Friday, April 25, 2025
spot_img

NHC YAHESABU FAIDA YA BIL. 92.9, MAPATO JUMLA BIL. 257

CHARLES MULLINDA

SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), limevuna faida kabla ya kodi ya Shilingi bilioni 92.9 mwaka 2022 na limeingiza mapato ya jumla ya Shilingi bilioni 257.47 katika kipindi hicho.

Hayo yameelezwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alipokuwa akitoa taarifa ya shirika lake kwa waandishi wa habari kuhusu ufanisi lililoupata kwa mwaka 2022 na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli kwa mwaka 2023 kwenye mkutano uliofanyika Makao Makuu ya NHC yaliyopo Jengo la Kambarage, jijini Dar es Salaam.

Mchechu ambaye anakuwa Mkurugenzi wa kwanza wa Shirika la Umma hapa nchini kusimama mbele ya waandishi wa habari kutoa ripoti ya aina hiyo kwa umma, amesema utaratibu huo aliouanzisha utakuwa wa kudumu ambapo kila mwaka NHC itakuwa inatoa ripoti ya ufanisi na mwelekeo wa utekelezaji wa shughuli za shirika kwa mwaka unaofuata; lengo likiwa kutimiza maadili ya msingi ya shirika hilo.

Katika mkutano huo ambao Mchechu alijikita zaidi kwenye kutoa takwimu za mafanikio yaliyofikiwa na NHC, alisema mapato ya jumla yamepanda kutoka Shilingi bilioni 144.42 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi bilioni 257.47na mapato ya kodi sasa yamefikia Shilingi bilioni 90.76 kutoka Shilingi bilioni 89.23 kwa mwaka 2020/21.

Amesema mapato ya mauzo ya nyumba yamepanda kutoka Shilingi bilioni 29.33 kwa mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/2022 na kwa upande wa mapato yatokanayo na shughuli za ukandarasi nayo yamepanda kutoka Shilingi bilioni 43.98 kwa mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi bilioni 52.60 mwaka 2021/22.

Akifafanua zaidi kuhusu faida, amesema; “Hata hivyo, faida halisi inayotokana na shughuli za shirika iliongozeka hadi kufikia Shilingi bilioni 60.7 mwaka 2021/22 kutoka Shilingi bilioni 31.7 mwaka 2020/21.

“Ongezeko hili lilienda sambamba na ongezeko la majengo. Hali ya soko la nyumba imeanza kuimarika, Ni matarajio ya shirika kuwa mwaka wa fedha 2022/2023 litaendelea kupata faida kubwa,” amesema Mchechu.

Akizungumzia mizania ya shirika hilo analoliongoza, Mchehu amesema imeendelea kuimarika na thamani ya mali za shirika alizoziita kwa jina la kimombo total assets kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hadi Juni 31, 2022 zilikuwa ni Shilingi trilioni 5.04.

“Mizania hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka kwa wastani wa asilimia 12 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2019. Thamani hii inahusisha vitega uchumi vya majengo na ardhi ghafi inayomilikiwa na shirika ambayo bado haijaendelezwa ikiwa ni pamoja na miradi ya nyumba inayoendelea,” amesema Mchechu.

Aidha Mchechu amesema mtaji wa NHC hadi kufikia Juni 2022 umefikia Shilingi trilioni 3.4 kutoka Shilingi trilioni 2.9 mwaka 2019.

Kuhusu mwelekeo wa shirika kwa mwaka 2023, Mchechu amesema ili kuongeza mapato ya shirika na kuwahudumia Watanzania, NHC itaendelea kukamilisha miradi iliyokuwa imesimama, kutekeleza mradi wa Samia Housing Scheme (SHS), kuanza ujenzi wa Shopping Mall jijini Dodoma na kuendelea kukusanya madeni ya kodi ya nyumba yanayofikia Shilingi bilioni 21.

Mchechu amezitaja shughuli nyingine zitakazotekelezwa na NHC kwa mwaka 2023 kuwa ni kuendelea kutekeleza miradi ya ubia kwa kushirikiana na sekta binafsi, kuendelea kusimamia miliki ya nyumba 18,622 za shirika na kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi ya NHC.

Shughuli nyingine ambazo Mchechu amezitaja ni kuendelea kujenga uhusiano wenye tija na wabia na taasisi, kusimamia nidhamu ya utendaji kazi ndani ya shirika na kuendelea kushirikiana na  vyombo vya habari.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya