RIPOTA WA WAZIRI MKUU
Dodoma
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amemwagiza Waziri wa Madini, Dotto Biteko kuzifuatilia taasisi za fedha zinazowakopesha wachimbaji wadogo kwa kuangalia viwango vya riba vinavyotolewa na aina ya shughuli wanazozifanya wajasiriamali hao ili kurahisisha urejeshaji wa mikopo.
Agizo hilo alilitoa jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba wakati wa kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.
Makamba alimuuliza Waziri Mkuu Majaliwa kuwa Serikali ina mpango gani wa kutengeneza mazingira rafiki ya upatikanaji wa mikopo kwa wachimbaji wadogo kulingana na uhalisia wa biashara zao.
Akijibu, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali inatambua changamoto ya masharti mbalimbali kwa taasisi za kifedha, hivyo imetoa maelekezo kwa taasisi hizo kutambua aina ya shughuli zinazofanywa na wajasiriamali hao na muda unaotumika kuanzia uwekezaji hadi uzalishaji ili masharti yaendane na shughuli husika.
Aliwashauri wajasiriamali hao wajiunge katika vikundi ili waweze kupata mikopo inayotolewa na Serikali (asilimia 10 ya mapato ya halmashauri), mifuko ya uwezeshaji pamoja na taasisi mbalimbali za kifedha.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaagiza viongozi wote katika maeneo yanayonufaika na fedha za uwajibikaji (CSR) kutokana na miradi mbalimbali ya uwekezaji kuzisimamia vizuri na kuzitambulisha kwenye mabaraza ya madiwani ili waweze kuzipangia utaratibu wa matumizi kama ilivyokusudiwa.
Aliyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busega, Simon Songe aliyetaka kujua mpango wa Serikali kuhakikisha fedha za CSR zinatumika kwa wakati pindi zinapofikishwa katika maeneo husika.
Aliseima fedha za CSR zinapaswa kuingia kwenye mfuko wa mapato ya ndani ya kijiji au halmashauri ili ziratibiwe na kupangiwa miradi ya kutekeleza kulingana na mahitaji ya jamii husika. “Fedha hii inapoingia inakuwa sehemu ya bajeti na ni lazima itumike na Serikali inazisimamia kupitia halmashauri zetu.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa alisema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa vibali kwa Wizara ya Afya kuajiri watumishi wa sekta ya afya watakaoongeza nguvu ya kuwahudumia wananchi kwenye maeneo yote ya kutolea huduma zikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Alisema hilo linakuja baada ya kukamilika kwa ujenzi wa maeneo ya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo zahanati, vituo vya afya, hospitali za halmashauri za wilaya, mikoa na kanda. “Kazi nyingine inayoendelea kwa kasi ni ya kupeleka vifaa tiba na dawa.”
Akijibu swali la Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde aliyehoji mpango wa Serikali kuhakikisha miundombinu iliyopo katika maeneo ya kutolea huduma za afya na vifaa vinaendana na utoaji huduma wa uhakika kwa kupitia uwepo wa wataalamu wa kutosha.
“Kazi kubwa imefanywa, nampongeza Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake na kwa usimamizi wake, sisi tutaendelea kuimarisha maeneo hayo ya utoaji huduma na Serikali itaendelea kujenga miundombinu hiyo kulingana na mahitaji ya eneo husika,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa alitaja mpango mwingine wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ua upungufu wa watumishi ni kufanya mapitio ya ikama ya watumishi na kwa kuhamisha watumishi katika maeneo yenye watumishi wengi kuwapeleka kwenye upungufu.