Tuesday, December 24, 2024
spot_img

VYURA WA KIHANSI KUREJESHWA WOTE KUTOKA MAREKANI MWEZI UJAO

RIPOTA PANORAMA

SERIKALI itawarejesha nchini vyura wote wa Kihansi waliokuwa wamehifadhiwa kwenye maabara nchini Marekani mwezi ujao.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa leo na Waziri wa Nishati, Januari Makamba alipokuwa akijibu maswali aliyoulizwa na Tanzania PANORAMA Blog, ambayo pamoja na mambo mengine yalihusu kumalizika kwa mkataba baina ya Serikali na Kampuni ya Bronx na Toledo ya Marekani wa kuwatunza vyura hao.

Waziri Makamba amesema mkataba wa kuwatunza vyura hao nchini Marekani uliisha Juni, 2020 lakini Serikali ilishindwa kuwarejesha nchini kwa sababu ya uwepo wa janga la UVIKO 19, hivyo iliongeza mkataba huo hadi Juni 2022.

Amesema mpango wa kuwarudisha vyura hao nchini ulianza Disemba, 2012 kwa kurejesha vyura 2,500 na hadi ilipofika 2019 zaidi ya vyura 12,000 walikuwa wamerejeshwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2021/2022; vyura 500 wa kipekee ambao hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani isipokuwa katika Bonde la Kihansi lililopo Tanzania, walisafirishwa na Serikali kwenda kwenye bustani ya wanyama ya Bronx na Toledo iliyopo nchini Marekani ili kuepuka hatari ya kupotea ambayo ilitokana na utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji wa Kihansi, mwaka 1994.

Ripoti ya CAG inaeleza kuwa ingawa haiwezekani kubainisha idadi kamili ya sasa ya vyura hao, Shirika la Umeme (Tanesco) linalipa Dola za Marekani 130,000 kwa mwaka kwa ajili ya kuwatunza huko Marekani.

“Inakadiriwa takribani Dola za Marekani milioni 2.86 zilitumika kwa miaka yote 22 ya kuhudumia vyura. Mwaka 2020/2021 na 2021/2022, Serikali ilifanya malipo ya Shilingi milioni 611.92, sawa na Dola za Marekani 260,000.

“Nimebaini kuwa mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na bustani za wanyama za Marekani ulimalizika Juni, 2020 na kuongezewa muda wa miaka miwili hadi Juni, 2022 japokuwa hakuna mpango wowote wa kurudisha vyura hao Tanzania ikizingatiwa kuwa tayari miaka 22 imepita tangu vyura 500 wapelekwe kwenye bustani za wanyama za huko Marekani,” inasomeka ripoti ya CAG.

Aidha, CAG anashauri Tanesco kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Maliasili na Utalii kuweke mpango mkakati wa kurudisha vyura wa Kihansi ili kuepuka gharama kwa Tanesco.

Waziri Makamba, yeye ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa gharama za awali za kuwahifadhi vyura hao nchini Marekani zililipwa na Benki ya Dunia na Global Environmental Facility.

Amesema Tanesco ilianza kulipa gharama za kuwatunza vyura hao Juni, 2019 na hadi Juni, 2022 ilikuwa imelipa jumla ya Dola za Marekani 385,000 ambazo ni sawa na Shilingi milioni 847, chini ya mradi wa Tanzania Energy Development and Access Project (TEDAP.)

“Kama nchi, tayari tumeishajenga uwezo wa kuhifadhi vyura hawa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Kihansi,” amesema Makamba.

Akifafanua kuhusu kusafirishwa kwa vyura hao kwenda kutunzwa Marekani na mpango wa kuwarejesha nchini, Waziri Makamba amesema; “Ujenzi wa mradi wa bwawa la kufua umeme la Kihansi lenye uwezo wa kufua megawati 180 ulianza mwaka 1993 na kukamilika mwaka 1999 na kugharimu jumla ya Shilingi bilioni 598.

“Mnamo mwaka 1996, kuligundulika vyura wa kipekee ambao hawapatikani sehemu nyingine duniani isipokuwa katika Bonde la Kihansi nchini Tanzania. Vyura hawa huzaa badala ya kutaga mayai kwa kuwa mayai hukaa ndani ya mwili wa chura hadi siku za kuzaa.

“Vyura hawa wanaishi kwenye mazingira ya maji yanayotiririka na kutoa mvuke au ukungu (mist) mwingi sana kutokana nguvu ya maji na walikuwa wapo katika hatari ya kutoweka.

“Kwa hiyo kama nchi tulikabiliana na uamuzi wa aina mbili; kuendelea na ujenzi wa mradi wa umeme na kupoteza vyura au kupata vyote viwili kwa wakati mmoja, yaani kuwalinda vyura hawa wasipotee na kuendelea na ujenzi wa mradi wa umeme,” amesema Waziri Makamba.

Akieleza zaidi, Waziri Makamba amesema ili kuwa na maendeleo endelevu, Serikali iliamua kuwalinda vyura wa Kihansi na kuendelea na ujenzi wa mradi.

“Ili kufikia azma hii, hatua mbili zilichukuliwa ambazo ni kujenga miundombinu ya kuzalisha mvuke au ukungu ili vyura wasife lakini kwa kuwa miundombinu hii haikuwa ya asili ililazimu kuwapeleka vyura 500 kwenye maabara nchini Marekani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kwa hiyo kama nchi tumepata faida kubwa za uwepo wa mradi kwani umekuwa ukisaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika na wenye ubora na kuliingizia shirika mapato ya trilioni 3.4 ukilinganisha na matumizi yaliyofanyika,” amesema Waziri Makamba.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya