Monday, December 23, 2024
spot_img

VURUGU ZAIDI ZARIPOTIWA KSIJ TANGA JAMAAT

RIPOTA PANORAMA

MWENENDO wa mambo katika jumuiya ya kidini ya KSIJ Tanga Jamaat si shwari ambapo habari za hivi karibuni zinadai kuzuka kwa vurugu pamoja na kutimuliwa kwa wawakilishi wa Shirikisho la Jamaat Afrika waliokuwa wakihudhuria mkutano ulioitishwa kujadili hali ya jumuiya hiyo.

Taarifa zilizopatikana hivi karibuni kutokana ndani ya jumuiya hiyo zinadai kuwa katika mkutano huo kulizuka vurugu baada ya Mwenyekiti wa KSIJ Tanga Jamaat, Hussein Walje kuzuia hoja za wajumbe kujadiliwa huku mpambe wake, Gulam Peera akidaiwa kuibua vurugu na kuwatimua wawakilishi wa Shirikisho la Jamaat Afrika waliotumwa kama wawakilishi wa jumuiya kwenye mkutano huo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Tanzania PANORAMA Blog kutoka ndani ya jumuiya hiyo, wanachama wanashinikiza mwenyekiti wao Walje aachie ngazi kwa sababu alipoka kwa nguvu wadhfa wa uenyekiti na kwamba ana rekodi ya uhalifu na alipata kutiwa hatiani na mahakama kwa makosa ya wizi.

Mwenyekiti Walje pia anatuhumiwa kufuja fedha za jumuiya pamoja na kudhulumu fedha zinazotolewa na Shirikisho la Afrika kwa ajili ya kusaidia watu masikini hususan wanawake wajane na walemavu.

Inadaiwa, katika mkutano huo uliofanyika Julai mwaka jana Mwenyekiti Walje alijiandaa kukabiliana na wajumbe wanaoshinikiza ang’oke madarakani kwa kuwazuia wasitimize azma yao hiyo akisaidiwa na Peera.

“Hii migogoro kwenye jumuiya hizi za kidini mwisho wake huwa si mzuri kwani huwa kuna visasi ndani yake vya siri siri. Kwenye Jamaat hapa tuna mgogoro wa muda mrefu mpaka watu wanatishiwa, Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani anajua, Polisi Tanga wanajua kuwa mgogoro huu sasa upo pabaya lakini hatuoni hatua kuchukuliwa.

“Siku ya mkutano wa Julai mwaka jana, wawakilishi kutoka Shirikisho la Afrika walikuwepo, na ujue huyu mwenyekiti Walje alijipa uenyekiti kwa nguvu, hakuchaguliwa, sasa nadhani alijua siku hiyo anang’olewa mbele ya wale wawakilishi kwa hiyo alijiandaa.

“Pale mbele aliweka kiti cha mpambe wake Gulam Peera na wakati mkutano unaanza, alianza kubabaika kuhakiki wanachama halali, akawa anampigia simu mtu mwingine ambaye hakuwepo mkutanoni akawa anamsaidia kumpa maelezo. Ujue huyu anaongoza hii jumuiya peke yake, hana katibu, hana mweka hazina wala wajumbe; kinyume kabisa cha Katiba yetu,” kinasema chanzo chetu cha habari.

Taarifa zinadai zaidi Mwenyekiti Walje kwa sababu ya kutojua idadi wa wanachama hai wa jumuiya anayoiongoza alitangaza kuwa mtu yoyote ambaye si mwanajumuiya aliyesajiliwa hapaswi kuwa ndani ya ukumbi wa mkutano lakini tangazo lake hilo lilikosolewa na wawakilishi wa Shirikisho la Jamaat Afrika walioelekeza kuwa kwa sababu watu walio ndani ya ukumbi ni sehemu ya jamii siyo busara kuwafukuza ila hawapaswi kuongea bila idhini yake mwenyekiti.

Inadaiwa zaidi kuwa mwenendo wa mkutano huo ulianza kwenda mrama zaidi baada ya kuwasili kwa Gulam ambaye alikuwa amewekewa kiti upande wa mbele na baada ya kuketi alianza kuongea bila kufuata utaratibu huku mwenyekiti akimpa uhuru wa kufanya atakavyo.

“Dalili za mkutano kuharibika zilionekana mapema lakini zilikuwa wazi baada ya Gulam Peera kufika na ujue huyu Gulam Peera naye ana mambo mengi sana, hapa Tanga anaogopwa sana huyo, uliza wenyeji wa hapa watakupa habari na jinsi anavyowatendea watu anaotofautiana nao hapa Tanga. Huyu habari zake zitakujia baadaye kwa undani ila ndani ya kikao kulikuwa na kurekodi pia jambo ambalo siyo utaratibu wetu.

“Pamoja na hoja nyingine zilizojadiliwa kulikuwa na hoja ya kumwondoa mwenyekiti kwa sababu ya kuingia madarakani kinyume cha Katiba, kuvunja Katiba na kuwa kesi polisi pamoja na wana jumuiya ambayo baada ya kuwasilishwa, mwenyekiti aliikataa kibabe.

“Gulam naye akaanza kupiga kelele huku akipiga meza. Wawakilishi wa Shirikisho la Jamaat Afrika walipojaribu kumsihi atulie na mwenyekiti awasikilize wajumbe, Gulam akawaambia wao ni watazamaji tu hawapaswi kusema lolote hata wakiulizwa na wajumbe wakae kimya,” anadai zaidi mtoa taarifa wetu.

Tanzania PANORAMA Blog imethibitishiwa kuwa mkutano huo ulifungwa kibabe huku wawakilishi wa Shirikisho la Jamaat Afrika wakitimuliwa na kwa upande wa wanajumuiya waliokuwa wakitaka haki za walemavu na wajane kupata misaada inayotolewa na shirikisho zizingatiwe wakiachwa bila majibu.

Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa

Mwenyekiti Walje, katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog hakukanusha wala kukubali tuhuma anazoelekezewa na badala yake alitaka kuonana na Tanzania PANORAMA Blog kwa mazungumzo na kwa upande wa Gulam alipoulizwa alisema mwenye majibu ya tuhuma hizo ni walje.

Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa amekwishaeleza msimamo wa ofisi yake kuwa masuala ya migogoro ya jumuiya za kidini hawezi kuyazungumzia kwenye vyombo vya habari.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya