RIPOTA PANORAMA
MFUKO wa Bima ya Afya (NHIF) umeyakataa madai ya Shilingi bilioni 6.42 ya gharama za huduma za matibabu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wanachama wa mfuko huo.
Sambamba na hilo, NHIF imeyakataa madai ya taasisi nne yaliyowasilishwa kwa ajili ya kulipwa baada ya kutoa huduma za matibabu kwa wateja wa mfuko huo ambazo ni Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili – Mloganzila.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka wa fedha 2021/2022, Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipeleka madai kwa NHIF ya Shilingi bilioni 44.52 kwa kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wa mfuko huo lakini ilikataa kulipa madai ya Shilingi bilioni 6.42 ambayo hayakuzingatia vigezo vilivyowekwa na mfuko huo.
Katika ripoti hiyo, CAG anaeleza kuwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ilipeleka NHIF madai ya Shilingi bilioni 22.26 lakini katika deni hilo, NHIF ilikataa deni la Shilingi milioni 13 na Taasisi ya Mifupa Muhimbili ilipeleka madai ya Shilingi bilioni 14.53 lakini deni la Shilingi bilioni 1.30 lilikataliwa.
Taasisi nyingine iliyokataliwa sehemu ya madai yake ni Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha ambacho kilipeleka NHIF madai ya Shilingi bilioni 1.62 lakini deni la Shilingi milioni tano lilikataliwa.
Ripoti ya CAG inaeleza kuwa jumla ya madai ya mashirika na taasisi za umma tano kwa NHIF kwa mwaka wa fedha 2021/2022 yalikuwa Shilingi bilioni 92.44 ambapo madai ya Shilingi bilioni 8.84 yalikataliwa.
Aidha, CAG anaeleza katika ripoti yake kuwa madai ya fedha yaliyowasilishwa NHIF kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 yanaashiria kuwepo kwa ongezeko kubwa la madai yaliyokataliwa ikilinganishwa na mwaka wa fedha 2020/2021 ambapo madeni yaliyokataliwa yalitokea kwenye mashirika na taasisi za umma mbili yakiwa na thamani ya Shilingi bilioni 3.87.
Kuhusu sababu za kukataliwa kwa madai hayo alizozibaini kwenye ukaguzi wake, CAG anaeleza kuwa ni kutokana na matukio ya kudai mara mbili, matumizi makubwa ya huduma, kutozingatiwa kwa bei elekezi za NHIF na utoaji wa huduma ambazo hazijaainishwa na mfuko huo.
Sababu nyingine alizozitaja ni kukosekana namba za idhinisho, ukosefu wa maelezo katika huduma zinazodaiwa, kughushiwa kwa saini za wagonjwa, huduma ambazo si sehemu ya kifurushi cha NHIF, makosa ya kukokotoa, matumizi kupita kiasi ya huduma, na kutofuata kanuni za matibabu.
CAG ameeleza kuwa sababu hizo zinaonesha wapo baadhi ya watumishi wanaohusika kutoa huduma za matibabu kwa wanachama wa NHIF ambao hawazingatii taratibu zilizowekwa na zilizokubaliwa kati ya NHIF na hospitali au vituo vya afya katika kutoa huduma.