Tuesday, December 24, 2024
spot_img

MGOGORO TANGA POLISI WANYAMAZA KIMYA

RIPOTA PANORAMA

HALI ya sintofahamu imetamalaki baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kuukalia kimya mgogoro wa wanajumuiya wa Khoja Shia Ithinaasheri Jamaat (KSIJ) wanaoshutumiana na kutuhumiana kwa mambo mbalimbali yakiwemo ya kijinai.

Mbali ya hilo, Tanzania PANORAMA Blog imekuwa katikati ya misukosuko tangu ilipoanza kuripoti mgogoro huo, ikiwemo kuitwa na kuhojiwa na vyombo vya usalama na pia kutishwa na wanasheria wa Mwenyekiti wa KSIJ Tanga, Hussein Walje.

Ikiwa ni zaidi ya miezi miwili sasa tangu Tanzania PANAROMA Blog kuripoti kuhusu hali hiyo na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kusema linafuatilia huku likiahidi kutoa kauli baada ya kuliona faili ya uchunguzi ambalo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP), Henry Mwaibambe alisema halijaliona ingawa PANORAMA inazo taarifa kuwa lilikwishafikishwa mezani kwake, hadi sasa yupo kimya.

Kwa mara ya kwanza, Tanzania PANORAMA iliripoti kuwepo kwa mgogoro kwenye Jumuiya ya KSIJ Tanga mapema Februari, mwaka huu, ambao chanzo chake ni uongozi wa kiimla na ufisadi wa mali za jumuiya hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wanajumuiya hiyo na nyaraka ambazo Tanzania PANORAMA imeziona, wanajumuiya zaidi ya 40 wa KSIJ Tanga walitia saini waraka wa kutokuwa na imani na mwenyekiti wa Jamaat hiyo, Hussein Walje wakimtuhumu kuiendesha kiimla, kudhulumu fedha za misaada za watu masikini wakiwemo wajanae na walemavu ambao huwa anawapatia kiasi kidogo cha fedha za misaada na kuwalazimisha kusaini nyaraka zinazoonyesha wamepokea kiasi kikubwa cha fedha na kukiuka taratibu za uchukuaji fedha za jumuiya zilizohifadhiwa benki.

Tuhuma nyingine anazoelekezewa Walje ni kutumia uwezo wake wa kifedha pamoja na washirika wake kuwashughulikia wakosoaji wake ikiwemo kuwafungulia kesi za uongo polisi na kuwatisha kwa kutumia majina ya viongozi.

Katikati ya tuhuma hizo, baadhi ya wanajumuiya waliibua hoja ya uadilifu kwa Walje kuwa hafai kuwa kiongozi wa jumuiya hiyo, kwa kurejea mashtaka yaliyopata kumkabili mahakamani kabla ya kukutwa na hatia ya wizi wa friza kwenye kesi ya jinai namba 272 ya mwaka 2019 iliyosikilizwa Mahakama ya Mwanzo Tanga Mjini ambayo ilimuhukumu kifungo cha nje cha miezi sita.

Walje alishtakiwa mahakamani kwa kukutwa na friza alilodaiwa kuliiba katika duka la mfanyabiashara mwenzake na katika hukumu yake, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Tanga Mjini, S. B Odeyo alisema utetezi uliotolewa na Walje mahakamani hapo haukuwa wa kweli bali wa kughushi na kwamba kughushi huko kulikofanywa na Walje kwenye nyaraka alizowasilisha mahakamani kunaweza kumfanya ashtakiwe kwa kosa la kughushi.

Tanzania PANORAMA ilimtafuta Walje na kumuuliza kuhusu tuhuma hizo naye alishindwa kukanusha wale kukubali na badala yake alisema hayo atayazungumzia atakapokuwa ameketi kitako ofisini kwake na Tanzania PANORAMA.

Kwa nyakati tofauti, baada ya Tanzania PANORAMA kuripoti habari zinazomuhusu, Walje aliwatumia wanasheria wake kuitisha Tanzania PANORAMA na aidha, alikuwa akituma picha mbalimbali akiwa na viongozi wa Serikali wa sasa na waliostaafu wakiwemo baadhi ya viongozi wakuu wa kitaifa na muda mfupi baadaye anazifuta.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga (RPC) Kamishna Msaidizi (ACP) Henry Mwaibambe, awali alipozungumzia mgogoro huo alikana kuujua na kueleza kuwa hata yeye taarifa za kuwepo kwake alizisikia kwenye mitandao.

“Hata mimi nimesoma tu kwenye mtandao kuhusu hizo taarifa lakini mimi binafsi sijapata taarifa hizo. Hapa ndiyo ninataka nifuatilie, labda niulize kama walileta malalamiko lakini mimi binafsi sijalipata hilo. Unajua RPC ni ofisi labda kuna taarifa zilifika mimi nikiwa sijafika. Ngoja nifike hapo maana saa hizi ndiyo natoka kwenye msiba kwa hiyo kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu sijajua lakini tumepokea hizo taarifa, tunazifuatilia, tunachunguza kujua ukweli, kiini cha mgogoro ni kitu gani. Nipe muda kidogo niongee na OCD,” alisema RPC Mwaibambe.

Wakati RPC Mwaibambe akisema hayo, Tanzania PANORAMA ilikuwa na taarifa za uhakika kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga lilifanya uchunguzi kuhusu mgogoro huo baada ya Walje kuwashtaki baadhi ya wanajumuiya waliokuwa wakitaka aachie ngazi na kubaini mambo kadhaa yakiwemo mambo mazito kabla ya kuliweka kapuni faili hilo kwa kile kinachodaiwa ni maagizo kutoka juu.

Siku chache baadaye RPC Mwaibambe aliliambia Tanzania PANORAMA kuwa faili la kesi hiyo halijafika ofisini kwake hivyo amemuagiza Kamanda wa Makosa ya Jinai wa Mkoa wa Tanga (RCO) kulisaka na kulifanyia kazi kikamilifu.

“Wanalitafuta hilo jalada nataka waniletee nilione, huyu RCO aliyepo ni mgeni ana kama mwezi mmoja. Nitakupa majibu nikishaliona lakini kama kuna mtu anatishia watu, mimi nawapenda sana watu wa aina hiyo, napenda kushughulika nao, hakuna mtu aliye juu ya sheria. Taarifa nimepata, acha nione faili. Tutafanya kazi yetu,” alisema Kamanda Mwaibambe.

Wakati Kamanda Mwaibambe akisema hayo, taarifa ilizopata Tanzania PANORAMA kutoka ndani ya ofisi yake zilieleza kuwa aliliitisha faili la uchunguzi wa KSIJ Tanga na kupelekewa mkononi na baada ya kulisoma aliita baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Tanga kuzungumza nao kuhusu suala la mgogoro wa KSIJ Tanga lakini Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilikuwa ikiripoti suala hilo hakuiita.

Tangu wakati huo, Tanzania PANORAMA imefanya jitihada kubwa za kumpata Kamanda Mwaibambe kuzungumzia hilo kama alivyoahidi pasipo mafanikio na badala yake imekuwa ikikutana na misukosuko ya hapa na pale ikiwemo kuhojiwa na vyombo vya usalama na aidha kutakiwa kutoa vielelezo au ushahidi ilionao kuhusu sakata hilo.

USIKOSE KUPERUZI TANZANIA PANORAMA KESHO KUSOMA KILICHOJIFICHA NYUMA YA SAKATA HILI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya