GENEVA, Uswisi
KAMPUNI ya masuala ya usalama ya SICPA inayofanya kazi katika maeneo mbalimbali duniani, imehukumiwa kulipa Dola za Marekani milioni 90.6 baada ya kutiwa hatiani na mahakama kwa mamosa ya mbalimbali ikiwemo za kutoa rushwa.
SICPA ambayo shughuli zake zipo pia Tanzania ilitiwa hatiani Aprili 27, mwaka huu nchini Uswisi, ambapo taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Uswisi ilisema mahakama nchini humo imeikuiku na makosa ya jinai katika biashara.
Kutokana na hukumu hiyo, Mamlaka ya Mapato (TRA) na Shirika la Viwango (TBS) ambazo ni taasisi za Serikali zinazofanya biashara na kampuni hiyo, zimepewa angalizo kuwa makini na kuona kama kampuni hiyo bado inapaswa kuendelea kufanya kazi na mamlaka hizo mbili za nchi.
SICPA imekuwa ikifanya kazi na TRA na TBS katika mambo mbalimbali yakiwemo ya nyaraka za ukusanyaji wa kodi na nembo za ubora.
Pamoja na SICPA, Mahakama ya Uswisi ilimtia hatiani aliyekuwa Meneja Mauzo wa SICPA na kumuhukumu kifungo cha nje cha siku 170 kutokana na kesi hiyo.
Mahakama ya Uswisi ilibaini kuwa SICPA ilikiuka taratibu kwa makusudi, ikiwemo udhaifu katika kusimamia kanuni, ukosefu wa umakini katika menejimenti ya majanga na kushindwa kufuata taratibu za kibiashara.
Pia, mahakama ilimwagiza Ofisa Mtendaji Mkuu wa SICPA kuwajibika kwa kugharamia gharama za kesi lakini ikisitisha uchunguzi wa jinai dhidi yake.
MWENENDO WA UCHUNG\UZI
Mwendesha Mashitaka Mkuu alianzisha uchunguzi dhidi ya SICPA ambayo hujihusisha na biashara ya usalama wa fedha na nyaraka duniani, tangu mwaka 2015 kutokana na maombi ya kisheria.
Uchunguzi huo ulihusisha malipo yaliyohusisha tuhuma za rushwa katika nchi za Brazil, Venezuela na Colombia. Katika uchunguzi huo, aliyekuwa Meneja Mauzo wa SICPA alituhumiwa kuwahonga baadhi ya maofisa wa juu katika nchi za Venezuela na Colombia kati ya mwaka 2009 na 2011.
Kampuni hiyo pia imekuwa ikilengwa katika uchunguzi wa aina mbalimbali kuhusiana na rushwa katika biashara; ambapo mwaka 2021 ililazimika kulipa kiasi cha CHF 135 milioni kumaliza tuhuma za ukiukaji sheria nchini Brazil.
SICPA ilianzishwa mwaka 1927 mjini Lauseanne na mmiliki wake alikuwa Maurice Amon, kwa lengo la kuuza mazao ya biashara ya wakulima wa Uswisi lakini imekuwa ikizongwa na tuhuma za rushwa katika biashara.