Saturday, April 19, 2025
spot_img

SINOTASHIP KUTUMIA BILIONI 6 KUIMARISHA USAFIRISHAJI MIZIGO BAHARINI

RIPOTA PANORAMA

KAMPUNI ya ubia kati ya Tanzania na China (SINOTASHIP) itatumia Shilingi bilioni sita kuimarisha huduma za usafirishaji mizigo katika masafa marefu kwa njia ya bahari.

Matumizi ya fedha hizo yalipitishwa na Bunge wiki iliyopita baada ya kujadili kisha kupitisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Akisoma hotuba hiyo bungeni Dodoma, Waziri na Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, kampuni hiyo imetenga Shilingi bilioni sita ili kuendelea kutoa huduma za usafirishaji wa mizigo kwa masafa marefu kwa njia ya Bahari, kusimamia usalama wa mabaharia, mizigo na meli pamoja na kutoa huduma za uwakala wa meli.

Profesa Mbarawa alisema majukumu yatayotekelezwa na SINATOSHIP kwa mwaka wa fedha 2023/24 ni kuendelea kutoa huduma za usafirishaji wa mizigo kutoka tani 610,774 mwaka 2022 hadi kufikia tani 615,000 kwa mwaka 2023.

Aliyataja majukumu mengine yatakayotekelezwa na kampuni hiyo ni kuendelea kuongeza mapato kwa kushawishi wamiliki wa meli kuongeza idadi ya meli na mizigo itakayoingia bandarini kutoka makasha 63,529 mwaka 2022 hadi kufikia makasha 65,000 mwaka 2023.

Pia kupunguza gharana za uendeshaji kampuni kutoka Shilingi bilioni 13.37 mwaka 2022/23 hadi kufikia Shilingi bilioni 13.01 mwaka 2023/24 na kushirikiana na taasisi za fedha za ndani na nje ya nchi kufanikisha upatikanaji wa mikopo itayowezesha kununua meli moja ya mizigo kwa kutegemea hali ya soko.

Aidha, Bunge lilipitisha matumizi ya Shilingi bilioni 100 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) zitakazotumiwa kutekeleza kazi kumi.

Profesa Mbarawa alizitaja kazi hizo alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake kuwa ni kujenga meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 za shehena ya mizigo na kujenga shipyard kwa ajili ya ujenzi wa meli katika Ziwa Tanganyika.

“Kufanya ukarabati mkubwa wa meli ya MV. Liemba katika Ziwa Tanganyika, kufanya ukarabati mkubwa wa meli ya MT. Ukerewe na MT. Nyangumi katika Ziwa Victoria na kufanya ukarabati wa boti moja ya mwendokasi kwa ajili ya kusaidia kazi za uokoaji, sambamba na usafirishaji watalii wanaotembelea Kisiwa cha Gombe, yenye uwezo wa kubeba abiria kumi katika Ziwa Tanganyika.

“Ujenzi wa meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mabehewa ya mizigo katika Ziwa Victoria, ujenzi wa meli mpya ya mafuta Ziwa Tanganyika na kufanya ukaguzi wa kina wa meli ya MV. Mwongozo Ziwa Tanganyika,” alisema Profesa Mbarawa alipokuwa akisoma hotuba yake.

Akihitimisha kutaja kazi zitakazofanywa na MSCL alisema itaendelea na ufungaji wa mifumo ya TEHEMA katika vituo vya maziwa makuu ambayo ni Victoria, Tanganyika na Nyasa na kufanya upembuzi yakinifu kuhusu biashara ya usafirishaji baharini ili kuwezesha ujenzi wa meli moja baharini.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya