RIPOTA PANORAMA
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, imeielekeza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yaliyoibuliwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kujua kiini chake na kukipatia ufumbuzi.
CCM pia ameielekeza Serikali kutengeneza utaratibu wa ufuatiliaji wa karibu wa changamoto zinazoibuka sehemu mbalimbali nchini ili zisilete madhara kama yaliyotokea Kariakoo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophie Mjema, maelekezo hayo yametolewa leo wakati wa kikao cha kawaida cha chama hicho kilichoketi Dodoma chini ya uenyekiti wa Rais Samia Saluhu Hassan.
Taarifa ya Mjema (pichani juu) imeeleza kuwa kikao hicho kilipokea na kujadili kwa kina masuala mbalimbali ya kitaifa, ikiwemo hatua zinazochukuliwa na Rais Samia na Rais Mwinyi katika utekelezaji wa majukumu yao ya urais ikiwa ni sehemu ya kuendelea kutekeleza na kutafsiri ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020 hadi 2025 kwa vitendo.
Amesema, kamati kuu imempongeza Rais Samia kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya, kukamilisha ujenzi wa Ikulu mpya iliyojengwa Chamwino, Dodoma pamoja na kuzinduliwa kwa Ikulu hiyo.
Mjema amesema Kamati Kuu pia imempongeza Rais Samia kwa kuendelea kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kitaifa pamoja na ujenzi wa mji mpya wa kiserikali katika Jiji la Dodoma.