Thursday, July 17, 2025
spot_img

MAJALIWA AIPA TANO FOUNTAIN GATE KUTWAA UBINGWA CAF

RIPOTA WA WAZIRI MKUU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameipongeza timu ya soka ya wasichana ya Fountain Gate kwa kutwaa ubingwa wa soka la wanawake kwa shule za sekondari barani Afrika (CAF African School Football Championship) kwenye mashindano yaliyofanyika nchini Afrika Kusini.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema ushindi wa timu hiyo ni heshima kwa Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kukuza na kuendeleza sekta michezo nchini.

Pongezi hizo kwa timu hiyo alizitoa Aprili 13, 2023 alipokutana nayo kuipongeza kwa kutwaa ubingwa huo baada ya kuzifunga shule kutoka Nchi za Gambia, Afrika Kusini, Congo na Morocco.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Rais Samia amekuwa na utaratibu wa kukutana na timu zinazoshiriki michuano mbalimbali ya kimataifa, lengo likiwa kutoa hamasa na kutekeleza azma yake ya kuimarisha sekta ya michezo nchini

Alitoa wito kwa wamiliki wa shule binafsi kuanzisha idara za michezo kwenye shule zao ili kutoa fursa kwa vijana kuonesha vipaji kwa kushiriki michezo mbalimbali kwani itasaidia kutoa mchango kwa Taifa kupitia sekta ya michezo.

Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana alisema kabla ya timu hiyo kwenda Afrika Kusini kushiriki michuano hiyo, tayari ilishakuwa bingwa wa mashindano kwa upande wa CECAFA kwenye mashindano kama hayo.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Angela Kairuki aliwapongeza wanafunzi hao kwa kuiwakilisha vema nchi kwenye michuano hiyo iliyoandaliwa kwa mara ya kwanza. “Wasichana wakiamua jambo lolote wanaweza, yapo mengi ambayo mnaweza kuyafikia,” alisema Kairuki.

Mbali ya kutwaa ubingwa huo, timu ya Fountain Gate pia ilitwaa tuzo tatu zikiwemo za golikipa bora, mchezaji bora na mfungaji bora wa mashindano hayo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya