KAMISHNA wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, (NCA) Dk. Freddy Manongi amewaalika Watanzania na watalii kutoka pande zote za dunia kutembelea hifadhi hiyo wakati huu huduma zinazotolewa ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro zikiwa zimeimarishwa.
Akiandika katika Jarida la NCA, toleo la kwanza kwa mwaka 2023, lililotolewa mwezi huu, Dk. Manongi ameeleza kuwa taasisi anayoiongoza imepiga hatua kubwa katika mkakati wake wa kuboresha miundombinu ya barabara ndani ya hifadhi na kwamba ni jambo la kujivunia kuwa fedha zilizofanikisha kazi hiyo ni sehemu ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19.
Dk. Manongi ameandika kuwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitimiza miaka miwili madarakani, amefanikiwa kuleta mageuzi makubwa ya utangazaji utalii na uhifadhi ambayo yameiwezesha NCA kuhimili athari za mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO 19, pamoja na kurudisha kasi ya ongezeko la watalii nchini.
Ameendelea kuandika kuwa kutokana na juhudi hizo za Rais Samia, Tanzania na hasa NCA ilifanikiwa kupata idadi kubwa ya watalii, sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii hifadhini.

Kwa mujibu wa andiko la Dk. Manongi (pichani juu) kwenye jarida hilo, NCA mbali na kuboresha miundombinu ya barabara, pia imeboresha huduma zitolewazo kwa wageni hifadhini ikiwa ni pamoja na maji, vyoo na mawasiliano.
Kwamba katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Samia akiwa madarakani, NCA imeendelea kutekeleza mradi mkubwa unaolenga kuboresha maisha ya wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na imeshajenga nyumba za kisasa 503 kwa ajili ya wakazi wa NCAA wanaohamia kwa hiari katika Kijiji cha Msomera, mkoani Tanga.
Katika hilo, Dk. Manongi ameandika kuwa nyumba hizo ni sehemu ya mkakati wa kuwapa wananchi hao uhakika wa maisha bora katika makazi yao mapya na kwamba mamlaka anayoiongoza, mbali ya kuwajengea nyumba hizo imeikabidhi kila kaya shamba lenye ukubwa wa ekari tano na fedha tasilimu.
Dk. Manongi ameendelea kuandika kuwa NCA imeweka na kuboresha miundombinu pamoja na huduma za kijamii na amezitaja kwa uchache kuwa ni pamoja na shule, zahanati, maji, umeme na mawasiliano.
Ameandika zaidi kuwa kutokana na ufanisi ulioonyeshwa na NCA kwenye majukumu ya uhifadhi, sasa imekabidhiwa kusimamia Pori la Akiba la Pololeti na kwamba tangu ilipokabidhiwa jukumu hilo, hali ya ulinzi, uhifadhi na mvuto kwa wageni imeimarika kwa kiwango kikubwa.

Akihitimisha andiko lake hilo, Dk Manongi ameandika kuwa NCA inaendelea na juhudi za kuwashirikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi katika shughuli mbalimbali za uhifadhi kwa sababu ushirikishwaji huo; pamoja na mambo mengine umepunguza migogoro iliyokuwapo awali baina ya hifadhi na vijiji.
ANDIKO HILI LA KAMISHNA WA UHIFADHI WA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO (NCA) DK. FREDDY MANONGI LIMECHAPISHWA KATIKA JARIDA LA NCA LA ROBO MWAKA WA 2023, LILITOLEWA MWEZI APRILI, 2023. KUTOKANA NA UMUHIMU WAKE, TANZANIA PANORAMA BLOG IMELITUMIA LIKIWA LIMEHARIRIWA KWA KIWANGO KIDOGO ILI KUWAFIKIA WASOMAJI WAKE WA NDANI NA NJE, HUSUSAN DIASPORA AMBAO WAMEKUWA WASOMAJI WETU NA WAUNGAJI MKONO WETU WAKUBWA KUTOKANA NA UBORA WA HABARI ZETU.