RIPOTA PANORAMA
PADRE Evodius Msigwa wa Jimbo Katoliki la Bunda lililopo Mkoa wa Mara anadaiwa kumpiga risasi mbili kwenye paja mtoto mwenye umri wa miaka tisa aliyemtuhumu kumwimbia Sungura.
Taarifa zilizopatikana kutoka kwa ndugu wa karibu wa kijana huyo aliyetajwa kwa jina moja la Adam zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea mwaka 2021 katika Kijiji cha Manyamanyama, Wilaya ya Bunda mkoani Mara lakini limekuwa likifichwa na kwamba ingawa liliripotiwa polisi; Polisi walifunika kombe.
Inadaiwa, siku ya tukio Padre Msigwa alikuwa akikata miti katika eneo lililo karibu na Banda lake la Sungura ndipo alipomuona mtoto Adam aliyekuwa amebeba mkaa akielekea nyumbani kwao akipita mbele ya banda lake la sungura akamwita na kuanza kumtuhumu kwa kumwimbia sungura wake.
“Lile banda la sungura wa Padre lipo karibu na njia ya kwenda kanisani, ni njiani, watu wote huwa tunapita pale. Tulipomuhoji mtoto alisema kuwa baada ya kufika usawa wa lile banda, yule Padre alikuwa anakata miti, alikuwa na panga mkononi, akaanza kumwita we kijana njoo.
“Alipoenda akaanza kumuhoji ni kwanini huwa anamuibia sungura wake, kijana akasema yeye siyo mwizi bali mpita njia na anatoka kununua mkaa aliotumwa na wazazi wake anaupeleka nyumbani. Akamkamata mkono akamuongoza kwenye banda la sungura.
“Adam baada ya kuona kuna hatari mbele yake akaanza purukushani za kujinasua kwenye mikono ya Padre ili akimbie lakini hakuweza, Padre akamwamuru alale chini kifudifundi, mtoto akalala, akiwa amelala pale chini akachomoa bastola akampiga risasi mbili mguuni kwenye paja,” amedai mmoja wa ndugu wa mtoto huyo.
Taarifa nyingine kutoka kwa watu wa karibu na familia ya mtoto Adamu zimedai kuwa Padre Msigwa baada ya kumpiga risasi Adam alieleza kuwa alimkuta akiiba sungura wake, akamtaka ajisalimishe au akimbie kutoka kwenye banda lake kwa kufyatua risasi juu lakini Adamu hakukimbia bali alisimama hapo hapo bandani.
“Padre anasema alimkamata mtoto akiwa anaiba, alimkamata na sungura wake, akawa amefyatua risasi ya kwanza juu ili mtoto ajisalimishe au akimbie. Mtoto hakukimbia wala nini, Padre Msigwa akaona inaweza kuleta shida zaidi labda mtoto ana silaha ndipo akaamua kumpiga risasi ya mguu ili amkamate, akafanikiwa kumkamata.
“Padre Msigwa aliamua kulimaliza jambo hilo kwa kuelewana na wazazi wake Adam kwa kugharamia matibabu baada ya Askari Polisi waliofika eneo la tukio kuwabembeleza wazazi hao wakubali kupokea fedha za matibabu jambo ambalo waliliafiki kwa kupokea fedha za matibabu na fidia nyingine.
“Lakini kauli hiyo ya Padre Msigwa ilikanushwa vikali na wazazi wa Adamu, wao walieleza kuwa baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi, alipelekwa hospitali akiwa chini ya ulinzi wa Polisi kwa ajili ya matatibu na alilazwa akiwa chini ya ulinzi wa Polisi.
“Polisi walimlinda Adamu kwa zamu, usiku na mchana kwa muda wa siku mbili akiwa anapatiwa matibabu kabla hawajatoweka na kumuacha akiendelea na matibabu kwa gharama na uangalizi wa wazazi wake, hivyo hata alipotoka polisi hawakujui ingawa wao ndiyo walimpeleka pale hospitali na wakawa wanamlinda kwa zile siku mbili.
“Adamu alipotoka hospitali nadhani hakuwa amepona vizuri kwa sababu mguu uliendelea kumsumbua akashindwa kuendelea na masoma, alikuwa anasoma darasa la pili huo mwaka 2021. Wazazi wake walishindwa kuchukua hatua dhidi ya Padre Msigwa kwa sababu ya kutishiwa maisha, hivi sasa Adamu yupo anatibiwa kwa mganga wa kienyeji,” ameeleza mtoa taarifa huyo.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Padre Msigwa kwa simu yake ya kiganjani na kumuuliza kuhusu kuhusika na tukio la kumpiga risasi Adamu lakini amekataa kutoa ushirikiano;
Mahojiano ya Padre Msigwa na Tanzania PANORAMA Blog yalikuwa hivi;
PANORAMA, Padre habari za leo.
PADRE MSIGWA- Nzuri.
PANORAMA – Naongea na Padre Msigwa.
PADRE MSIGWA – Ndiyo.
PANORAMA – Nafurahi kukupa Padre, mimi naitwa (mwandishi wa Tanzania PANORAMA anajitambulisha jina), ni mwandishi wa habari, naomba nisaidie jambo moja, naomba kusukia kutoka kwako, hivi tukio la wewe kumpiga risasi kijana mwenye umri wa miaka tisa lilitokeatokeaje Padre.
PADRE MSIGWA – Wewe ni mwandishi wa wapi?
PANORAMA – Mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog.
PADRE MSIGWA – Sasa kwenye simu siwezi kuongea.
PANORAMA – Kwanini?
PADRE MSIGWA – Njoo hapa ofisini kwangu.
PANORAMA – Ofisi zako zipo wapi.
PADRE MSIGWA – Jimbo Katoliki la Bunda.
PANORAMA – Mimi niko Dar es Salaam ndiyo maana. nimekupigia simu na kujitambulisha kwako.
PADRE MSIGWA – Wewe, nimesema hatuwezi kuongea kwenye simu, tuma mtu basi.
Akakata simu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) wa Mara, Longinus Tibashubwamu alipoulizwa alisema ndiyo kwanza analisikia tukio hilo na kuahidi kufuatilia kabla ya kutoa taarifa.