Florida, Marekani
RAIS wa zamani wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuwania tena nafasi ya urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika 2024.
Trump alitangaza nia yake hiyo wiki moja baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula, akiwa katika jumba lake la kifahari la Mar – a – Lago lililo Florida wakati akizungumza na wafuasi wake kuhusu mwenendo wa kisiasa nchini humo na siasa za kimataifa.
“Mabibi na mabwana, wageni waheshimiwa na raia wenzangu, Marekani inaanza sasa kurejea kwenye utukufu wake,” alisema Trump.
Katika hotuba yake hiyo iliyochukua takribani saa moja na iliyoshangiliwa sana na wafuasi wake waliokuwa wamefurika kwenye ukumbi wa jumba lake hilo, alisema amedhamiria kuirejesha Marekani kwenye utukufu wake ambao alianza kuujenga wakati wa utawala wake wa miaka minne kabla ya kukatishwa njiani, mwaka 2020 na Rais Joe Biden aliyemshinda kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka huo.
“Lakini daima tumejua kuwa huo haukuwa mwisho, ulikuwa mwanzo tu wa mapambano yetu kuiokoa ndoto ya Marekani. Ili kuirejeshea Marekani utukufu na heshima yake, usiku huu natangaza kuwania urais wa Marekani,” alisema Trump.
Trump ambaye alizungumza na wafuasi wake baada ya chama chake cha Republican kushindwa kupata viti vingi kwenye Baraza la Congress, aliyalinganisha mafanikio yake wakati akiwa Rais na utawala wa sasa wa Rais Biden huku akitumia lugha kali dhidi ya wahamiaji.
Alisema miji ya Marekani imegeuka majalala yaliyojaa uhalifu na damu kutokana na wageni waliofurika nchini humo.
Akizungumza kuhusu siasa za kimataifa, Trump alisema wakati wa utawala wake alizidhibiti nchi hasimu na zilimuheshimu kwa sababu alizijua vizuri.
“China, Urusi, Iran na Korea Kaskazini zilidhibitiwa na kuheshimiwa, waliiheshimu Marekani na ni wazi kuwa waliniheshimu mimi. Niliwajua vema,” alisema Trump.
Wakati Trump akitangaza nia yake hiyo, binti yake, Ivanka Trump ambaye wakati wa urais wake alimchagua kuwa mshauri wake mkuu maalumu alisema hataungana na baba yake kwenye mbio zake za urais za 2024.
“Nampenda sana baba yangu lakini safari hii nimechagua kuwaweka mbele watoto wangu wadogo na maisha ya faragha kama familia. Sipangi kuingia kwenye siasa ingawa nitampenda na kumuunga mkono baba yangu siku zote.
“Ninashukuru kupata nafasi ya kuwatumikia watu wa Marekani katika maisha yangu, ninayo fahari kwa mafanikio mengi yaliyopatikana wakati wa utawala wetu,” aliandika Ivanka kwenye mtandao wa Twitter.
Rais Biden alikataa kuzungumzia uamuzi wa Trump kuwania tena urais hata hivyo aliutumia ukurasa wake katika mtandao wa Twitter kuikosoa rekodi ya Trump wakati akiwa madarakani.