RIPOTA PANORAMA
WAFANYAKAZI wa benki moja kubwa hapa nchini (jina tunalihifadhi kwa sasa) wanadaiwa kuwaibia wateja fedha zilizo kwenye akaunti zao.
Madai ya kuwepo kwa wizi huo yametolewa na baadhi ya wateja wa benki hiyo waliozungumza na Tanzania PANORAMA Blog hivi karibuni.
Mmoja wa wateja wa benki hiyo (jina lake tunalihifadhi kwa muda) ambaye ametoa madai ya kuibiwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti yake amesema baada ya kubaini wizi huo aliwasiliana na uongozi wa benki hiyo ambao ulikiri wafanyakazi wake kuhusika na tukio hilo la wizi na kumuomba samahani huku ukiwaelekeza wafanyakazi wanaodaiwa kuiba kulipa fedha za mteja huyo.
Alisema meneja huyo wa benki aliwaita wafanyakazi waliohusika na tukio hilo ofisini kwake na kuwataka wamlipe mteja huyo fedha zake huku akiahidi pia kumlipa gharama za malipo wa mwanasheria aliyekuwa amempa jukumu la kuishtaki benki hiyo.
Akisimulia jinsi alivyobaini wizi huo alisema alipokwenda kuchukua fedha zake benki alikuta zimetolewa na kubakiziwa Shilingi 6,860 na alipokwenda kwa mmoja wa wafanyakazi kutaka kujua kilichotokea kwenye akaunti yake, alikosa majibu na kumpeleka kwa ‘supervisor.’
Alisema ‘supervisor’ huyo naye alikosa majibu ya jinsi wizi huo ulivyofanyika na alimuomba amuachie namba yake ya simu kwa ajili ya kuwasiliana naye baada ya kufanya uchunguzi wa suala hilo.
Akiendelea kusimulia tukio hilo, alisema baada ya kuona wafanyakazi wa benki hiyo wanashindwa kumpa majibu aliangalia ‘bank statement’ yake na kubaini kuna makato ambayo yameandikwa kwa namna ambayo mtu asiyekuwa na uelewa wa mambo ya kibenki hawezi kugundua kuwa siyo ya halali.
Alisema baada ya kugundua jambo hilo aliwasiliana na mwanasheria ambaye alimshauri kupeleka malalamiko yake kwa maandishi kwa meneja wa benki hiyo na kwamba amfikishie mwenyewe mezani kwake.
“Nilipofika kwa meneja na kumweleza kuna barua yako hii aliisoma akasema we bwana vipi mbona unaniambia rejea barua yangu, mbona mimi sina barua hapa mezani. Nikamwambia ipo kwenye deski la watu wako hapa hapa ndani. Ipo kwa ‘supervisor’ wako.
“Akawasaliana na ‘supervisor’ akasema ni kweli, wakazungumza pale baada ya kuzungumza wakasema kama ni hivyo, tunaomba samahani, uniachie hili jambo niweze kulishughulikia, waniletee faili niweze kulikagua, basi mimi nikaondoka.
“Saa tisa au saa kumi ‘supervisor’ akanipigia simu akaniambia baba samahani tunaomba uje uchukue hela yako hapa benki, nikamwambia hili jambo siyo rahisi kama unavyolichukua. Kwangu naliona ni jambo nyeti, inawezakana nyie mnaona siyo jambo nyeti lakini kwangu naona ni jambo nyeti,” alisema.
Alisema baada ya kumweleza hayo alimtaarifu pia kuwa amekwishawasiliana na mwanasheria hivyo hawezi kufanya jambo lolote nje ya maelekezo ya mwanasheria wake.
Alisema baadaye alipigiwa simu na meneja wa benki hiyo akimuomba afike ofisini kwake kwa mazungumzo lakini hakuweza kufika mara moja kwa sababu alikuwa safarini na badala yake alikwenda kuonana naye wiki moja baadaye na kumpa masharti ya kukubaliana na matakwa yake vinginevyo atachukua hatua za kisheria.
“Nikazungumza naye akasema bwana tunaomba utusamehe sana sana kwa jinsi tulivyolifanya hili jambo, kwa mujibu maadili ya benki, maana yake sisi system nzima hapa ya benki inapanguliwa, inafukuzwa kazi,” alisema.
Alisema baada ya meneja huyo kumlilia hali, alimwambia kwa vile amejua watu wake wanafanya mambo hayo na wamekuwa wakiwaibia wateja kwa namna mbalimbali kwa sababu hawajui lugha za kibenki, wamrudishie fedha zake na walipe gharama za mwanasheria wake alizokuwa amemlipa kama malipo ya awali ya kuendesha kesi yake dhidi ya benki hiyo.
“Basi akanisihi hapo akaniambia acha niwakamate wale vijana wakusanyesanye hiyo hela yako, wakakusanya baadaye akanambia bwana haijapatikana hela yote, naomba hii iliyopo uchukue,” alisema.
ILI KUJUA UNDANI WA SAKATA HILI, SOMA TANZANIA PANORAMA KESHO.