RIPOTA PANORAMA
SERIKALI imesema migogoro inayohusu taasisi za dini inaishughulikia kwa usiri kwa kutoianika kwenye vyombo vya habari kwa sababu ya kulinda hadhi na heshima ya taasisi hizo.
Hayo yameelezwa leo na Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Emamnuel Kihampa katika mahojiano yake na Tanzania PANORAMA Blog yaliyofanyika kwa njia ya simu kuhusu mgogoro unaoendelea kufukuta katika Taasisi ya KSIJ Tanga Jamaat unaodaiwa kuwa na viashiria vya uvunjifu wa amani.
Aidha, mgogoro huo unadaiwa kuhusisha matumizi mabaya ya fedha za taasisi hiyo, uongozi wa kiimla na kutishiana kuangamizana na kwamba Serikali kupitia Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ilimwita mwenyekiti wa taasisi hiyo, Hussein Walje anayedaiwa kuwa kiini cha mgogoro; lakini Walje aliigomea Serikali kwa kutoitikia wito huo.
Katika majibu yake, Kihampa amesema Serikali ina utaratibu wake wa kushughulikia migogoro wa kidini hivyo hawezi kuthibitisha au kukataa, kutoa maelezo au ufafanuzi kuhusu kuwepo kwa mgogoro huo.
“Sasa kwa sababu unanieleza kuwa ni mgogoro unaohusu taasisi ya dini na sisi Serikali huwa tuna utaratibu maalumu wa kushughulikia migogoro ya dini, huwa hatuianiki kwenye vyombo vya habari.
“Kwa hiyo utaniwia radhi nikishindwa kuthibitisha au kukataa usemi wako, wala kutoa maelezo au ufafanuzi kuhusiana na hilo na kama kweli kuna mgogoro ndani ya taasisi hiyo au lah na hatua gani ambazo sisi Serikali tumezichukua. Maana itakuwa ni kama kuianika taasisi ya dini,” amesema Kihampa.
Akizungumza kuhusu wito wa Serikali kupuuzwa na anayedaiwa kuwa ndiye kiini cha mgogoro huo, amesema taarifa hizo ndiyo anazisikia na alishukuru kwa kupata taarifa hiyo huku akiahidi kuifuatilia.
Aidha, Kihampa amekataa kuzungumza lolote kuhusu ofisi yake kuhusika na mgogoro wa taasisi hiyo kwa kueleza kuwa masuala yanayohusu migogoro ya kidini ikiwa ni pamoja na mgogoro ndani ya taasisi hiyo ni nyeti na hushughulikiwa kwa unyeti wake.
“Kama nilivyosema siwezi kuzungumzia hilo maana sisi hatufanyi kazi kwa utaratibu huo na tunafanya hivyo kwa nia njema kabisa,” amesema Kihampa.
Alipoulizwa iwapo ofisi yake itakuwa tayari kutoa kauli au itaendelea na msimamo wake wa kutotoa kauli iwapo utatokea uvunjifu wa amani kama inavyodaiwa kuwepo kwa viashiria hivyo, amesema iwapo kuna taarifa hizo ziwasilishwe kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) kwa sababu ndiye mamlaka husika.
Amesema ipo migogoro mingi ya kidini ambayo inashughulikiwa na Seriikali lakini wananchi hawajui na hawapaswi kuifahamu na iwapo wanapaswa kuifahamu, vyombo au taasisi husika ndivyo vyenye jukumu la kutoa taarifa.
“Kuna migogoro mingi ya kidini ambayo inashughulikiwa na Serikali lakini wananchi hawafahamu na wala hawapaswi kufahamu na kama watapaswa kufahamu basi vyombo au taasisi husika ndiyo zinatakiwa zitoe taarifa yao.
“Sisi kama Serikali lengo letu ni kulinda hadhi na heshima ya taasisi za dini kwa hiyo hata kukitokea mgogoro, lengo letu ni kusuluhisha hiyo migogoro bila kuleta taharuki katika jamii, huo ndiyo wajibu wetu,” amesema Kihampa.
Zaidi ya wanajumuiya 40 wa KSIJ Tanga Jamaat wanamtuhumu mwenyekiti wao, Hussein Walji kuiongoza Jamaat hiyo kiimla, kufuja mali za Jamaat na kudhulumu fedha za misaada za wajane na walemavu na sambamba naye, wanamtuhumu pia mmoja wa wafanyabiasha mwenye ukwasi mkubwa wanayemtaja kuwa mshirika wa karibu wa Walji kwa kuwatisha kuwa atawapoteza duniani na kwamba anatumia uwezo wake wa kifedha kuwabambikia kesi polisi.
Walji alipofanya mahojiano na Tanzania PANORAMA Blog hakukanusha wala kukubali tuhuma anazoelekezewa na badala yake alisema mambo hayo anaweza kuyazungumzia iwapo Tanzania PANORAMA Blog itafika ofisini kwake na kukutana naye ana kwa ana.