RIPOTA WA WAZIRI MKUU
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wanawake wote na Watanzania kwa ujumla waendelee kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotokana na matumizi ya teknolojia katika kujenga uchumi wa kidijitali.
Wito huo leo mchana, alipokuwa akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano mkuu wa tano wa mwanamke kiongozi kwa mwaka 2023 uliofanyika kwenye Hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliambatana na mahafali ya nane ya programu ya mwanamke kiongozi ambapo jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti. Washiriki 11 wa programu hiyo walijidhamini wenyewe na wengine 54 wanatoka kwenye kampuni 29.
Akitoa msisitizo kuhusu umuhimu wa mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema: “Wanawake wajitokeze kwa wingi kushiriki katika programu hii kwani imeendelea kuwa na matokeo chanya kwa washiriki na kuleta mabadiliko makubwa kwenye utendaji wao wa kazi na kugusa maisha yao binafsi.
“Pia nitoe rai kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kiendelee kutoa mafunzo haya ya uongozi kwa wanawake pamoja na kuendelea kuwa vinara wa usawa wa kijinsia katika maeneo ya kazi,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Amesema suala la mabadiliko ya kidigitali ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwani maendeleo ya uchumi yanategemea zaidi utandawazi.
“Lakini pia katika mabadiliko haya ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika uchumi wetu na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi wa kidijitali,” amesema.
Kuhusu Serikali kutambua umuhimu wa uchumi wa kidijitali, amesema Serikali imeendelea kubuni mikakati ambayo itaiwezesha nchi kutumia vema fursa za kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi.
“Ili kutimiza azma hiyo, tayari Mkakati wa Taifa wa Brodibandi wa Mwaka 2021–2025 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo mwaka 2025 umeshaandaliwa. Serikali inaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali,” amesema.
Mapema akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM)Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa. Joyce Ndalichako alisema ofisi yake kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) wataendelea kusimamia sheria za kazi na masuala ya ajira nchini na kuweka mazingira rafiki katika sehemu za kazi.
Akielezea kuhusu suala la kima cha chini cha mshahara kwenye sekta binafsi, Profesa. Ndalichako alisema: “Utekelezaji wa kima cha chini ulianza Januari Mosi, 2023. Niwasihi ATE waendelee kutoa elimu na kuwasimamia wale ambao bado hawajatekeleza kikamilifu kwani hiyo ni haki ya kila mfanyakazi.”
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima alisema Serikali imewainua wanawake kiuchumi kwa kuwapatia fursa za kiteknolojia na mikopo yenye masharti nafuu ili waweze kupambana na ukatili wa kijinsia.
Alisema Serikali imeratibu programu ya kuwezesha wanawake katika maendeleo na mwelekeo wa kidijitali ili wafahamu masuala ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hesabu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Dk. Saada Salum Mkuya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wawakilishi Wanawake Zanzibar (UWAWAZA) yeye aliiomba ATE iangalie uwezekano wa kupeleka hadi ngazi ya chini zaidi programu ya mwanamke kiongozi ili iweze kuibua vipaji vingi zaidi.
“ATE iangalie uwezekano wa kushuka hadi shule za sekondari na vyuo vikuu ili kuibua vipaji vya wanawake wengi zaidi,” alisema Mkuya.
Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Doran alisema tangu kuanza kwa programu hiyo kwa kushirikiana na ESAMI, wamekwishatoa mafunzo kwa wanawake 274 kutoka kampuni 79 wakiwemo wabunge na wawakilishi 150.