Vatican
RAIS wa Ukraine, Vlodymyr Zelensky, Jumamosi ya Mei 13, 2023 aliingia makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani, Vatican akitumia gari la kivita na kufanya mazungumzo ya faragha na Papa Francisco.
Rais Zelensky aliingia Vatican majira ya saa 10 jioni akipitia kwenye uwanja uliopo katika ukumbi wa Paulo VI, muda mfupi baada ya kuondoka Ikulu ya Chigi, Jijini Rome, Italia.
Kwa mujibu wa mtandao wa habari za kanisa katoliki wa Vatican, Zelensky alisafiri kwa gari la kivita lililokuwa chini ya ulinzi mkali akipita katikati ya viunga vya Jiji la Rome ambavyo navyo vilikuwa na ulinzi mkali .
Msafari wa Zelensky ulielekea moja kwa moja Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ambako rais huyo alipokelewa na mwakilishi wa nyumba ya kipapa, Mansinyo Leonardo Sapienza akiwa na Balozi wa Ukraine mjini Vatican, Andrii Yurash na Mkuu wa Ofisi ya Rais, Andriy Yermak.
Kabla ya kukutana na Papa Francisco, Rais Zelensky alisalimiana na waandishi wa habari waliokuwa eneo hilo kisha akakaribishwa na Papa kuingia kwenye jumba la kitume kwa mazungumzo ya faragha.
Mazungumzo ya Papa Francisco na Rais Zelensky yalichukua takriban dakika 40 na taarifa fupi iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo na ofisi ya vyombo vya habari vya Vatican, ilieleza kuwa yalihusu hali ya kibinadamu na siasa nchini Ukraine.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa Papa Francisco alimuhakikishia Rais Zalensky kuiweka Ukraine katika maombi yake ya kila siku na kwamba Papa alisisitiza hitaji la dharura la ubinadamu kwa watu dhaifu wa Ukraine.
Baada ya mkutano wake huo na Papa Francisco, Rais Zelensky alikutana na Katibu wa Vatican anashughulikia uhusiano na mataifa pamoja na mashirika ya kimataifa, Askofu Mkuu, Paul Gallagher. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Kardinali Pietro Parolin.





