Tuesday, December 24, 2024
spot_img

JINSI MALI YA UMMA INAVYOFUJWA

RIPOTA PANORAMA

SEKRETARIETI ya Mkoa wa Simiyu, imenunua gari bovu aina ya Nissan Patrol, GRX 61 kwa Shilingi milioni 188.67 kisha imelitekeleza kwenye karakana.

Gari hilo lilinunuliwa kupitia kwa wakala wa huduma ya ununuzi serikalini (GPSA) na kupelekwa mkoani Simiyu lakini lilifika na kutupwa karakana kwa sababu ya ubovu wa injini.

Hayo yameelezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

“Sekretarieti ya Mkoa wa Simiyu, iliagiza na kupokea gari aina ya Nissan Patrol, GRX 61 yenye thamani ya Shilingi milioni 188.67 kutoka GPSA, lakini lilitelekezwa kwenye karakana kutokana na ubovu wa injini,” ameeleza CAG Kichere kwenye ripoti yake.

Aidha, katika ukaguzi wake, CAG Kichere ameeleza kubaini Sekretarieti za mikoa 15 zililipa Shilingi bilioni 4.95 kwa wakala wa huduma ya ununuzi serikali kwa ajili ya ununuzi wa magari, lakini hadi disemba 2022, magari hayo yalikuwa hayajawasilishwa kwa taasisi zao.

CAG Kichere pia ameeleza kubaini Sekretarieti nne zilizofanya malipo ya Shilingi bilioni 1.02 kwa mabadiliko ya kazi ambayo hayakuidhinishwa.

Wakati huo huo, CAG Kichere ameeleza katika ripoti yake kuwa Sekretarieti ya Mkoa wa Mwanza, ilinunua vifaa vya ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa Shilingi milioni 233.46, lakini vifaa hivyo vilitelekezwa kutokana na kusitishwa kwa ujenzi wa uwanja huo tangu mwezi Juni 2022.

“Hii ilitokana na kutokuwepo kwa mipango na michoro iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) na kutoshirikishwa kwa washikadau wakuu katika uanzishwaji wake, hali iliyosababisha kurekebishwa mara kwa mara kwa miundo ya majengo,” ameeleza CAG.

Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta bila mafanikio Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk. Yahaya Nawanda kupata kauli yake kuhusu hatma ya gari hilo Aidha jitihada za kumpata Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki kuzungumzia ufujaji huo wa mali ua umma zinaendelea.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya