RIPOTA PANORAMA
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amesema itaiagiza Jumuiya ya KSIJ Tanga Jamaat kuwasilisha ofisini kwake hesabu za fedha za kipindi cha miezi mitatu iliyopita kabla ya kukutana na wana jumuiya hiyo kusikiliza malalamiko yao dhidi ya Mwenyekiti wao, Hussein Walji.
Akizungumza leo na Tanzania PANORAMA Blog, RC Mgumba amesema malalamiko dhidi ya wahitaji hao yana tuhuma za kufujwa kwa fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi ya wazee, wajane na wasiojiweza hivyo Serikali itayafanyia kazi kwa sababu kuna jinai ndani yake.
RC Mgumba ametoa kauli hiyo baada ya kuibuka malalamiko ya makundi hayo dhidi ya Mwenyekiti wa KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walji anayetuhumiwa kwa matumizi mabaya ya fedha za jumuiya hiyo, kudhulumu fedha za wahitaji kwa kuwasainisha vocha za malipo zinazoonyesha kiwango kikubwa cha fedha lakini anawapatia kiasi kidogo, kuchukua uongozi kwa nguvu na kusababisha vurugu ndani ya jumuiya hiyo.
“La kwanza, kwa sababu kuna tuhuma hapo za kufujwa kwa fedha za umma zilizochangwa kusaidia makundi hayo, sisi kama Serikali nafikiri hiyo ni NGO’s, Shirika Lisilokuwa la Kiserikali na kwa kuwa ndiyo unanipa taarifa. Nilikuwa sina taarifa kuhusu hilo suala, naomba nilifanyie kazi.
“Sisi kama Serikali, kwa sababu kuna jinai na wana utaratibu wa kuleta taarifa zao na hizo bado ni tuhuma hazijathibitishwa, basi ngoja tupate taarifa ya kwao hiyo taasisi kwa mujibu wa sheria kwa sababu wanatakiwa walete taarifa kila robo mwaka na Katibu Tawala wa Mkoa ndiyo mratibu wa mambo hayo, basi nitaomba taarifa hiyo waniletee.
“Nikipata hiyo taarifa ndiyo nitakuwa na nafasi ya kusema chochote lakini jambo la pili baada ya hiyo taarifa nitaenda hapo kuongea na hao wazee walalamikaji ili nikapate ukweli wa upande wa pili,” amesema RC Mgumba.
Mkuu huyo wa mkoa pia alitoa wito kwa wanafamilia kuwalee wazee, watoto na ndugu wasiojiweza badala ya kuwakimbia. “Lakini jambo la tatu nitoe wito kwa wanafamilia, tuwalee wazee wetu, tuwalee watoto wetu, tuwalee ndugu zetu, tusiwakimbie kwa sababu naamini wote wana ndugu hao.”
Aidha, RC Mgumba aliwataka wahitaji kutambua hali ya maisha kwa sasa imebadilika hivyo hata wahisani nao wamepunguza misaada wanayotoa na kutoa mfano kuwa hata wahisani waliokuwa wakitoa misaada kwa Serikali nao wamepunguza kiwango cha utoaji wa misaada yao.
“Lakini la mwisho hata wale wanufaika maana yake tumeenda pale tunasaidiwa, tunasaidiwa kwa sababu hali ya maisha imekuwa ngumu. Wasamaria wema wanachangia wanatusaidia.
“Sasa wale wanaokusaidia nao wakisema maisha magumu, misaada ikipungua usilalamike wakati jukumu hilo ndugu zetu sisi wenyewe tulilishindwa. Hali ya maisha duniani kote sasa hivi imebadilika ile misaada iliyokuwa inatolewa wakati ule haiwezi kufanana na sasa hivi.
Hata sisi Serikali hao waliokuwa wanatusaidia, rafiki zetu, kiwango cha misaada waliochokuwa wanatutumia zamani kina tofauti kubwa sana na sasa kwa sababu aidha nao hali imekuwa ngumu la pili inawezekana mahitaji yao yamekuwa makubwa kuliko mapato wanayopata.
“Au sasa hivi wanajua kuwa tumeishaimarika tunaweza kujisaidia sisi wenyewe. Kwa hiyo hayo yote yawe ni mafundisho, siyo mtu akikwambia anakusaidia inakuwa ni permanent mpaka kufa, Hapana,” amesema RC Mgumba.