*Awataka wahakikishe wananchi wanapata elimu na taarifa sahihi
RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini waongeze ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma badala ya kusubiri kazi zifanywe na waandishi wa habari wengine.
Aliyasema hayo Machi 27, 2023 wakati akifungua kikao kazi cha 18 cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kilichoanza kilichofanyika kwenye Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Mnapofanya kazi ongezeni ubunifu wa kusukuma ajenda za Serikali kwa umma na msisubiri kazi zifanywe na wanahabari wengine. Hakikisheni kila mwananchi anapata elimu na taaarifa sahihi kuhusu faida na umuhimu wa miradi na mipango au shughuli zinazotekelezwa na Serikali,” alisema.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Majaliwa alisemaMaafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini wana wajibu wa kuhakikisha yanayopangwa na kutekelezwa na Serikali yanafahamika kwa umma wa Watanzania kwa usahihi, kwa wakati na kwa tija.
Alisema maafisa hao wanapofanya mawasiliano hasa ya kimkakati, wahakikishe wanafahamu lengo la mawasiliano wanayotaka kufanya, faida na matarajio ya kutekeleza mawasiliano husika, nani mlengwa wa mawasiliano hayo pamoja na kuchagua njia sahihi za mawasiliano.
“Nimeona nisisitize hayo kwa kutambua kuwa mafanikio ya Serikali hayana budi kufahamika kwa wananchi wote na ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha mawasiliano hayo yanakuwa ya kimkakati ili yaweze kuleta tija na kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema.
Ili kuwawezesha maafisa hao kutekeleza majukumu yao, Majaliwa aliwaagiza makatibu wakuu, wakurugenzi wa halmashauri na taasisi za umma kutenge bajeti ya kutosha kugharamia shughuli za utoaji wa taarifa pamoja na elimu kwa umma na kuhakikisha jukumu hilo linatekelezwa kwa tija na ufanisi uliokusudiwa.
Pia aliwataka viongozi wa wizara na wakuu wa taasisi waweke kipaumbele cha kuwashirikisha maafisa habari kwenye vikao mbalimbali ikiwemo vikao vya menejimenti ili waweze kwenda na wakati na kupata ufahamu wa kutosha wa taasisi na mipango ya Serikali.

Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema wizara hiyo ipo katika hatua za mwisho kukamilisha utayarishaji wa mkakati wa Taifa wa mawasiliano kwa umma (The National communications strategy) ambao ukikamilika utaainisha na kufafanua utaratibu wa upatikanaji na usambazaji wa taarifa za Serikali kwa umma.
“Pamoja na mkakati huo, tuko kwenye hatua za mwisho za uandaaji wa mkakati wa mawasiliano serikalini wakati wa majanga (Risk Communication Strategy) na mkakati wa Taifa wa kujitangaza (National Branding Strategy),” alisema.
Alisema mkakati huo utakapokamilika na kuanza kutumika unatarajiwa kuweka misingi ya kusimamia usambazaji wa taarifa zenye maudhui ya ajenda za kitaifa, kuboresha mbinu na teknolojia ya ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa taarifa za Serikali kwa wananchi na kuweka mfumo madhubuti wa namna Serikali inavyopaswa kutoa ufafanuzi, kukanusha ama kutuliza na kuwatoa hofu wananchi pale ambapo kutatokea mkanganyiko au taarifa za upotoshaji.
Pia alimkabidhi tuzo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kuimarisha sekta ya habari, demokrasia, uwazi, uhuru wa kutoa maoni na kupata taarifa nchini.
Kikao kazi hicho kinachotarajiwa kumalizika Machi 31, 2023 kinahudhuriwa na washiriki zaidi ya 500 ambao ni Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kwenye wizara mbalimbali, taasisi za umma, halmashauri na idara zinazojitegemea. Kaulimbiu ya mwaka huu ni mawasiliano ya kimkakati, injini ya maendeleo.