RIPOTA PANORAMA
Moshi, Kilimanjaro
JESHI la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, linafuatilia taarifa za kuwepo watumiaji na wauza wa dawa kulevya, pamoja na watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja katika baa maarufu iliyopo mjini Moshi, inayofahamika kwa jina la Moshi Central Club.
Akizungumza na Tanzania PANORAMA Blog leo, Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema baa hiyo inapakana na eneo ambalo hukaa wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao lakini taarifa za kuwepo kwa watu wanaojihusha na uuzaji wa dawa za kulevya, kutumia dawa hizo na wale wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja zilikuwa hazijamfikia na kuahidi kuzifutilia.
RPC Maigwa ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu kuhusu barua aliyoandiikiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ikimuomba kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya watu wanaojihuisha na uuzaji wa dawa za kulevya, kutumia dawa hizo na wale wanaodaiwa kujihusisha na mapenzi moja katika eneo hilo.
“Hili sijalisikia, ila eneo hilo huwa tunawakamata sana hawa wanawake wanaouza miili yao, machangudoa, huwa wanakaa upande wa pili wa baa hiyo na wakiona gari letu la polisi huwa wanajificha, lakini hiyo baa ipo hapa mjini, acha tufuatilie,” alisema RPC Maigwa.
Kwa mujibu wa barua ambayo ameandikiwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona, inaeleza kuwa katika Mji wa Moshi, Kata ya Mawenzi kwenye kiwanja kinachomilikiwa na Chama Kikuu cha Ushirika, Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU), pamejengwa klabu moja na usiku inayoitwa Moshi Central Club.
Barua hiyo inaeleza kuwa hali ya usalama kwenye club hiyo si nzuri na kuna matukio ya mara kwa mara ya uvunjifu wa amani ambayo huhatarisha usalama wa raia na mali zao hasa wale wanaofika kwa ajili ya kupata huduma ya chakula na vinywaj.
“Mheshimiwa mkuu wa mkoa, mbali na matukio hayo, klabu hiyo imegeuka kuwa maficho ya wahalifu wa kila aina, wakiwamo wauzaji na watumiaji wa mihadarati (dawa za kulevya) pamoja na wanaume wanaodaiwa kuwa katika mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja, maarufu kama mashoga.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, wanaume hawa walioko kwenye mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja wamekuwa kero kubwa kwa wateja wanaofika kwenye klabu hiyo kutokana na matukio ya aibu wanayoyafanya mbele ya kadamnasi,” inasomeka barua hiyo ambayo Tanzania PANORAMA Blog imeiona.
Aidha, inasomeka zaidi kuwa mashoga hao wamekuwa wakiwavizia wateja wanaokwenda kujisaidia na kuwabughudhi na mara kadhaa kumetokea vurumai kwa watu wanaochukizwa na vitendo vya mashoga hao.
Alipoulizwa mmiliki wa eneo hilo, alisema klabu yake ipo karibu na makao makuu ya polisi hivyo kama kungekuwa na vitendo vya aina hiyo, polisi wangechukua hatua.