RIPOTA PANORAMA
MBUNGE wa Jimbo la Kisesa na waziri wa zamani wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina ‘amevuliwa nguo’ na wananchi wa Kijiji cha Dalla kilichopo Halmashauri ya Morogoro Vijijini waliomtuhumu hadharani kwa ukatili ya udhulumaji.
Tuhuma hizo zimetolewa hivi karibuni na wananchi hao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro (DC), Rebecca Nsemwa aliyesimamishwa akiwa njiani kwenda kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi wa Vijiji vya Dalla, Kongwa na Mbwade.
DC Nsemwa aliyekuwa ameongozana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya yake, alisimamishwa na wananchi waliokuwa na mabango yenye ujumbe wa kutaka kurudishiwi ardhi yao zaidi ya ekari 700 wanazodai kudhulumiwa na Mpina, ambaye alizichukua kinyume cha utaratibu na pia kufyeka mazao yao yakiwa shambani huku akikataa kulipa fidia kwa kitendo chake hicho cha kikatili.
Mbali na ujumbe uliokuwa kwenye mabango hayo, mabango mengine yalikuwa na ujumbe unaomuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusikia kilio chao kuhusu dhuluma waliyofanyiwa na Mpina kwenye ardhi yao.
Baada ya DC Nsemwa na msafara wake kusimama kuwasikiliza wananchi hao, wa kwanza kueleza kile alichodai ni dhuluma iliyofanywa kwa wananchi wa Kijiji cha Dalla, alikuwa Consolata Mchuma aliyeeleza kuwa yeye na wanakijiji wenzake wameteseka kwa zaidi ya miaka nane kwa sababu ya ukatili na udhulumaji wa Mpina.
Alisema, awali akiwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Dalla, ilitangazwa kupatikana kwa mwekezaji ambaye ni Kampuni ya MPSONS Co. Ltd ambayo Mpina ni mwanahisa mkubwa aliyetaka kumegewa pande la ardhi lenye ukubwa wa ekari 300 kwa ajili ya shughuli za kilimo na kukubali kulipa Shilingi elfu tano kwa kila ekari moja pamoja na kujenga madarasa manne, mawili katika Shule ya Msingi Dalla na mengine mawili katika Shule ya Msingi Kilengesi.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Tanzania PANORAMA Blog, Kampuni ya MPSONS iliyotajwa na wananchi wa Dalla katika malalamiko yao, ilisajiliwa Agosti Mosi, 2006 na kupewa namba ya usajili 57225 ikiwa na ofisi Mtaa wa Lindi, uliopo Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam.
Nyaraka zilizoko Serikali zinaonyesha Kampuni ya MPSONS ilisajiliwa ikiwa na mtaji wa Shilingi milioni mbili na pia ikiwa na wanahisa wanne, Mpina akiwa mwanahisa mkubwa mwenye hisa 520. Wakurugenzi wa kampuni hiyo ni Juma Isack Mpina, Amos Kulwa Zephania, Benedict James Kasele na Luhaga Joelson Mpina.
Consolata alisema, mwaka 2016 akiwa Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Dalla, Mpina alipeleka barua ya kutaka kuongozewa eneo lingine la ekari 700 lakini wanakijiji walikataa huku wakimtaka afike Ofisi ya Serikali ya Kijiji ili atekeleze ahadi yake, jambo ambalo alilikaidi.

Alisema baadaye Mpina (pichani juu) alilitwaa eneo hilo kwa madai kwamba amelinunua, jambo lililowashangaza wanakijiji kwa sababu hawakushirikishwa wala hakukuwa na muhtasari wa mkutano wa kijiji wa kuidhinisha uuzwaji wa eneo lao hilo.
Mwingine aliyezungumza huku akibubujikwa machozi ni Diwani Mstaafu wa Tarafa ya Mvuha, Marrystela Chamlungo aliyesema pamoja na Mpina kuchuku eneo hilo, alifyeka mazao ya wanakijiji yaliyokuwa shambani na kuwasababishia hasara kubwa na alipoitwa kwenda kulipa fidia ya uhalibifu alioufanya, alikataa kwenda.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbwade, Salumu Malozo alisema Mpina amemega eneo katika vijiji vitatu vya Mbwade, Kongwa na Dalla na kusababisha mgogoro kwa wananchi wa vijiji hivyo.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Halima Mtawazo alisema Mpina alizungumza na wajumbe 25 wa halmashauri ya kijiji lakini maombi yake hayakukamilika kwa kuwa wajumbe hao hawakuitisha mkutano wa kijiji ili kuidhinisha kuuzwa kwa pande hilo kubwa la ardhi yao.
Akitoa uamuzi wa Serikali ya Wilaya, DC Nsemwa alisema anaunda timu ya watalaamu itakayopitia nyaraka za pande zote na kupima eneo la shamba hilo ili kubaini ukubwa wake.
DC Nsemwa aliipa timu hiyo siku 14 kubaini uhalali wa nyaraka na upimaji wa mipaka ili kila upande upate haki na alimtaka Mpina kutoa ushirikiano kwa timu hiyo.
Jitihada za kumpata Mpina kwa simu yake ya kiganjani kuzungumzia tuhuma alizoelekezewa na wananchi hao hazikufanikiwa; hata hivyo Tanzania PANORAMA Blog inaendelea na jitihada za kupata kauli yake na inafuatilia kwa karibu mwenendo wa sakata hilo.