Wednesday, May 28, 2025
spot_img

SERIKALI KUNUNUA NDEGE YA KUFUNDISHIA MARUBANI

SASA ni rasmi. Serikali itanunua ndege kwa ajili ya kufundishia marubani hapa nchini.

Mafunzo hayo ya urubani yatatolewa katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kilichopo Mabibo jijini Dar es Salaam.

Uamuzi wa Serikali kununua ndege maalumu kwa ajili ya kufundishia marubani umetangazwa bungeni jana na Waziri wa Ujenzi na Uchuikuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Profesa Mbarawa ambaye ameliomba Bunge kuidhinisha Shilingi trilioni 3.57 katika bajeti ya wizara yake ya mwaka 2023/2024, amesema Shilingi bilioni 2.27 kutoka mfuko mkuu wa Serikali ni kwa ajili ya kununua ndege moja ya kufundishia marubani, mafuta na matengenezo ya ndege hiyo ya kufundishia.

Amesema kiasi hicho cha fedha pia kitatumika kununulia vifaa maalumu vya kufundishia wataalamu wa sekta ya anga pamoja na kuendeleza ujenzi wa jengo la maktaba ya NIT.

Aidha, Profesa Mbarawa amesema fungu hilo la fedha litatumika kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa kampasi ya uanzishwaji wa mafunzo ya kituo atamizi cha kuandaa mafundi mahiri kwenye sekta ya usafirishaji majini, mafuta na gesi mkoani Lindi.

Mbali na uamuzi huo wa Serikali, Profesa Mbarawa amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi, Kampasi ya Morogoro itadahili wanafunzi wapya 150 wa ngazi ya cheti na pia itatoa mafunzo kwa wanafunzi 138 wanaoendelea na masomo ya stashahada katika fani za uhandisi ujenzi, umeme na mitambo.

“Kazi nyingine ni kudahili wanafunzi wapya 200na kuendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi 353 wanaoendelea na masomo ya elimu ya ufundi stadi (Vocational Education Training – VET).

“Vilevile, taasisi imepanga  kutoa kozi fupi 10kwa washiriki 400zinazohusisha kozi za umeme wa magari, maopareta wa mitambo ya kazi za ujenzi, matumizi ya “software” katika kufanya kazi za kihandisi, matengenezo ya madaraja pamoja na udereva wa awali na udereva wa magari ya abiria,” amesema Profesa Mbarawa.

Ameitaja mipango mingine iliyopangwa kutekelezwa na wizara yake katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kuwa ni kukamilisha upatikanaji wa usajili wa mafunzo ya elimu ya ufundi stadi ngazi ya VET 3 pamoja na kufanya tathmini ya mafunzo kwa vitendo yanayofanyika viwandani na kwa wanafunzi wa kozi ndefu za Stashahada.

Maeneo mengine ambayo yataguswa na bajeti ya Wizara ya Ujenzi ya mwaka wa fedha 2023/2024 ni Kampasi ya Mbeya ambayo itatoa mafunzo ya kozi nane za matumizi ya teknolojia stahiki ya nguvu kazi katika ujenzi na kwa upande wa Chuo cha Bandari, amesema Serikali imetenga Shilingi bilioni moja kutoka mfuko mkuu wa Serikari kwa ajili ya chuo hicho ambazo zitagharamia ununuzi wa kifaa cha kufundishia kinachofahamika kwa jina la ‘full mission crane simulator.’

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya