Monday, December 23, 2024
spot_img

VIFO VYA WAJAWAZITO, WATOTO WACHANGA VYAONGEZEKA, WAZIRI UMMY MWALIMU AWA ‘BUBU’

RIPOTA PANORAMA

VIFO vya akinamama wajawazito vimeongezeka kwa wastani wa kati ya vifo 102 hadi 989 kwa kila vizazi hai 1000 katika halmashauri 20 hapa nchini.

Ongezeko hili la vifo vya akinamama wajawazito limebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka 2021/2022, ikiwa ni ongezeko la juu ya shabaha ya vifo 100 kwa kila vizazi hai 100,000.

Pembeni ya hilo, ripoti hiyo CAG imebainisha kuwa uwiano wa vizazi hai na vifo kwa watoto wachanga havitambuliwi katika halmashauri 20 hapa nchini kutokana na kutopatikana kwa takwimu za uzazi na kwamba kwa miaka ya fedha ya 2020/2021 na 2021/2022 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 6,335 katika halmashauri 20 zilizofikiwa kwa ukaguzi na CAG.  

Kwa mujibu wa CAG, viwango vya juu zaidi vya vifo vya watoto wachanga vimebainika katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambako kiwango cha vifo ni 135 kwa kila vizazi 1000, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya yenye viwango vya vifo 49 kwa kila vizazi 1000.

Wakati CAG akibainisha haya, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye alifikiwa mara kadhaa kwa wito wa simu yake ya kiganjani, ameshindwa kutoa kauli yoyote kuhusu sababu ya kuwepo kwa ongezako la juu la vifo vya akinamama wajazito na watoto wachanga katika halmashauri hizo na hata kitengo cha mawasiliano kwa umma cha wizara yake yake, tangu Mei 15, nacho kimekosa kauli kuhusu jambo hilo.

Waziri Ummy Mwalimu ambaye pia amepelekewa maswali kwa maandishi, ameshindwa kueleza hatua zinazochukuliwa na wizara yake kukabiliana na ongezeko la vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga na pia ameshindwa kujibu swali aliloulizwa na Tanzania PANORAMA Blog, lililohoji sababu ya kuwepo kwa vifo vingi vya watoto wachanga katika halmashauri hizo 20.

Aidha, Waziri Ummy amekosa kauli kuhusu utaratibu unaotumiwa na hospitali za hapa nchini kutunza kumbukumbu za vizazi hai na vifo; na hata alipoulizwa mtizamo wake kuhusu utaratibu unaotumika sasa kutunza kumbukumbu za vizazi na vifo kama unafaa au unapaswa kuboreshwa, alinyamaza kimya.

CAG katika ripoti yake anaeleza kuwa viwango hivyo vya vifo viko juu kuliko shabaha inayotarajiwa ya vifo 30 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa ambavyo vinahitaji kufikiwa ndani ya mpango wa miaka mitano.  

Katika hatua nyingine, CAG ameeleza katika ripoti yake kuwa ukaguzi wake kwenye sekta ya afya umebaini miradi mingi ya vituo vya afya kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa haijakamilika.

“Kwanza kuna miradi ambayo haijakamilika yenye thamani ya Shilingi bilioni 82.95 katika halmashauri 91 na vile vile miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.64 ambayo haijaanza,” inasomeka ripoti hiyo.

Ukaguzi wa CAG pia ulibaini kuwepo kwa miradi iliyokamilika katika halmashauri 16 yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.93 ambayo licha ya kukamilika, haijaanza kutumika.

Ripoti inaeleza zaidi kuwa dawa zenye thamani ya Shilingi bilioni 8.16 zilizoagizwa na halmashauri 10 kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hazikufikishwa kwenye vituo vya afya husika.

Aidha, ameeleza kubaini kuwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikataa kulipa madai ya Shilingi bilioni 11 ya Halmashauri 16 ambayo hayakuzingatia miongozo ya mfuko huo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya