RIPOTA WA WAZIRI MKUU
Ruangwa, Lindi
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amekabidhi pikipiki 100 zenye thamani ya Shilingi milioni 260 kwa vijana wa Wilaya ya Ruangwa watakazozitumia kufanya biashara ya usafirishaji.
Akizungumza na vijana wa Ruangwa kwenye hafla ya kukabidhi pikipiki hizo iliyofanyika mwishoni mwa wiki kwenye viwanja vya CWT, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi, Majaliwa alisema utoaji wa pikipiki hizo ni muendelezo wa mpango wa ofisi ya Mbunge wa kuwawezesha vijana, wanaume, wanawake na wazee.
“Mwaka 2016/2017 tulichukua pikipiki 235 na kuzigawa kwenye wilaya yote hii. Na jambo zuri kwa sasa, kwenye Serikali ya awamu ya sita, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yeye ameamua kuwa na kada ya wasafirishaji wadogo, wa kati na wakubwa,” alisema.
Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa aliwaeleza vijana hao watambue kwamba na wao ni wasafirishaji wa usafiri wa kawaida kwa kutumia pikipiki.
Mapema akielezea mradi huo, mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Martin Mbwana alimweleza Majaliwa kwamba pikipiki hizo zitakopeshwa kwa bei ya Shilingi milioni 2.6 bila riba yoyote na kwamba muda wa marejesho ni miezi nane.
“Kuanzia sasa hadi Desemba, mwaka huu mtu anapaswa awe amekamilisha mkopo wake. Na kianzio ni kati ya sh. 500,000 hadi 700,000. Mkopo huu umetolewa chini ya mdhamini mkuu, Mpaluka Hashim Mtopela,” alisema.
Alimshukuru Rais Samia kwa kufungua milango ya biashara na kuongeza: “Nikiwa mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo wa Soko la Kariakoo, niko hapa Ruangwa ili kuwawezesha vijana wa Ruangwa,” alisema.
Kwa upande wake, mdhamini mkuu wa pikipiki hizo, Mpaluka Hashim Mtopela alimshuruku Majaliwa kwa kuamua kuwajali vijana wa jimbo lake.
“Mwaka 2016 ulitoa pikipiki 235 ambazo zimewesha vijana zaidi ya 600 kuishi maisha mazuri wao na familia zao. Wako waliopewa pikipiki moja lakini leo hii wanamiliki pikipiki tatu hadi nne.
“Hii ina maana leo tukimpa kijana Shilingi milioni 2.6, baada ya muda ataweza kutengeneza Shilingi milioni 7. Vijana hawa nimewachukulia dhamana kwa sababu ninaamini wanaweza kuzirejesha. Safari hii tumechukua pikipiki lakini muda ujao tutachukua mashine ya kufyatulia matofali au ya kumwagilia bustani kwa sababu tunao vijana wenye uwezo,” alisema.
MATUKIO KATIKA PICHA WAZIRI MKUU ALIPOGAWA PIKIPIKI 100 KWA VIJANA WA RUANGWA


