RIPOTA PANORAMA, Tanga
WANACHAMA wa Jumuiya ya Khoja Shia Isinaather Jamaat (KSIJ) na watu wanaopatiwa msaada wa kujikimu kimaisha na jumuiya hiyo iliyopo Mkoa wa Tanga wamemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aingilie kati mgogoro unaotishia uwepo wake ili kuinusuru isivunjike na kuepusha uvunjifu wa amani.
Wamesema wanamuomba Waziri Mkuu Majaliwa aliamuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga litoe taarifa ya uchunguzi lilioufanya kuhusu mgogoro wa jumuiya hiyo na aviagize vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomuandama Mwenyekiti wa KSIJ Tanga, Hussein Walji.
Wakizungumza na Tanzania PANORAMA Blog kuhusu sintofahamu iliyojitokeza kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kuufungia kabatini uchunguzi lilioufanya kuhusu mgogoro wa KSIJ Tanga na kauli iliyotolewa na Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa kuwa Serikali huwa inashughulikia migogoro ya dini kwa siri, wamesema ukimya wa polisi umewanyong’onyeza na kwamba Serikali aingalie upya uamuzi wake wa kuweka usiri kwenye tuhuma za jinai zinahusu jumuiya za kidi.
“Tumemsikia Waziri Mkuu akiwa bungeni Jijini Dodoma akiwaagiza polisi wafanye uchunguzi wa watu walioteswa na au kuuawa wakituhumiwa kuingia kwenye hifadhi. Tunaamini polisi hawawezi kudharau agizo hilo la Waziri Mkuu, watalifanyia kazi na kwa vile ni mfuatiliaji tunaamini wakimwambia walivyofanya kazi, yeye atawaambia watanzania.
“Tunamlilia baba yetu Waziri Mkuu sisi watu masikini ambao hatuna kauli maana hata tukisema, Walji anatufungulia kesi polisi, wanatuita wanaanza vitisho vyao. Tunamuomba Waziri Mkuu kama alivyowaagiza polisi kufanya uchunguzi kwa watu walioteswa na wengine kuuawa hifadhini, awaagize polisi wa makao makuu, amwambie Mkuu wa Polisi atume watu wake waje wachunguze na hiki kinachoendelea hapa Tanga.
“Tunachomuomba ni polisi wa kutoka juu siyo hawa wa hapa kwetu ambao wametunyong’onyeza sana. Tangu walipofanya uchunguzi tena waliwaita baadhi ya wanajumuiya wenzetu kuwahoji wakawaambia ukweli wote lakini mpaka leo huo uchunguzi walioufanya wanao kabati, sisi tunaumia.
“Hizi fedha zinazoliwa na anazo tudhulumu huyu Walji siyo zake za mfukoni ni za wacha Mungu waliochanga kutusaidia masikini na pia kwa ajili ya maendeleo ya jumuiya. Hivi mtu anachukua uongozi kwa nguvu halafu anaanza kutudhulumu masikini kama sisi, anakwenda benki anachota mamilioni ya jumuiya kisirisiri akisaidiana na rafiki zake, uchunguzi wamefanya lakini wamekaa nao kimya, wananchi tueleweje?” alisema mmoja wa wanajumuiya waliozungumza na PANORAMA.
Mwanajumuiya mwingine wa KSIJ Tanga aliyezungumza na Tanzania PANORAMA alisema kilio chao kwa Waziri Mkuu Majaliwa ni kuinusuru jumuiya isivunjike kwa sababu imekuwa msaada mkubwa kwa watu inaosawaidia licha ya uongozi wake wa sasa kujihusisha na vitendo vya ukosefu wa maadili.
“Hapa Tanga wamemshindwa Walji, tunaamini viongozi wetu wakuu ndiyo wanaoweza kutusaidia kwa sababu wamesaidia wananchi wenzetu wengi. Hatuna uwezo wa kumfikia Waziri Mkuu kumwambia tatizo lililopo hapa lakini najua kwa sababu anafuatilia vyombo vya habari na anao wasaidizi wake watasikia kilio chetu mkikiweka hadharani.
“Hii jumuiya haipaswi kufa kwa sababu ya mtu mmoja ambaye kwanza hakuna aliyemchagua na wote hata polisi wa hapa Tanga wanajua hivyo. Historia yake inajulikana huyu mtu na siyo kwamba hii ni mara yake ya kwanza kuwa kiongozi wa jumuiya hii, alishawahi kuwa kiongozi huko nyuma akasababisha mgogoro wa fedha, akaombwa ripoti hakutoa.
“Hivi wewe unakuwa na mtu mmoja ndiye mwenyekiti, katibu ni yeye na mwekahazina ni yeye huyo huyo na huyo mtu hakuna aliyemchagua. Serikali ya mkoa ipo lakini nayo haiheshimu, hizo hesabu za kila robo ya mwaka hapeleki Serikali ya mkoa kama sheria inavyotaka lakini wanamwangilia tu halafu wanasema mambo ya dini ni siri, yaani wanafanya siri kwenye mambo ya kihalifu?” amesema.
Kwa muda mrefu sasa watu wanaosaidiwa kujikimu kimaisha na KSIJ Tanga wamekuwa wakilia kukosa chakula na wengine kulazimika kuwa ombaomba kwa wasamaria wema kwa kile wanachodai Mwenyekiti wao Walji amekuwa akiwadhulumu fedha ambazo huwa wanapatiwa na jumuiya hiyo kujikimu na kwamba yeye na washirika wake wamekuwa wakitishia hali ya amani na usalama ndani ya jumuiya ikiwemo kuwafukuza kwa aibu wawakilishi wa Jumuiya ya Afrika ambayo ni jumuiya mama waliotumwa kwenda kutatua mgogoro.
Walji anadaiwa kupoka uenyekiti wa jumuiya hiyo na kuiongoza kiimla, bila msaidizi na badala yake anashirikiana na maswahiba wake wanaodaiwa kuwa na rekodi zenye shaka na hasa kutishia watu na kujitapa kuhusika na matukio ya kihalifu.
Aidha, Walji anadaiwa kuwadhulumu baadhi ya wahitaji kwa kuwasainisha vocha zinazoonyesha wamepokea kiasi kikubwa cha fedha huku akiwapatia pungufu ya zile alizowasainisha.
Inadaiwa Septemba 19, 2022 Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa aliuandikia barua uongozi wa Walji akiutaka kufika ofisi kwake kwa ajili ya kuzungumzia tuhuma na malalamiko anayoelekezewa, hata hivyo Walji alipuuza wito huo.
Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kihampa alipoulizwa alisema mambo ya jumuiya za dini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi na heshima ya jumuiya za aina hiyo na huyashughulikia kwa usiri.
Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Henry Mwaibambe yeye alisema anafuatilia lilipo faili la mgogoro huo kwani uliporipotiwa alikuwa hajahamishimiwa katika mkoa huo.
Hata hivyo, wasaidizi wake walieleza kuwa jalada hilo walikwishalifikisha mezeni kwake na aliita baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga kuzungumza nao kuhusu hilo lakini Tanzania PANORAMA imeshindwa kupata kauli yake kama alivyoahidi kwani kila anapotafutwa; awali simu ilipokelewa na msaidizi wake aliyeeleza kuwa yupo likizo na siku za karibuni simu yake inaita lakini haipokelewi.
Inadaiwa polisi mkoani Tanga walifanya uchunguzi wa mgogoro huo na kubaini mambo kadhaa ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za KSIJ Tanga lakini badala ya kuchukua hatua, faili hilo liliwekwa kando.
Walji mwenyewe hajakanusha wala kukubali tuhuma hizo na badala yake awali aliomba kukutana na Tanzania PANORAMA Blog kwa mazungumzo ya mezani lakini alipoelezwa kuwa huo siyo utaratibu sahihi wa kazi za mwandishi wa habari, alianza kutuma picha zinazomuonyesha akiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo waliopo madarakani na waliostaafu.
Aidha, Walji amekuwa akitumia wanasheria wake kuitisha Tanzania PANORAMA ili isiendelee kuripoti habari zinazomuhusu na katika hatua ya kushangaza, maafisa wa polisi waliingilia kati suala hilo kwa kuwaita na kuwahoji waandishi wa PANORAMA kuhusu habari za Walji na kutaka kutajiwa vyanzo vyake vya habari na kupewa vielelezo vilivyopo ya habari hiyo.