RIPOTA MAALUMU – Panorama
KUNA kurasa mpya katika kitabu cha historia ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zinazoelezea jinsi Rais Samia Suluhu Hassan alivyokanyaga na kuacha nyayo za miguu yake kwenye hifadhi hiyo.
Kama ilivyo kwa binadamu ambaye historia inaeleza namna ambavyo amekuwa akipitia kwenye mabadiliko ya kimaumbile; kutoka binadamu wa zama kale za mawe hadi binadamu wa sasa wa zama za sayansi ya teknolojia na kama ilivyo kwenye uso wa dunia ambao tangu uwepo umekuwa ukikutana na mabadiliko mengi, ndivyo ilivyo kwa Hifadhi ya Ngorongoro ambayo nayo tangu kuwepo kwake imekutana na mabadiliko mengi hadi haya ya sasa ya Rais Samia ambayo yameingia kwenye kitabu cha historia ya hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Mhariri wa Jarida la NCAA, Kassim Nyaki ambaye ameandika kwa kina mageuzi yenye mafanikio yaliyofanyika kwenye hifadhi hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, anaitaja filamu ya The Royal Tour, iliyoigizwa na Rais Samia Suluhu Hassan kama msingi imara wa matokeo ya mafanikio hayo.
Nyaki, akiandika katika toleo la robo ya kwanza ya mwaka 2023 katika Jarida la NCAA, anaeleza kuwa Machi, 2023 Rais Samia alitimiza miaka miwili ya urais wake huku akiwa amefanya mambo mengi ya kukumbukwa katika Sekta ya Maliasili na Utalii na hasa kuitangaza Tanzania kupitia utengezaji wa filamu ya The Royal Tour ambayo imechagiza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii na kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Akifafanua mafanikio hayo, Nyaki anaandika kuwa kati ya mwezi Machi, 2021 hadi Februari, 2023 watalii waliotembelea vivutio vilivyoko Hifadhi ya Ngorongoro ni 1,057, 127. Kati ya hao, watalii kutoka nje ni 609,199 na watalii wa ndani ni 447, 928 na mapato ambayo NCAA iliingiza kutokana na idadi hiyo ya watalii ni Shilingi 233,116,973,350.
Mbali ya hayo, Nyaki anaandika kuwa Hifadhi ya Ngorongoro ina mengi ya kujivunia ikiwemo uboreshaji wa maisha ya wakazi wenyeji wanaoishi katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambao Serikali imewajengea nyumba 503 za awamu ya kwanza katika Kijiji cha Msomera, mkoani Tanga. Hawa ni wale waliokubali kuhama kwa hiari kutoka eneo la hifadhi.
Kwamba ujenzi wa nyumba hizo umeenda sambamba na kuwapatia hati za umiliki wa nyumba iliyo kwenye kiwanja cha ukubwa wa ekari 2.5, kila kaya kupatiwa shamba lenye ukubwa wa ekari tano kwa ajili ya shughuli za kilimo, kuchimbwa kwa visima vya maji karibu na maeneo ya makazi na kutengewa maeneo ya malisho na majosho.
Akiandika bila kusahau takwimu, Nyaki anaonyesha kuwa tangu kuanza kwa kazi hiyo Juni, 2022 hadi Januari 2023, kaya 547 zenye watu 3,010 zilizokuwa kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zimehamia Kijiji cha Msomera kwa hiari.
Aidha, hadi Januari, 2023 kaya 1,524 zenye watu 8,715 na mifugo 32,842 wamejiandikisha kuhama kwa hiari kwenye eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Jambo la kujivunia kwa NCAA ni uboreshaji wa miundombinu ya utalii uliofanyika baada ya Serikali kuipatia NCAA Shilingi bilioni 6 zilizotokana na mkopo wa mpango wa maendeleo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ambazo ziliiwezesha kununua mitambo ya ukarabati wa ujenzi wa barabara ndani ya hifadhi.
Nyaki anazitaja katika andiko lake barabara zilizokarabatiwa kwa kutumia fedha hizo kuwa ni ya kutoka lango kuu la kuingia NCA (geti la Loduare hadi golini), Barabara ya Golini hadi Jabali la Nasera, barabara ya kutoka View Point, Empukai hadi Nayobi, Golini Ndutu na kipande cha barabara ya kutoka njia kuu ya Serengeti kwenye Makumbusho ya Olduvai.
Anaendelea kuandika Nyaki kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya urais wa Rais Samia, Barabara ya Seneto hadi Kreta yenye urefu wa kilomita 4,2 imejengwa kwa teknolojia ya mawe ikigharimu Shilingi bilioni 1.7 na kwamba wakati wa ujenzi ilitoa ajira kwa watu 90.
Anataja pia ukarabati wa chanzo cha maji na kujengwa kwa mtambo wa kutibu maji, maabara ya maji na nyumba ya waendesha mtambo katika eneo la Mama Hhau, pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro. Gharama za ujenzi wa tenki ni Shilingi 890,050,000 na lina uwezo wa kutibu lita milioni 1.5 za maji kwa siku.
Hivi sasa watalii wanaoingia ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wanapata huduma ya maji safi yaliyotibiwa kwenye tenki hilo.
Katika mikanyago yake Rais Samia ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro inayotajwa na Nyaki kuacha alama za kukumbukwa ni pamoja na uwekaji wa vigingi katika eneo la pori la Akiba la Pololeti kwa ajili ya kuboresha shughuli za uhifadhi na ulinzi na hivi sasa pori hilo limekabidhiwa kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kusimamia shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali zilizopo.
Akihitimisha, Nyaki anaandika kuwa ni kutokana na mabadiliko hayo chanya ambayo yameingizwa katika kitabu cha historia ya Hifadhi ya Ngorongoro yakisomeka kuwa yanakwenda sambamba na uboreshaji wa mazao ya utalii hasa kwenye eneo la malikale; eneo la Kimondo pamoja na Mapango ya Amboni.
Kwamba miongoni mwa mazao hayo ni makumbusho mpya iliyopo eneo la Kimondo cha Mbozi ambayo imesheheni vitu vya mila na desturi za jamii ya makabila ya kusini kama Wanyiha, Wandali na Wanyamwanga yakionyesha akiolojia na zana za mawe, zana za kilimo, chakula na ngoma za asili zilizotumika yapata miaka 40 iliyopita.
Na katika mapango ya Amboni, Tanga historia mpya inaonyesha Serikali imeweka mifumo ya umeme ndani ya pango, ujenzi wa daraja ndani ya pango na ujenzi wa geti la kisasa la kuingia mapangoni, lenye thamani ya Shilingi milioni 244.