MASHIRIKA YA HABARI YA KIMATAIFA
WATU 130 waliofariki dunia baada ya kukumbwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha siku ya Mei 4, usiku katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa Rwanda wamezikwa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Rwanda na mashirika ya habari ya kimataifa, watu hao walizikwa katika Mji wa Rubavu ulioko Magharibi ya Rwanda na mazishi yao yaliongozwa na Waziri Mkuu, Dk. Edouard Ngirente.
Akizungumza wakati wa mazishi, Dk. Ngirente alisema idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwa sababu bado miili mingine ya watu wanaohofiwa kufariki katika mafuriko hayo inaendelea kutafutwa.
“Kuna watu ambao tunaendelea kuwatafuta na huenda idadi ya waliokufa ikaongezeka. Kusema ukweli hili ni janga lililoiangukia nchi yetu kwani maji mengi ya mvua yaliyomomonyoa udongo na kusababisha nyumba kuwaangukia watu.
“Tunatambua uchungu na matatizo mnayoyapata, Serikali itajitahidi kuwapa msaada kadri inavyowezekana na mimi niko hapa kumwakilisha Rais ambaye kuanzia jana amekuwa akiwapa taarifa kuhusu msimamo wa Serikali,” alisema Dk. Ngirente.
Watu hao hao walifariki dunia baada ya kunyesha mvua kubwa iliyosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Kwa mujibu wa Sauti ya Amerika (VOA), baadhi ya watu waliopoteza ndugu zao walieleza kuwa waliofariki dunia walifunikwa na vifusi vya nyumba na kingo za mlima.
“Kifusi kilianguka na kutufunika mimi na mume wangu na mtoto wetu, nilipozinduka nikaona mimi kichwa changu bado kinaonekana ndipo mume wangu akaanza kunivuta lakini tulipoangalia vizuri alipokuwa amelala mtoto wetu tukakuta yeye kimemfunika kabisa.
“Tukajaribu kuondoa matofali lakini tulishindwa, mimi nikapanda ukuta kwenda nje kuomba msaada,” alisema mmoja wa watu walionusurika.
Gashonga Jean Marie Vianney ambaye alinusurika katika mkasa huo alisema amepoteza watoto watatu wa kike.
“Kifusi cha mlima kilimeguka na kuangukia nyumba yetu upande wa juu karibu na chumba cha watoto wangu wa kike na wa kiume na mara moja kikafunika chumba cha watoto wangu watatu wa kike waliokuwa pamoja ambao walifariki papo hapo.
“Upande wa chumba cha wavulana wao waliweza kujivuta wakatoka na ndiyo waliomsaidia mama yao kumuondoa kwenye kifusi kilichokuwa kimemfunika,” alisema Vianney.
Tayari Serikali ya Rwanda imepeleka msaada wa tani 60 za chakula kwa waathirika ambao wengi wao wamehifadhiwa kwenye majengo ya shule na makanisa na baadhi wamepewa hifadhi na jamaa na marafiki.
Sambamba na hilo, Serikali ya Rwanda imeanza kuzihamisha familia 137 kutoka maeneo hatarishi na imewataka raia wake wanaoishi maeneo yaliyo jirani na kingo za milima mirefu kuhama kwenye maeneo hayo.
Naye Waziri wa Usimamizi wa Masuala ya Dharura wa Rwanda, Marie Solange Kayisire aliwataka watu wote kuwa katika hali ya tahadhali na wanaoishi karibu na kingo za milima mirefu kuhama ili wasije kuangukiwa na kingo za milima.
Mwaka 2020, zaidi ya watu 80 walifariki dunia nchini Rwanda kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa na tangu wakati huo Serikali ya Rwanda imekuwa ikifanya kazi ya kuwahamisha watu wenye makazi katika maeneo hatarishi na kuwajengea makazi mengine mapya.
Hii ni mara ya kwanza kwa Rwanda kupoteza idadi kubwa ya raia wake kwa usiku mmoja kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.