Monday, June 9, 2025
spot_img

MADIWANI CCM MOSHI ‘WAVUANA NGUO,’ WATISHANA

RIPOTA PANORAMA

MWENENDO wa mambo ndani ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini si shwari.

Taarifa zilizoifikia Tanzania PANORAMA Blog kutoka vyanzo vyake vya habari vilivyoko ndani ya manispaa hiyo, zinadai Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini limegawanyika katika makundi mawili hasimu na kwamba madiwani wawili walio katika makundi tofauti yanayohasimiana wamekuwa wakitukanana hadharani matusi mazito ya nguoni.

Taarifa hizo zinakwenda mbali zaidi zikidai madiwani hao, wanaotajwa kuwa ni Diwani wa Kata ya Miembeni, Mohamedi Mushi na Diwani wa Kata ya Bomambuzi ambaye pia alipata kuwa meya wa manispaa hiyo, Juma Raibu hivi karibuni walishambuliana kwa maneno makali wakiwa katika kikao cha Kamati ya Mipangp Miji na kwamba Raibu alitishia kumuangamiza Mushi.     

Inadaiwa, Diwani Raibu alitishia kumuangamiza Mushi wakati wa kikao cha Kamati ya Mipango Miji ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, kilichoketi Januari 20, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Manispaa ya Moshi.

Vyanzo vya habari vinadai kuwa katika kikao hicho, Mushi alihoji kuhusu maeneo ya wazi ambayo Raibu anadaiwa kujimilikisha baada ya kutengeneza hati yeye mwenyewe jambo ambalo lilimkasirisha Raibu na kuanza kumshambulia Mushi kwa maneno makali kabla ya kutishia kumwangamiza.

Inadaiwa zaidi kuwa baada ya tukio hilo, Mushi aliandika barua ya malalamiko kwenda Kamati ya Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi lakini alipoulizwa jana na Tanzania PANORAMA kuhusu hilo alikataa kulizungumzia kwa madai kuwa anayemuuliza (mwandishi wa PANORAMA) anaweza kuwa ametumwa na mbaya wake, Raibu.

Alipoulizwa leo Raibu kuhusu hilo, huku akitumia baadhi ya maneno makali ambayo PANORAMA haitayaandika kwa sababu za kimaadili, alisema hilo jambo siyo la kweli na kwamba Mushi asitafute ‘kiki’ dhidi yake kwa sababu jambo la kutokea mtafaruku kwenye kikao ni jambo la kimaadili hivyo vipo vyombo vinavyoshughulikia mambo hayo alivyovitaja kuwa ni kamati ya  maadili ya chama, maadili ya halmashauri lakini pia Jeshi la Polisi.

“Hilo jambo siyo la kweli, na mwambie huyo diwani asitafute ‘kiki’ dhidi yangu….., kwa sababu amekwishakufa kisiasa asitafute ‘kiki’ kwa watu wengine, hakujawahi kutokea mtafaruki kwenye uongozi wangu au nje ya uongozi wangu.

“Tuna uhusianio mzuri ila yeye mwenyewe ndiyo anafikiri kwamba, labda anajihisi kufanya hivyo kwa sababu ya ‘interest’ zake akimini kuwa yeye ndiyo amewekwa na wakubwa hapo ili afanye kazi ya kuharibia wengine, lakini mimi kama Raibu naendelea kuchapa kazi,” alisema Raibu.

Alipoulizwa Mushi anamchafuaje, huku akitumia baadhi ya maneno makali yasiyoandikika, alisema zipo fitna nyingi na kwamba amekuwa akitangaza ndiye aliyemtoa kwenye wadhfa wa umeya wakati aliyemtoa kwenye wadhfa huo ni katibu wa mkoa na mkuu wa mkoa.

“Mimi ningetaka kufanya naye fujo ningemfuata nyumbani kwake, napajua lakini mimi sina tabia hiyo na wala siwezi kufanya vitu hivyo….. yeye anajishtukia tu kwa sababu shida yake ni shule……

“….Mimi siwezi kubishana naye, hivi wewe mwandishi ukifika pale stendi ukatukanwa na vichaa utaenda polisi? Kwa hiyo ukimshtaki utampa ‘kiki’…..ndiyo maana mimi akinitukana huwa namsamehe tu, ameishanitukana mara kadhaa yaani anaingilia mpaka ‘personal life’ yangu, anaingilia mpaka maisha yangu binafsi,” alisema Raibu.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini, Zuberi Kidumo alipoulizwa kuhusu hilo alisema hawezi kuzungumzia mambo ya watu kutishiana kuangamizana kwa sababu ni ya kijinai lakini alithibitisha kuwepo kwa mgogoro na kutukakana matusi mazito ya nguoni baina ya Raibu na Mushi.

“Ofcourse kwenye kikao kulitokea kutupiana maneno baina ya hao wawili, hicho nakikumbuka. Ni kikao kilichofanyika muda mrefu tu, siyo jana wala juzi lakini kweli siku hiyo kulitokea kutupiana maneno hayo baada ya mtu kuhoji kwamba sijui umiliki wa nini na nini.

“Sasa kama baada ya pale walitoka wakaendelea kutishiana tena na maneno mengine magumu hayo ni ya kwao lakini kulitokea kutokuelewana, kulumbana wao wenyewe kwa wenyewe.

“Na niseme jambo moja, Mohamedi Mushi na Raibu wamekuwa wakitofautiana mara kwa mara sana. Mara nyingi Juma Raibu amekuwa na tabia ya kumtukana sana Mohamedi Mushi, hilo nalithibitisha hata siku ya kiama, siku ya mwenyezi Mungu mbele ya haki, hilo mimi nalithibitisha, nimewahi kumsikia kabisa Juma akimtukana mbele yangu.

“Huwa haipiti siku mbili tatu utasikia wameleteana tabu. Kuna siku nimeambiwa tena wametukakana huko makaburini, wakatishiana tena hivyo yaani wakishatukanana wanafikia hadi kutishiana masuala yao ya kimaisha na nini sasa nani anamtishia mwenzake hilo litakapofika kwenye vyombo vya sheria ndiyo watajua zaidi lakini ni watu ambao wamekuwa wakilumbana mara kwa mara.

“Lakini hilo la Juma Raibu kumtukana Mohamedi Mushi hilo wala siyo la kuuliza mtu wa pembeni hilo nimelisikia kwa masikio yangu kabisa anamtukana matusi mazito hapa kwa hapa,” amesema Mstahiki Meya Kidumo.

Alipoulizwa iwapo kuna hatua zilizopata kuchukuliwa kwa madiwani hao kwa vitendo vyao vya kutukanana matusi mazito na kutishiana wakiwa hadharani ikiwa ni pamoja na makaburini alisema huwa wanayatenda hayo nje ya eneo la halmashauri.

“Kama ninavyokwambia kuna siku walitukanana makaburini, kuna siku walikutana uswahili huko wakaanza kutukanana, kwa mambo ambayo wanatukakana huko nje ambayo unaweza ukawa unayasikia tu lakini sasa anayepaswa kuonyesha kuwa jambo hilo linamkera ni muhusika mwenyewe.

“Unajua ni kosa la jinai kama ataenda kushtaki kuwa ametukanwa, tukaitwa tutoe ushahidi, tutatoa kile tulichokisikia, hivyo yeye mwenyewe anayetendewa anatakiwa aanze kulalamika kwenye vyombo vya sheria halafu pale tutakapohitajika sasa sisi kwenda kulithibitisha hilo ndiyo tutaenda,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu siku waliyoanza kutukanana ndani ya kikao baada ya mtu mmoja kuhoji kuhusu viwanja anavyodaiwa kujimikilisha Raibu, alisema mambo ya kwenye vikao vya kamati za madiwani ni ya siri hivyo hawezi kutoa taarifa za vikao

“Yeye aliyetukanwa endapo atakwenda kushtaki kwenye mamlaka husika, mamlaka zikataka kuthibitisha kama kilichosemwa ni kweli hapo ndipo tunaweza kulitolea majibu lakini taarifa za kikao ni siri,” alisisitiza.

Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai alipoulizwa kuhusu tukio la madiwani hao kushambuliana kwa maneno makali kikaoni na kutishana kuangamizana alikiri kulifahamu tukio hilo lakini alikataa kulizungumzia kwa kile alichodai yeye si msemaji wa chama ngazi ya wilaya huku akitaka asihusishwe kwa namna yoyote na migogoro ya kutengenezwa.

Wakati Mwenyekiti Swai akijiweka pembeni na mgogoro huo, Katibu wa Madiwani wa CCM, ambaye pia wa Diwani wa Kata ya Korongoni, Witness Mziray alipoulizwa naye alikataa kuzungumza kwa madai kuwa yeye si Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji.

Tanzania PANORAMA imemtafuta Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa na kumuuliza iwapo ofisi yake imekwishapokea malalamiko yoyote kuhusiana na mgogoro wa madiwani hao naye alisema jambo hilo hajawahi kulisikia na kwamba ni geni kwake.

“Hawa ninawasiliana nao kila siku, unajua hao ni wanasiasa sasa kama mimi ni RPC, kama kuna malalamiko inabidi wayaripoti kituoni, hakuna aliye juu ya sheria. Mwanasiasa ni mtu mkubwa, ni diwani kwa hiyo kama kuna jambo ana namba yangu anaweza kunipigia ‘direct.’

“Inawezekana imeripotiwa sijui kwa sababu wakati mwingine siyo kila kitu utakijua lakini naamini kwa nafasi yake anajitambua, anajua haki zake kwa hiyo ‘automatically’ ningeishajulishwa, ‘anyway’ labda niulizie maana ni kigeni kwangu,” alisema Kamanda Maigwa.

Haya yanadaiwa kutokea ikiwa ni miezi kadhaa imepita baada ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi Mjini kumwondoa Raibu kwenye wadhfa wa umeya kwa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimuandama.

Raibu aliondolewa kwenye wadhfa wa umeya Agosti 11, mwaka jana baada ya kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye na madiwani 20 kati ya 30 wa baraza hilo akituhumiwa kuhudhuria sherehe ya siku za kuzaliwa na kijana anayedaiwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Raibu alihudhuria sherehe hiyo iliyofanyika kwenye Mgahawa wa Bondeni Lounge, Februari 13, mwaka jana na baadaye picha zake akiwa kwenye tikio hilo zilisambaa mitandaoni, moja ya picha hizo ilimwonyesha akilishwa keki na kijana huyo ambaye alikuwa amevaa heleni kwenye masikio yake.  

Akiwa kwenye sherehe hizo, Raibu anadaiwa kupokea ‘kilio’ cha mashoga hao na kuahidi kukipatia ufumbuzi; mashoga hao inadaiwa pamoja na mambo yao mengine, ‘walilia’ kutotambuliwa kwa haki zao za ushoga.

Mbali na hilo, Raibu pia alikuwa akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya, rushwa katika utoaji wa vibali vya ujenzi kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kufanyika shughuli za ujenzi wa majengo ya chini.

Katika mlolongo wa tuhuma zilizokuwa zikimuandamana ilikuwemo pia ya kutoa maamuzi ambayo hayajaidhinishwa na baraza la madiwani, kutowaheshimu wajumbe wa Kamati ya Fedha na Utawala na kutoruhusu mjadala kuhusu vikundi vilivyoomba mikopo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya