Thursday, July 17, 2025
spot_img

HIFADHI YA NGORONGORO YAHARIBIWA

RIPOTA PANORAMA

BAADHI ya maeneo yaliyo chini ya Mamlaka ya Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro yemewekewa mahema yanayotoa huduma ya kuhifadhi watalii kwa muda mrefu na yamewekewa miundombinu ya kudumu kinyume na utaratibu wa uwekaji kambi za aina hiyo katika maeneo ya uhifadhi.

Maeneo hayo yamebainika kuwa yana uwezo wa kubeba mahema 76 na yamekuwa yakifanya kazi kwa kipindi cha kuanzia miaka minne hadi kumi, yakiwa na uwezo wa kutoa hifadhi ya malazi kwa watalii 168.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/22, maeneo hayo yaliyo ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro yameharibika kutokana na ujenzi wa mahema na miundombinu ya kudumu kwenye kambi maalumu.

“Maeneo maalumu ya kambi huruhusu wageni kupiga kambi kwa kutumia mahema yasiyo ya kudumu kwa muda wa miezi mitatu hadi sita. Katika ukaguzi wangu nilitembelea maeneo saba ya kambi maalumu ambayo yako chini ya Mamlaka ya Uhifadhi wa Eneo la Ngorongoro,” anaeleza CAG katika ripoti yake.

Anayataja maeneo aliyotembelea kuwa ni Simba B, Ole Kamwanga, Laandama namba moja, Nyati, Acacia namba moja, Tembo B na Lemala kubwa ambayo yana uwezo wa kubeba mahema 76 yenye uwezo wa kulaza watalii 168.

“Katika ziara yangu ya ukaguzi nilibaini kwamba baadhi ya maeneo ya kambi hizo yalikuwa na mahema na miundombinu ya kudumu kwa hadi misimu 10 jambio ambalo ni kinyume na maelekezo ya maeneo maalumu ambayo yanahitaji kambi kuvunjwa baada ya msimu kuisha,” anaeleza CAG katika ripoti yake hiyo.

Katika eneo la Simba B, CAG anaeleza kuwepo kwa kambi ya kudumu inayoendeshwa na Kampuni ya Tyche Limited, East Africa Camps ambayo ina idadi ya mahema 10 yenye uwezo wa kuhifadhi watalii 22 na kwamba kambi hiyo imekuwa eneo hilo kwa miaka 10.

CAG anaeleza kuwa katika eneo la Ole Kamwanga kuna kambi inayoendeshwa na Kampuni ya African Environment Ltd yenye mahema 10 ambayo yana uwezo wa kuhifadhi watalii 25 na kwamba imedumu katika eneo hilo kwa miaka mitano.

Eneo la tatu analolitaja CAG kwenye ripoti yake ni Laandama namba moja ambako kuna Kampuni ya Tortilis Tanzania Limited ambayo ina idadi ya mahema 10 yenye uwezo wa kubeba watalii 22 ambayo imedumu kwenye eneo hilo kwa muda wa miaka 10.

CAG anataja pia eneo la Nyati ambako kuna Kampuni ya Wildlife Guides of Tanzania yenye mahema kumi ambayo yana uwezo wa kuhifadhi watalii 25 na idadi ya miaka ambayo kampuni hiyo imeendesha shughuli zake hapo ni minne.

Kwenye orodha hiyo ya CAG imo pia Kampuni ya Grumet Expeditions Limited ambayo ina mahema kumi katika eneo la Acacia namba moja yakiwa na uwezo wa kuhifadhi watalii 22 na kwamba imekuwa eneo hilo kwa miaka minane mfululizo.

Anaendelea CAG kwa kuitaja Kampuni ya Abercromble and Tent (T) Limited iliyoko eneo la Tembo B ikiwa na mahema 10 yenye uwezo kubeba watalii 22 na idadi ya miaka ambayo imedumu kwenye eneo hilo ni mitano.

CAG anamalizia orodha hiyo kwa kuitaja Kampyuni ya Kuhama Camps/ TNS Hospitality ambayo ina mehama 16 katika eneo la Lemala kubwa, yenye uwezo wa kubeba watalii 30 ikiwa imeendesha shughuli zake eneo hilo kwa miaka mitano.

“Kutohamisha mahema mara kwa mara kutoka kwenye maeneo hayo ya kambi maalumu kuna madhara makubwa kwa wanyamapori na mimea kutokana na uharibifu wa uoto wa asili unaotokana na kuweka mahema kwa muda mrefu,” anaeleza CAG.

Anapendekeza kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa ya Eneo la Ngorongoro kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi ili kuruhusu ufufuaji wa uoto wa asili kwa ajili ya ustawi wa mimea na mazingira bora kwa wanyamapori.

USIKOSE KUSOMA TANZANIA PANORAMA ILI KUZIJUA KWA UNDANI KAMPUNI ZILIZOTAJWA KWENYE RIPOTI YA CAG.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya