yake ya kuchukua hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, polisi wa benki amefanya uchunguzi wa kina baada ya maafisa hao kukanusha kupokea barua za Nsyenge ikiwa ni pamoja kufuatilia kamera za benki hiyo na imeelezwa zaidi kuwa tayari ameishakamilisha uchunguzi wake na kurejea makao makuu, Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna alipoulizwa iwapo uchunguzi huo umekamilika hakujibu.
Miezi miwili iliyopita, Tanzania PANORAMA iliripoti taarifa kuhusu mbinu zinazodaiwa kutumiwa na wafanyakazi wa NMB kuiba fedha kwenye akaunti za wateja kisha kuzirejesha wanapobainika.
Habakuki Stefano Nsyenge ndiye aliyefichua mbinu hizo katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog, jijini Dar es Salaam alipoeleze madai ya kuibiwa fedha zake kwenye akaunti na wafanyakazi wa benki hiyo, kisha kurejeshewa huku akiombwa msamaha na Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Mafinga, Focus Lubembe.
Katika mahojiano hayo, Nsyenge alidai alibaini fedha zake zimeibiwa kwenye akaunti baada ya kuangalia bank statement yake na kubaini akaunti yake ya mkulima inakatwa ‘service charges’ mara mbili ambazo ni ‘saving na ‘current.’
Akielezea jinsi alivyobaini hilo, alisema; “Yule mhudumu wa benki alipoangalia kwenye akaunti yangu, ‘psychologically’ nikaona anashtuka. Baadaye ninapongoja majibu nikaona hana majibu ya kunipa na wakati huo huo kwenye dirisha lake kukawa kuna mstari mrefu wa wateja wanangoja. Mimi nikamwambia kijana naona hii ni ‘technical issue’ naomba niruhusu uendelee na wateja wengine mimi nitakuja kesho.
“Kwa hiyo tukaachana pale nikamfuatilia kesho yake, lakini ninapomfuatilia kesho yake sikwenda kwa maneno, nilikuwa nimeishaandika barua kabisa inayoonyesha mazingira ya akaunti yangu ni nini nimechukua na kile ambacho kinapungua kwenye akaunti yangu. Bahati nzuri kesho yake nilimkuta yule yule mhudumu nikampatia ile barua akaipeleka kwa supervisor wake.
“Ilipopelekwa kwa supervisor, ninaposubiri majibu, supervisor naye akakosa majibu. Baada ya kukosa majibu akanambia samahani baba naomba uniachie namba yako ya simu nitakupigia baada ya siku kadhaa, siku mbili, tatu. Nikampa namba yangu ya simu, ilikuwa nafikiri ijumaa, jumamosi ikawa kimya, jumatatu ikawa kimya, jumanne mimi nikaenda lakini bado akawa hana majibu ya kunipa.
“Baadaye mimi nikalazimika kuingia na kuangalia kwenye ‘bank statement’ yangu ili nione uhalisia maana kabla ya hapo nilikuwa sijaangalia, sasa nilipo‘check’ kwenye ile ‘statement’ ndipo sasa nikaona kwanini kuna kigugumizi katika suala la akaunti yangu.
“Nilipo‘check’ nikagundua kuna makato ambayo yameandikwa kwa namna ambayo mtu mwingine asiyejua, anaweza kuona ni ya kawaida. Lakini ikaonekana makato yanaandikwa, ‘service charges, savings and current.’ Sasa nikajiuliza toka lini akaunti moja ikawa inasomeka ‘savings and current,” alidai Nsyenge.

Alisema baada ya sintofahamu hiyo alitafuta mwanasheria ambaye baada ya kuangalia ‘bank statement’ yake alimwelekeza kumwandikia barua Meneja wa NMB Tawi la Mafinga kuyahoji makato hayo kwenye akaunti yake.
Nsyenge alisema baada ya kumkabidhi meneja barua, aliwasiliana na ‘supervisor’ naye akakiri kuona barua ya malalamiko yake na kwamba wawili hao walishauriana kwa muda kabla ya kumuomba awape muda wa kushughulikia tuhuma alizokuwa akiielekezea benki hiyo.
Alisema aliwahoji maswali ambayo maafisa hao wa benki hawakuwa na majibu na badala yake walimuomba awasamehe naye aliwataka warudishe fedha zilizoibiwa kwenye akaunti yake, walipe hela (advance) aliyokuwa amemlipa wakili kisha angefunga akaunti yake kwa kile alichoeleza hakuwa na sababu ya kuweka fedha kwenye benki ya watu ambao hawaheshimu maadili ya kazi yao.
Nsyenge alisema Meneja wa NMB Mafinga, Lubembe aliwaita ofisini kwake vijana waliohusika na hilo na kuwataka warudishe fedha walizokuwa wamezichukua kwenye akaunti ya Nsyenge ambao walimlipa kiasi kwa kumpa mkononi huku wakiahidi kuendelea kumlipa taratibu.
Tanzania PANORAMA ilimuuliza Kaimu Meneja Habari na Mawasiliano wa NMB, Vicent Mnyanyika kuhusu hilo naye akijibu, alisema hawezi kujibu kila malalamiko inayoelekezewa Benki ya NMB.