Monday, December 23, 2024
spot_img

MAMILIONI YA JUMUIYA YA DINI YADAIWA KUCHOTWA BENKI

RIPOTA PANORAMA

MAMILIONI ya Fedha za Jumuiya ya KSIJ Tanga Jamaat yaliyokuwa yamehifadhiwa katika benki moja iliyopo mkoani Tanga yanadaiwa kuchotwa kinyemela na mtu anayetajwa kwa jina la Sajad Khakoo.

Taarifa kutoka vyanzo vya habari vilivyo ndani ya KSIJ Tanga Jamaat zimedai kuwa Khakoo na mmoja wa wanafamilia yake ambaye ana umri ulio chini ya miaka 18 wamekuwa wakichota mamilioni ya fedha za jumuiya hiyo kwa nyakati tofauti.

Yeye mwenyewe Khakoo alipoulizwa kuhusiana na madai hayo, alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya KSIJ Tanga Jamaat ndiye mtu sahihi wa kujibu maswali yote ya jumuiya hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walji ambaye PANORAMA imekuwa ikijitahidi kupata kauli yake kuhusu madai na tuhuma lukuki anazoelekezewa na wanajumuiya, badala ya kujibu amekuwa akituma picha alizopiga na viongozi mbalimbali wa kitaifa kupitia simu yake ya mkononi na muda mfupi baadaye anazifuta.

PANORAMA imeelezwa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya KSIJ Tanga Jamaat, kifungu cha 20 (e) mwenyekiti wa jumuiya anaruhusiwa kutoa kiasi kisichozidi Shilingi 100,000 katika ukaunti ya jumuiya iwapo kuna dharura na kwamba mwenyekiti haruhusiwa kumtuma mtu ambaye siyo kiongozi wa jumuiya kwenda kuchukua fedha hizo benki.

Kifungu hicho cha Katiba kinaeleza zaidi kuwa iwapo itahitajika fedha zaidi ya Shilingi 100,000 kutolewa katika akaunti ya jumiya ni lazima kuwepo kibali cha wanachama cha kutolewa kwa fedha hizo.

Wakati Katiba ikieleza hivyo, Khakoo na mwanafamilia yake wanadaiwa kuchota mamilioni ya fedha kutoka kwenye akaunti ya KSIJ Tanga Jamaat na kwamba Mwenyekiti Hussein Walji anayedaiwa kuiongoza jumuiya hiyo kwa mkono wa chuma hana mweka hazina, katibu wala mjumbe yeyote anayeshirikiana naye katika uongozi.

Mwenyekiti wa KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walji

“Fedha za Jumuiya zinachotwa benki kwa mamilioni na watu wajanja, wanachukua fedha za jumuiya kutoka benki kinyume kabisa cha taratibu. Huyo Khakoo siyo kiongozi wa jumuiya lakini amekwishachota mamilioni ya fedha benki mara tatu na mjukuu wake ambaye hata hajafikisha umri wa miaka 18 naye amekwishachukua fedha hizo.

“Haya yote yamo kwenye ripoti ya uchunguzi uliofanywa na polisi kuhusu mgogoro wa uongozi wa KSIJ Tanga Jamaat maana waliwahoji wahusika na baadhi ya wanajumuiya pia walihojiwa na polisi walipata ushahidi wa kuchotwa kwa fedha hizo. Uchunguzi huo ukiwekwa wazi utaonyesha wazi kila kitu.

“Wazee, wajane na watu wasiojiweza wanakosa usaidizi kama yalivyo malengo ya jumuiya yetu wakati watu hawa wajanja wanachota fedha benki kutoka kwenye akaunti ya jumuiya wanazitia mfukoni. Tunaomba kilio chetu kisikike kwa mamlaka husika hatua zichukuliwe kwa sababu polisi walishafanya uchunguzi na kubaini kila kitu,” kilidai chanzo chetu cha habari.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi (ACP) Henry Mwaibambe katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA kuhusiana na mgogoro wa KSIJ Tanga Jamaat alisema hana taarifa kuhusu mgogoro huo na iwapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga lilifanya uchunguzi wa suala hilo lakini aliahidi kufuatilia jalada la kesi hilo na kutoa taarifa.

Taarifa nyingine zilizopatikana kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga zinadai kuwa tayari faili la mgogoro huo lilikwishakabidhiwa kwa RPC Mwaibambe naye baada ya kulipitia, alimuita ofisini kwake Mwenyekiti wa KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walji kwa mahojiano na kwamba aliwaita pia baadhi ya waandishi wa habari wa mkoani Tanga (Tanzania PANORAMA blog ambayo ilikuwa ya kwanza kuripoti mgogoro huo haikualikwa) na kuwapa ufafanuzi wa mwenendo wa uchunguzi wa polisi kuhusu mgogoro huo.

Inadaiwa Septemba 19, 2022 Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa aliuandikia barua  uongozi wa jumuiya hiyo kufika ofisi kwake kwa ajili ya kuzungumzia malalamiko ya wazee, wajane na watu wenye ulemavu wanaosaidiwa na KSIJ Tanga Jamaat lakini agizo lake hilo halikutekelezwa kwa madai kuwa wito huo ulichelewa kufika.

Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani alipoulizwa na Tanzania PANORAMA kuhusu hilo alisema mambo ya jumuiya za kidini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi na heshima za jumuiya za aina hiyo.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya