RIPOTA PANORAMA,
Moshi, Kilimanjaro
Wanafunzi wawili wa shule ya Sekondari Kisomachi iliyopo Kata ya Vunjo Mashariki, Tarafa ya Vunjo Kusini, Wilaya ya Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wamefariki dunia baada ya kukosa hewa wakatoa maharage kwenye tenki linalotumika kuyahifadhi.
Wanafunzi hao, Godwin John na Edson Mosha wote wana umri wa miaka 17 na walikuwa wanasoma kidato cha nne, walifariki dunia ijumaa jioni.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa vyombo ya habari iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa (ACP), Simon Maigwa, wanafunzi hao waliofariki dunia baada ya kuingia kwenye tanki hilo linalotumika kuhifadhia maharage ya shule.
Kamanda Maigwa amesema wanafunzi hao walitolewa kwenye tenki hilo na kukimbizwa Kituo cha Afya cha Kirua, Vunjo ambako ilibainika kuwa walikuwa wameishafariki.
Amesema watumishi watatu wa shule hiyo wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi akiwamo mwalimu mkuu, mwalimu wa zamu na mtunza stoo.
Kamanda Maigwa amesema miili ya wanafunzi hao imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa Mawenzi kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.