Thursday, July 17, 2025
spot_img

RAIS SAMIA ACHAPA MWENDO UJENZI WA BARABARA

RIPOTA TANROADS

RAIS Samia Suluhu Hassan amekaza mwendo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Hayo yalielezwa hivi karibuni mkoani Mbeya na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara; sehemu ya Msagala hadi uwanja wa ndege yenye urefu wa kilomita 29.

Prof. Mbarawa alisema kukamilika kwa miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara na kuitaja barabara ya Igawa, Uyole, Songwe hadi Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 ni miongoni mwa kazi kubwa zinazotekelezwa na Rais Samia katika sekta ya miundombinu.

Alisema manufaa ya ujenzi wa barabara hiyo yenye njia nne na inayojengwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na kuwaondolea wananchi kero ya msongamano, kuondoa ajali na kurahisisha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo.

Prof. Mbarawa aliwataka wakazi wa Mkoa wa Mbeya na Songwe kuchangamkia fursa za uzalishaji ili kunufaika na uwepo wa barabara hiyo.

“Bidhaa za Nchi za Malawi, Zambia na Congo zinazokwenda na zinazotoka Bandari ya Dar es Salaam zitafika kwa urahisi itakapokamilika barabara hii, hivyo ni wakati kwa wakazi wa Nyanda za Juu Kusini kutumia fursa ya uwepo wa barabara hiyo itakapokamilika,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akiteta na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Msagati hadi Uwanja wa Ndege. hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni mkoani Mbeya.

Waziri huyo aliutaka Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa katika ujenzi wa barabara hiyo na kukamilika kwa wakati ili kuchochea uchumi wa wananchi wa mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Nia ya Serikali ni kuhakikisha inaboresha miundombinu ili wananchi watumie fursa hizo kukuza uchumi binafsi na wa Taifa kwa ujumla,’ alisisitiza.

Naye Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ambaye alihudhuria hafla hiyo, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha miundombinu nchini hususan mkoani Mbeya hali itakayochochea kupanda kwa uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

“Barabara hiyo inayounganisha Tanzania na Nchi za Malawi na Congo ikikamilika itakuza biashara katika Jiji la Mbeya,” alisema Dk. Tulia.

Alisema Barabara ya Igawa, Uyole, Songwe hadi Tunduma ni sehemu ya Barabara Kuu ya TANZAM na barabara kuu ya nne inayotoka Cape Town, Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri.

HABARI HII ILIANDIKWA KWANZA KATIKA JARIDA MAALUMU LA TANROADS LA FEBRUARI, 2023. KUTOKANA NA UMUHIMU WAKE, TANZANIA PANORAMA BLOG INAICHAPISHA ILI KUWAFIKIA WASOMAJI WAKE WA NDANI NA NJE YA NCHI.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya