Monday, July 21, 2025
spot_img

TUHUMA ZA WIZI WA FEDHA ZA WATEJA BENKI YA NMB

RIPOTA PANORAMA

HABAKUKI Stefano Nsyenge, Mkazi wa Mafinga, Mkoa wa Iringa ameibua tuhuma za wizi wa fedha zake alizozihifadhi kwenye akaunti iliyoko Benki ya National Microfinance Bank (NMB) Tawi la Mafinga, akidai umefanywa na wafanyakazi wa benki hiyo.

Anadai, pamoja naye wapo wateja wengine waliokutana na kadhia hiyo ya kuibiwa fedha zao kwenye akaunti na anawataja kwa uchache kuwa ni mwanamke mmoja (jina tunalihifadhi kwa sasa) anayedai mapema wiki hii aligundua mamilioni ya fedha alizokuwa amehifadhi kwenye akaunti yake iliyopo kwenye benki hiyo yameibiwa na kubakiziwa Shilingi elfu tatu.

Nsyenge anataja tukio lingine la wizi katika benki hiyo kuwa limemkuta mteja mwingine ambaye ni mwanamke (jina lake linahifadhiwa kwa sababu hajafikiwa na Tanzania PANORAMA kuzungumza) aliyeingiziwa fedha kwenye akaunti yake kutoka mahali kusikojulikana kisha zikatolewa zote pamoja na zake zilizokuwa kwenye akaunti na kwamba shauri lake kwa sasa linashughulikiwa na vyombo vya usalama.

Akizungumza na Tanzania PANORAMA kuhusu mkasa wa kuibiwa fedha zake, Nsyenge anadai alifungua akaunti ya mkulima kwenye benki hiyo mwaka jana baada ya kufanyika kwa warsha ya kutambulisha fursa zinazoweza kupatikana kwa wakulima wa zao wa Parachichi kutoka Benki ya NMB.

Anadai wawasilishaji mada katika warsha hiyo waliwashawishi wakulima kufungua akaunti maalumu ya kilimo ambayo ingekuwa na ‘service charges’ za chini ikilinganishwa na za akaunti ya biashara na kwamba wangepata fursa ya kupewa mikopo kwa ajili ya kilimo cha zao la Parachichi.

Nsyenge anadai alifungua akaunti kwenye benki hiyo Februari 9, 2023 baada ya kupata fedha za mauzo yake ya kwanza ya zao la Parachichi na Februari 18, 2023 akiwa mkoani Mbeya alikwenda kwa wakala wa NMB na kutoa kiasi cha fedha, kisha Februari 19, 2023 alitoa kiasi kingine cha fedha kupitia kwa wakala  akiwa Mafinga.

Anaendelea kudai kuwa siku iliyofuata, Februari 20, 2023 alikwenda tena kwa wakala kwa ajili ya kutoa fedha lakini aliambiwa kuwa salio lake kwenye akaunti ni Shilingi 6,860 tu jambo ambalo lilimshtua kwa sababu akaunti yake ilikuwa bado na kiwango kikubwa cha fedha kuliko hicho alichoambiwa kimesalia.

Nsyenge anadai Februari 23, 2023 alikwenda NMB Mafinga kwenye dawati la huduma kwa wateja na kuhoji kilichotokea kwenye akaunti yake na kumpatia mfanyakazi wa benki hiyo kadi yake ili afuatilie na kumpatia majibu.

“Baada ya kuperuzi, swali la kwanza lilikuwa je ulifungua akaunti ya biashara nikamwambia hapana nilifungua akaunti ya mkulima baada ya kishawishiwa kwenye warsha iliyofanyika kwenye ukumbi mdogo wa CF Kinyanambo na swali la pili aliloniuliza ni akina nani walikuwepo nikamjibu ninaowakumbuka ni Fredy Mung’ongo, Santina Kiluka, Mama Timbla, Mama Mwapinga na Mama Dermokrasia Mbilinyi.

“Swali la tatu aliloniuliza ni je waliwatajia kiwango cha ‘service charges’ nikamjibu hapana. Baada ya kuona anakosa majibu na wateja walikuwa wanazidi kujaa katika dirisha lake na pia baada ya kugundua suala langu ni ‘technical issue,’ kwa hekima yangu nilimshauri akatishe mazungumzo na mimi ili aendelee kuwahudumia wateja wengine,” anadai Nsyenge.

Anadai zaidi kuwa baada ya kutoka hapo alifuatilia makato ya ‘service charges’ kwa Mucoba na kugundua kuwa ni Shilingi 1,500 tu kabla ya kuwasiliana na Meneja wa Benki ya MNB Tawi la Mafinga, Focus Lubende ambaye baada ya kufuatilia madai yake alibaini kuwa fedha zake ziliibiwa na wafanyakazi wa benki hiyo zikiwa kwenye akaunti yake na Lubende aliwataka wamrejeshee fedha zake pamoja na gharama za mwanasheria aliyekuwa amemlipa malipo ya awali kwa ajili ya kuishtaki benki hiyo.

Alipoulizwa Lubende kuhusu madai ya Nsyenge kuibiwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti na wafanyakazi wa NMB, kwanza alisema hajui lolote kuhusu wizi huo lakini alipoulizwa kwa msisitizo kama ana uhakika suala hilo halijawahi kufikishwa mezani kwake alibadili kauli yake na kusema yeye haruhusiwi kuongea na waandishi wa habari kwa njia ya simu.

Lubende alishauri badala ya mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog kuongea naye kwa simu afike ofisini kwake kwa mazungumzo vinginevyo alisisitiza kuwa yeye haruhusiwi kuongea na waandishi wa habari kwa njia ya simu na kwamba haruhusiwi kutoa habari za benki kwa waandishi wa habari hata kama zinahusu tawi analoliongoza.  

PANORAMA imemtafuta Kaimu Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilaino wa Benki ya NMB, Vicent Mnyanyika na kumuuliza maswali haya kuhusu madai yaliyotolewa na Nsyenge;

1) Kuna malalamiko kutoka kwa wateja wa NMB Tawi la Mafinga kuwa wanaibiwa fedha zao kwenye akaunti na wafanyakazi wa tawi hilo. Tukitambua dhamana kubwa ya taasisi za kifedha na tukitambua pia ukubwa wa taasisi yako na imani waliyonayo wateja kwenu, tunaomba kupata kauli yako kuhusu suala hilo.

2) Wateja walioibiwa fedha zao na wafanyakazi wa NMB Mafinga walioongea nasi wanadai kuwa badala ya fedha zilizoibiwa kurudishwa kwenye akaunti zao, wamekuwa wakirudishiwa kwa kupewa mkononi. Tunaomba kujua utaratibu unaotumiwa na NMB kurudisha fedha za wateja wake zilizobainika kuibiwa na wafanyakazi wake kutoka kwenye akaunti za wateja.

3) Imeelezwa na wateja walioibiwa fedha zao na wafanyakazi wa NMB Mafinga kuwa meneja wa tawi hilo baada ya kuwabaini wafanyakazi waliohusika na wizi huo amekuwa akiwaita na kuwakutanisha na wateja walioibiwa kisha anawaomba wawarudishie fedha hizo. Tunaomba kujua, je utaratibu huo  unaotumiwa na meneja huyu kushughulikia vitendo hivyo vya wizi ndio utaratibu rasmi wa benki yako? Na kama sio sahihi, ni utaratibu upi unaotumiwa na NMB kwenye kadhia kama hii?

4) Wateja walioibiwa fedha zao katika tawi hilo wanadai kuwa baada ya kuwabaini wezi na kufikishwa mbele ya Meneja wa Tawi na kuombwa kurejesha fedha wamekuwa wakizirejesha kwa mafungu jambo ambalo linawasababishia usumbufu na hasara katika shughuli zao za uzalishaji. Tuomba kujua NMB inawajibikaje kulinda fedha za wateja wake?

Akijibu Mnyanyika aliandika; Benki ya NMB haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa mteja yeyote kwenye tawi letu la Mafinga. Tunachukulia kwa uzito tuhuma zilizotolewa na kuelekezwa kwa baadhi ya wafanyakazi wetu kwani zina lengo zuri la kuifanya Benki ya NMB kuendelea kuwa namba moja kwenye kusimamia maadili.

Hata hivyo, tunashauri kama kuna mteja ambaye hajaridhika na huduma zetu kwenye tawi tajwa, tunamshauri awasiliane nasi kupitia njia zetu rasmi za mawasiliano ili tuweze kumsaidia kutatua shida yake.

USIKOSE KUTEMBELEA TANZANIA PANORAMA KESHO KUJUA MWENDELEZO WA SAKATA HILI. 

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya