LELA MUHAJI-Tanroads
KUNA maswali yanayoulizwa na wadau wa usafirishaji ambayo ni muhimu yajibiwe ili yasaidie kuwaongoza kutekeleza majukumu yao bila kukutana na changamoto ambazo wakati mwingine zinawaweka kwenye wakati mgumu.
Maswali haya yamekuwa yakiulizwa kila mara na kutolewa majibu au ufafanuzi kwa mtu mmoja mmoja huku wasiokuwa na majibu hayo wakiendelea kutatizwa nayo na kujikuta wakikiuka sheria na kanuni za matumizi sahihi ya barabara.
Kwa kutambua umuhimu wa kuufikishia umma taarifa sahihi za matumizi ya barabara, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Rogatus Mativila amekuwa akinyanyuka kwenye kiti chake, sambamba na wasaidizi wake kwenda kwa wadau wa usafirishaji, viongozi na watendaji wa Serikali kutoa elimu hiyo na moja ya darasa la hivi karibuni ambalo limewaibua wengi kutaka ufafanuzi wa kina, lilihusu sababu za uwepo wa hifadhi kubwa katika Barabara ya Morogoro (Morogoro Road).

Pamoja na hilo ambalo Tanzania PANORAMA Blog inafanya jitihada za kupata taarifa za kina kwa ajili ya kuufikishia umma, yapo maswali mengine ambayo Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano kwa Umma wa TANROADS, Lela Muhaji anayajibu katika jarida maalumu la TANROADS la Februari 12, 2023 na Tanzania PANORAMA Blog ambayo imekuwa ikichapisha habari za TANROADS na kuombwa ufafanuzi wa baadhi ya taarifa na wasomaji wake, inayachapisha maswali na majibu hayo kwa faida ya wasomaji wake na wananchi wote kwa ujumla.
Kwa mujibu wa jarida maalumu la TANROADS; Swali la kwanza ambalo limekuwa likiulizwa kila mara na wadau wa usafirishaji ni kwanini vipimo vya uzito wa gari vinatofautiana baina ya mizani ukizingatia mzigo husika ni wa ‘transit’ kwa maana kwamba umewekewa rakili (seal) ya Mamlaka ya Mapato (TRA?)
Akijibu swali hilo, Muhaji anaandika katika jarida hilo kuwa vipimo vya uzito wa magari hutofautiana kati ya mzani mmoja kwenda mwingine kutokana na sababu mbalimbali na baadhi ya hizo ni msafirishaji kuongeza mzigo, mafuta au abiria baada ya kupima katika mzani wa kwanza.
Lela anaitaja sababu ya pili kuwa ni mzigo kuhama kutoka kundi moja la ‘ekseli’ kwenda kundi jingine hasa msafirishaji anapokuwa amepakia mzigo wake na kuitumia sehemu kubwa ya nafuu ya asilimia tano kabla ya kuanza safari yake.
Nafuu ya asilimia tano iliwekwa ili kusaidia msafirishaji asizidishe uzito wakati akiwa safarini, mfano mzigo kuhama kutoka ‘ekseli’ moja kwenda nyingine kwa sababu ya miinuko na miteremko pamoja na matuta barabarani.
Sababu ya tatu anayoitaja Muhaji katika andiko lake ni matumizi mabaya ya mfumo; na hapa anautaja kwa lugha ya kimombo, unaitwa ‘air suspension’ hasa wakati wa upimaji.
Anataja pia ujazaji mchanga, mbao, kokoto na pumba kuwa zinapokumbana na mvua na kulowanishwa, mzigo huongezeka uzito.
Swali la pili ambalo limekuwa likiulizwa kila mara na wadau wa usafirishaji ni kuwa; gari kuvuja oil ni suala la kimitambo zaidi, je ni kwanini wasafirishaji wakifika mizani wanatozwa tozo?
Akitoa majibu ya taasisi yake, Muhaji anaandika kuwa kumwaga mafuta barabarani ni kosa kwa mujibu wa sheria namba 13 ya barabara na vituo vya mizani vinavyosimamiwa na TANROADS vinafanya kazi chini ya Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya udhibiti uzito wa magari ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.
Kwamba suala la udhibiti wa makosa mengine yaliyotajwa kwenye sheria ya barabara siyo jukumu la vituo vya mizani na aidha, ofisi za mameneja wa mikoa zina vitengo maalumu vya kushughulikia makosa ya aina hiyo.
Swali la tatu katika orodha hiyo linauliza ni kwanini gari linapokuwa mizani haliruhusiwi kurudia kupima tena uzito kabla ya kuandikiwa tozo.

Jibu la swali hilo linaelekezwa kwenye sheria, kuwa; sheria inaelekeza gari linapofika mzani lipimwe uzito na likikutwa limezidisha uzito litozwe tozo ya uharibifu wa barabara na baada ya kulipa tozo husika msafirishaji ataruhusiwa kupanga mzigo wake hadi apate uzito unaokubalika au kushusha mzigo uliozidi na hasa magari yaliyozidisha uzito wa jumla.
Lakini pia, Lela anaandika kuwa msafirishaji anaruhusiwa kurudia kupima baada ya mzigo wake kuwa katika vipimo vinavyokubalika na kupewa kile kinachoitwa kwa lugha ya kimombo ‘re-weight ticket.’
Katika mlolongo wa maswali ya wadau wa usafirishaji, lipo pia linalouliza ni kwanini hadi sasa kuna tozo za uzidishaji uzito wa magari kwa kutumia Dola za Marekani ikizingatiwa kuwa Tanzania nia nchi huru na ina sarafu yake?
Akijibu hilo, Lela anaandika kuwa kwanza sheria inayotumika kwa sasa ni sheria ya kikanda, yaani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo kwa kuwa jumuiya haina sarafu moja, ilichaguliwa Dola ya Marekani kuwa msingi wa tozo na msafirishaji atalipia tozo husika kwa kiwango cha ubadilishaji fedha cha nchi husika.
Kwamba hili linasaidia kutokuwepo marejeo ya kila mara ya tozo endapo sarafu ya nchi mojawapo katika jumuiya itabadilika thamani kwa kiwango kikubwa.
Aidha, malighafi kama lami ambayo kwa sehemu kubwa hutumika kwenye matengenezo ya barabara inaagizwa kutoka nje ya nchi kwa kutumia fedha za kigeni hivyo kwa kuwa fedha za tozo zinalenga kurekebisha sehemu ya barabara zinazoharibiwa na uzidishaji uzito, ndiyo maana tozo hizo zinatakiwa kulipwa kwa Dola za Marekani.
Swali kuhusu ni kwanini vibali vya mizigo maalumu visitolewe na meneja wa mkoa husika kama zamani linajibiwa kuwa; mfumo wa utoaji vibali wa zamani uliohusisha mameneja wa mikoa ulikuwa na upungufu mwingi, lakini mfumo wa sasa unaohusisha moja kwa moja wizara kutoa vibali hivyo kwa njia ya mtandao ni mzuri zaidi kwa sababu vibali vinatoka ndani ya muda mfupi.
Inaulizwa pia kuwa iwapo vituo vya mizani ni vyanzo vya mapato kwa Serikali, naye Lela anajibu akiandika kuwa hilo siyo sahihi bali vituo vya mizani vimewekwa kudhibiti uharibifu wa barabara unaotokana na uzidishaji uzito wa magari yanayopita kwenye barabara hizo.
Lela anaandika zaidi kuwa lengo ya TANROADS ni kuwa na makusanyo sifuri pindi wasafirishaji watakapofuata sheria na taratibu kwa kubeba uzito unaokubalika hivyo kuepusha uharibifu wa barabara.
Lipo pia swali linalouliza ni kwanini sheria na fomu ya kujaza kwa ajili ya maombi ya vibali vya mizigo maalumu imeelezwa au kuandikwa kwa Lugha ya Kiingereza?
Nalo linalojibiwa na Lela kuwa, tovuti ya wizara kwa ajili ya kuomba vibali vya mizigo maalumu ina sehemu inayomruhusu muombaji kuchagua lugha hivyo muombaji anaweza kuchagua kujaza fomu hiyo kwa Lugha ya Kiswahili na aidha, uandaaji wa sheria kwa Lugha ya Kiswahili unaendelea kufanyiwa kazi na Wizara ya Katiba na Sheria.

Wapo wadau wa usafirishaji wanaouliza kila mara kuhusu utaratibu unaopaswa kufuatwa kubeba au kuvuta gari lililoharibika naye Lela anajibu kuwa; ili kuweza kuvuta au kusafirisha gari lililoharibika barabarani, msafirishaji anapaswa kuomba kibali kwa njia ya mtandao akionyesha gari linalovuta lililoharibika na kuambatanisha picha husika.
Kwamba kibali hicho kinahitajika kwa sababu magari yanayovutana hayana muunganiko wa mfumo wa upepo kwa ajili ya breki na umeme kwa ajili ya taa za tahadhari wakati dereva wa mbele akifunga breki au kuonyesha anaelekea kushoto au kulia, hivyo magari mengine yanaweza kusababisha ajali kama hakutakuwa na tahadhari itakayowekwa.
Lela anaandika akifafanua kuwa iwapo gari lililoharibika litaenea ndani ya gari kubwa la mfano kwenye kichanja cha semitrela bila kuzidi vipimo vinavyokubalika na likafungwa madhubuti, msafirishaji anaweza kubeba gari hilo bila kulazimika kuomba kibali.
Inaulizwa pia kuwaa kwa vile sehemu za upakiaji mizigo hazina mizani za kujihakiki, je, ni nini mtizamo wa Serikali kwa wasafirishaji kutozwa tozo ya uzidishaji uzito wanapofika vituo vya mizani wakati hawawezi kujihakiki kwenye vituo vya upakiaji mizigo?
Hili linajibiwa na Lela ambaye anaandika hivi. ‘Kwa kuwa mizigo hii inaanzia sehemu mbalimbali za nchi yetu, tunatoa wito kwa wadau wa usafirishaji kujiwekea mizani hizo kwenye yadi zao hasa kwenye miji, maeneo ya machimbo ya madini ya ujenzi na mashamba makubwa ili kabla ya kuanza safari, wajihakiki.
‘Hatua hiyo ya kujihakiki kwanza itaondoa tatizo la kukumbwa na tozo za uzidishaji uzito wanapofika vituo vya mizani na ikumbukwe kuwa tozo ipo ili msafirishaji aliyezidisha uzito na kuharibu sehemu ya barabara kabla ya kufika mizani, afidie uharibifu alioufanya.
‘Hata hivyo Serikali imeanza kuweka mizani ya kujihakiki eneo la Kurasini na hii inahusu magari yote yanayotoka Bandari ya Dar es Salaam.’
Pengine, swali gumu zaidi linaloulizwa na wadau wa usafirishaji ni hili; ‘kwanini wanyama na lami visitolewe kwenye mizigo inayohitaji vibali kama ilivyofanyika kwa wasafirishaji mafuta?
Hili, Lela analijibu hivi; ‘Suala hili kwa kuwa liko kwenye sheria, tunalichukua na tutalifikisha kwenye ngazi husika za maamuzi kama ushauri kwa maboresho ya sheria zilizopo.
Swali kuhusu gari linapoharibika barabarani, sheria inatoa muda gani wa kulitoa kabla ya kuanza kulitoza toza; majibu yake ni haya:
‘Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara namba 13 ya mwaka 2017, magari yanayoharibika barabarani yamepewa muda kulingana na maeneo ambayo gari husika limeharibika; mosi ni saa sita kwa maeneo yote ya miji na saa 12 kwa maeneo yaliyo nje ya miji, lakini muda huo unaotajwa hauhusiani na magari yaliyofunga barabara.
Swali la mwisho linahoji ni kwanini Tanzania tunapima uzito wa mabasi wakati nchi jirani ya Kenya haipimi?
Akijibu. Lela anaandika kuwa kwa mujibu wa kifungu cha nane cha Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya udhibiti uzito wa magari ya mwaka 2016, magari yote yenye uzito wa kuanzia tani 3.5 yanapaswa kupimwa hivyo mabasi yanapimwa kwa kuwa yapo kwenye kundi hilo.
Lela anahitimisha kwa kuueleza umma kuwa takwimu zilizopo TANROADS zinaonyesha bado yapo mabasi yanayopimwa na kukutwa yamezidisha uzito na kwamba katika maeneo tofauti, yapo mabasi ya abiria ambayo huwekewa mizigo mingi kwenye buti hivyo wakati wa kupima hubainika yamezidi uzito wakati abiria hawajajaa kwenye viti.