RIPOTA PANORAMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ametoa salamu za pole kwa familia na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kifo cha Rubani Benard Shayo.
Taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii iliyotolewa leo na mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini wa wizara hiyo, John Mapepele, imeeleza kuwa Kapteni Shayo alikuwa mtumishi mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na amekutwa na umauti akiwa mtumishi wa Kampuni ya Frankfurt Zoological Society (FZS.)
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, pamoja na Kapteni Shayo, wengine waliofariki katika ajali hiyo ya ndege iliyokuwa na watu wanne ni Amani Mgogolo na Theonas Nota huku askari mmoja wa uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Evanda Elisha akijeruhiwa na anaendelea kupatiwa matibabu.
Awali Tanzania PANORAMA Blog iliripoti watu wawili kufariki dunia katika ajali hiyo ambao ni Kapteni Shayo na Mgogolo lakini taarifa ya hivi karibuni ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaonyesha idadi wa vifo kuongezeka na kuwa watu watatu.
“Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa anapenda kutoa pole kwa familia na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kifo cha mtumishi mstaafu wa Maliasili na Utalii, Rubani Benard Shayo kutoka Kampuni ya Frankfurt Zoological Society (FZS), Amani Mgogolo na Theonas Nota waliofariki dunia leo Mei 18, 2023 majira ya saa tano na nusu asubuhi wakiwa wanaenda doria kwa kutumia ndege tajwa hapo juu.
“Rubani Shayo na Mgogoro wamefariki dunia papo hapo baada ya kupata ajali wakati wakiruka na ndege hiyo aina ya Cessina 192 5H – FZS, mali ya Kampuni ya FZS katika Kiwanja cha Ndege cha Matambwe kwenye Hifadhi ya Taifa Nyerere wakati askari Mhifadhi Nola amefariki baada ya ndege iliyokuwa ikimkimbiza hospitali kutua uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam,” inaeleza taarifa hiyo.