LELA MUHAJI, TANROADS
HIFADHI kubwa iliyopo kwenye Barabara ya Morogoro (Morogoro road) inatokana na umuhimu wa barabara hiyo kwenye uchumi wa nchi.
Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila mapema mwaka huu alipokuwa akitoa elimu kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo kuhusu Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 na kanuni zake za mwaka 2009 inayohusu matumizi sahihi ya barabara.
Utoaji elimu huo uliandaliwa na TANROADS na kufanyika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambapo Mhandisi Mativila alisema kuna sintofahamu kuhusu matumizi ya hifadhi ya barabara, matumuzi ya ujenzi wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo hususan katika Barabara ya Morogoro ambayo upana wake umekuwa tofauti na maeneo mengine.
Pamoja na mambo mengine, Mativila alisema; “tumekutana na viongozi kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kuwapa mafunzo, lengo likiwa wao wapeleke elimu hii kwa wananchi ili waelewe na kuondoa malalamiko yao.”
Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka TANROADS, Usaje Mwambene ambaye aliambatana na Mhandisi Mativila katika utoaji wa elimu hiyo, alisema Sheria ya Barabara ya Mwaka 2007 na Kanuni zake za 2009 imeipa mamlaka Wakala wa Barabara kuondoa shughuli zote zilizopo ndani ya hifadhi ya barabara.
Wakitoa maoni yao wakati wa mafunzo hayo, viongozi wa Wilaya ya Ubungo na wadau waliishukuru TANROADS kwa kuwapatia elimu ya umuhimu wa hifadhi ya barabara ambayo itawasaidia watakapokuwa wakiwaelimisha wananchi.
Walisisitiza umuhimu wa Tanroads kuendelea kutoa elimu katika maeneo mengine ili kukuza uelewa wa matumuzi na hifadhi za barabara.

HABARI HII ILICHAPISHWA KWANZA KWENYE JARIDA LA MTANDAONI LA TANROADS LA FEBRUARI, 2023. TANZANIA PANORAMA IMEITUMIA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI AMBAO BADO WAMEKUWA NA MASWALI KUHUSU HIFADHI YA BARABARA YA MOROGORO.