RIPOTA PANORAMA
SHIRIKA la Uwakala wa Meli (TASAC), litatekeleza kazi 14 zitakazogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 71 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Utekelezaji wa kazi hizo ulitangazwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa wizara yake, ambayo Bunge liliijadili na kuipitisha, likiidhisha jumla ya Shilingi 3,554,783,957,000.
Profesa Mbarawa alisema kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, TASAC limetengewa Shilingi bilioni 1.73 zitakazotolewa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Shilingi bilioni 70.905 zitakazotokana na makusanyo yake ya ndani kwa ajili ya kutekeleza kazi hizo 14.
Alizitaja kazi hizo kuwa ni uongezaji wa wigo wa upatikanaji wa mawasiliano katika Ziwa Victoria, ujenzi wa kituo cha kikanda cha kuratibu utafutaji na uokoaji Ilelema, Mwanza (MRCC) na ujenzi wa vituo vitatu vya kitaifa vya utafutaji na uokoaji.
Profesa Mbarawa alisema kazi nyingine zitakazotekelezwa na TASAC ni kununua na kufunga mfumo wa kuwezesha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwenye Ziwa Victoria, kununua boti mbili za utafutaji na uokoaji pamoja na boti moja ya matibabu.
Pia kudhibiti gharama, nauli na tozo mbalimbali za usafiri majini kwa kuzingatia sheria na kanuni ili kuhakikisha tozo hizo zinaleta ushindani kwenye soko na kufanya ukaguzi wa meli za nje zinazokuja katika Bandari za Tanzania Bara na meli zilizosajiliwa nchini ili kuhakikisha zinazingatia viwango vya ubora.
Profesa Mbarawa alisema TASAC itafanya kazi ya kuimarisha mifumo ya TEHEMA kwa ajili ya utoaji wa vyeti vya mabaharia, kuweka mifumo thabiti ya kukabiliana na uchafuzi wa mazingira majini utokanao na meli na kusimamia utekelezaji wa sheria ya usalama wa vyombo vya majini.
āKusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu usafirishaji kwa njia ya maji inayoratibiwa na Shirika la Bahari duniani, uwakala wa ugomboaji na uondoshaji wa shehena zifuatazo: Silaha na vilipuzi, makinikia, wanyama hai kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa wanyamapori, nyara za Serikali na kemikali zinazotumiwa na kampuni za madini,ā alisema Profesa Mbarawa.
Alitaja pia kushirikisha wadau kufanya mapitio na marekebisho ya sheria na kanuni mbalimbali pamoja na kuimarisha mifumo na kukuza matumizi ya TEHEMA katika kudhibiti huduma za usafiri kwa njia ya maji na ufanyaji biashara ya meli.