Monday, December 23, 2024
spot_img

KASISI MACKENZIE ANAPOHUBIRI ELIMU NI USHOGA, MADAKTARI KUMKUFURU MUNGU

MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA

PAUL Nthenge Mackenzie, Kasisi wa dhehebu la Kikristu nchini Kenya anayeongoza Kanisa la Good News International, mahubiri yake kwa maelfu ya watu waliojisali kwenye ukurasa wake wa Facebook na wanaoangalia chaneli yake ya You Tube yanakinzana kwa kiasi kikubwa na mwenendo wa kawaida wa maisha ya watu.

Mackenzie, ambaye sasa anakabiliwa na kesi mahakamani akituhumiwa kusababisha vifo vya zaidi ya wafuasi wake 110 anaodaiwa kuwaelekeza wafunge kula na kunywa hadi wafe ili wakaonane na Mungu kabla mwisho wa dunia haujawadia, katika mahubiri yake yanayopatikana kwenye chaneli yake ya You Tube na kwenye ukurasa wake wa Facebook, anawafundisha wafuasi wake kuwa elimu rasmi ni ushetani na hutumiwa kupora fedha.

Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) limeripoti kuwa katika mahubiri yake Kasisi Mackenzie, anawafundisha maelfu ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii kuwa elimu inaendekeza mapenzi ya jinsia moja kwa kufundisha program za elimu ya ngono na kwamba madaktari wanamtumikia Mungu tofauti.

Kwa mujibu wa BBC, Kasisi Paul Nthenge Mackenzie ambaye kabla ya kukamatwa alipata kudai kuwa alilifunga kanisa lake miaka minne iliyopita baada ya kufanya kazi ya kueneza mafundisho yake kwa watu kwa takriban miongo miwili, imebainika katika kipindi hicho, mahubiri yake yalikuwa yanapatikana mtandaoni.

“Wanajua elimu ni mbaya lakini wanaitumia kujinufaisha. Wale wanaouza sare, wanaoandika vitabu, wale wanaotengeneza kalamu, kila aina ya takataka, wanatumia pesa zako kijitajirisha huku wewe ukiwa masikini,” hayo ni maneno ya Kasisi Mackenzie kwa wafuasi wake.

Kasisi Mackenzie ambaye mwaka 2017 na 2018 alipata kukamatwa kwa kuhimiza watoto wasiende shule kwa kile alichokuwa akieleza kuwa elimu haitambuliki kwenye Biblia, pia amekuwa akiilaani na katika mahojiano aliyopata kuyafanya na Gazeti la National la Kenya alisema; “Niliwaambia watu elimu ni mbaya, watoto wanafundishwa kuhusu mapenzi ya jinsia moja.”

Amehubiri pia kuhusu urembo kwa wanawake na madaktari kumtumia Mungu kinyume na inayotakiwa kwa kuwahimiza akina mama kuepuka kutafuta matibabu wakati wa kujifungua na kutowachanja watoto wao.

Anaungwa mkono na wafuasi wake kwani katika moja ya video zilizo kwenye mtandao wake, anaonekana mwanamke mmoja akisimulia jinsi alivyosaidiwa kujifungua mtoto kwa njia ya maombi bila kuhitaji upasuaji.

Mwanamke huyo anaeleza kuwa baadaye alipata msukumo kutoka kwa roho mtakatifu ili kumwonya jirani yake dhidi ya kumchanja mtoto wake, kisha Kasisi Mackenzie anamuunga mkono kwa kueleza kuwa chanjo siyo lazima na kwamba madaktari huwa wanamtumikia Mungu tofauti.

Kasisi Mackenzie pia anawaonya wanawake kuhusu kusuka nywele zao, kuvaa wingi kichwani na au kuvalia mapambo.

BBC inamkariri Kasisi Mackenzie kwenye moja ya mikusanyiko ya wafuasi wake; akihubiri kwa sauti ya shauku mbele ya mkusanyiko mkubwa wa watu kuwa ushindi wa vita yao upo karibu hivyo asitokee mtu akarudi nyuma.

Kwenye bango moja lililopo katika skrini inayoonyesha mafundisho yake mtandaoni linasomeka, “Tunakaribia kushinda vita… mtu yeyote asirudi nyuma, safari inakaribia kukamilika.”

Video nyingine kwenye chaneli ya You Tube ya kanisa lake inatanguliwa na maneno ‘End time kids’ na inawaonyesha watoto wadogo wakitoa shuhuda mbalimbali zinazotokana na mafundisho yake.

Katika kipindi kinachoaminika Kasisi Mackenzie alikuwa amefunga kanisa lake na kusitisha mafundisho yake, uhalisia wa hili ni kwamba kasisi huyo alikuwa akiendelea kuwahubiri maelfu wa wafuasi wake mtandaoni na moja ya mada zilizoko kwenye mafundisho yake ya mtandaoni zinatahadharisha watu kuhusu maangamizi ya ulimwengu yanayokuja.

Video nyingine za Kasisi Mackenzie zinamuonyesha akiwatoa mapepo wafuasi wake na hasa wanawake ambao wanajigaraza sakafuni wakati yeye akiwa ‘anakabiliana na nguvu za mapepo.’

Ingawa haijajulikana hasa Kasisi Mackenzie alirekodi lini video hizo, yapo marejeo ya tukio la Januari, 2020 jijini Nairobi ambalo linakinzana na kauli yake kuwa alisitisha shughuli zake mwaka 2019.

Kwa upande mwingine, BBC inaripoti kuwa ingawa hakuna ushahidi wa moja kwa moja uliopatikana ukimuonyesha Kasisi Mackenzie akiwaamuru wafuasi wake wafunge kula na kunywa, wafuasi wa zamani wa kanisa lake waliohojiwa walieleza kuwa walilazimika kufunga kama sehemu ya kufuata mafundisho yake na katika mafundisho yaliyo kwenye baadhi ya video zake, kuna ujumbe unaojirudia mara kwa mara ukiwasihi wafuasi wake kutolea sadaka kile wanachokiamini ikiwa ni pamoja na maisha yao.

Yeye mwenyewe Kasisi Mackenzie alipofanya mahojiano na Gazeti la Daily National la Kenya siku chache kabla ya mkasa wa vifo vya madazani ya wafuasi wake kuibuliwa, alikanusha kuwalazimisha kufunga kula na kunywa ili wafe. 

 KASISI MACKENZIE NA ALAMA ZA SHETANI NA NJAMA ZA KIMATAIFA.

Mpaka sasa, haina shaka kuwa Kasisi Mackenzie ndiye mhubiri mwenye mahuburi yenye utata zaidi nchini Kenya yakiwemo yanayohusiana na utimilifu wa unabii wa Biblia kuhusu siku ya hukumu na hata maudhui ya kanisa lake mtandaoni yanaangazia machapisho kuhusu mwisho wa dunia, maangamizi yanayokaribia na hatari zinazodhaniwa kuwa za sayansi.

Kanisa lake limekuwa likitoa onyo la mara kwa mara kuhusu kile linachokiita nguvu ya kishetani yenye uwezo na ambayo inasemekana imejipenyeza kwenye ngazi za juu zaidi za mamlaka kote duniani.

Katika mahubiri yake, Kasisi Mackenzie hurejea mara kwa mara maneno, ‘New World order,’ nadharia kuhusu njama ya wasomi wa kimataifa kuleta Serikali ya kimabavu ulimwenguni kuchukua nafasi ya mataifa.

Kasisi Mackenzie pia amekuwa akihubiri mashaka aliyonayo kuhusu teknolojia ya zama za sasa na alianza hili kwa kuonyesha mashaka yake kwa Serikali ya Kenya alipodai kuwa ina mpango wa kutoa namba ya kipekee ya utambulisho kwa raia kupata huduma za Serikali; namba ambayo ilikuwa na alama ya mnyama.

.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya