RIPOTA PANORAMA
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari (TPA) imefanya mapinduzi makubwa katika maeneo sita muhimu ya uendeshaji wa shughuli zake yaliyotajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwa yanapaswa kuboreshwa.
Maeneo hayo ni upanuzi wa wigo wa soko la shehena za mizigo inayokwenda nchi jirani zinazopakana na Bahari, kushiriki kwenye maonyesho ya biashara katika masoko ya usafiri na kupanga na kufanya ukaguzi wa njia kila nusu mwaka kwa ukanda wa kati na Dar es Salaam.
Maeneo mengine yaliyoguswa na mapinduzi hayo ni mpangomkakati wa kupanua wigo wa soko, utendaji wa ofisi na wakala wa kutangaza biashara katika nchi za Rwanda, Zambia na Burundi, mpango wa uendeshaji wa ofisi na wakala wa biashara wenye malengo ya kina wa kuanzishwa kwa ofisi na wakala hizo pamoja na kufuatilia na kufanya tathmini ili kubaini kama malengo ya TPA yanafikiwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mkeli Mbossa aliyoitoa jana kwa Tanzania PANORAMA Blog kuhusu maeneo hayo muhimu yaliyotajwa na CAG kwenye ripoti yake ya 2020/2021 kisha kufanyiwa mapinduzi, kulingana na malengo yaliyowekwa mwaka wa fedha 2022/2023, utendaji jumla wa Bandari za TPA kwa miezi sita ya kwanza ambayo ni Julai hadi Disemba 2022 umevuka lengo kwa asilimia 12 kutoka tani milioni 10.8 zilizopangwa kupokelewa hadi tani 12.1 milioni zilizopokelewa.
Mbossa ameieleza Tanzania PANORAMA Blog kuwa malengo mengine katika kipindi cha Julai hadi Disemba, 2022 nayo yameongezeka huku akitaja takwimu kuwa katika kipindi hicho, malengo ya TPA yalikuwa kupokea shehena zenye uzito wa tani milioni 10,807,218 lakini shehena iliyopokelewa ilikuwa na uzito wa tani milioni 12,136,319.
Amesema kwa upande wa makasha, malengo yalikuwa kupokea makasha 407,700 lakini hadi Disemba 2022 makasha yalipokelewa yalikuwa 454,659 na idadi ya meli zilizotarajiwa kutia nanga katika Bandari za Tanzania zilikuwa 2,214 lakini hadi Disemba mwaka jana meli zilizotia nanga ni 2,828.

Kuhusu uzito wa meli zilizohudumiwa kwenye Bandari za Tanzania, alisema malengo yalikuwa kuhudumia meli zenye uzito unaofikia 16,328,568 lakini hadi mwishoni mwa mwaka 2022 uzito wa meli zilizohuduniwa ulikuwa 18,742,765 huku mapato yaliyotarajiwa kupatikana yalikuwa Shilingi bilioni 612,203 lakini kiasi halisi cha mapato yaliyopatikana hadi Disemba 2022 kilikuwa Shilingi bilioni 660,827.
Mbossa amefafanua katika taarifa yake hiyo kuwa utendaji wa Bandari za Tanzania dhidi ya bandari shindani katika soko la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika hupimwa kwa viashiria vya malengo yanayopangwa mwaka hadi mwaka.
Kwamba malengo hayo huwekwa kwa vigezo vya kisayansi na hufuata jinsi soko lilivyo na matarajio ya mwaka husika yanayoongozwa na ukuaji wa uchumi wa nchi husika, idadi ya watu, ukuaji wa biashara na mwenendo wa biashara ya usafirishaji majini na nchi kavu.
“Aidha, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019/20 hadi 2021/22) shehena ya nchi jirani iliyopita kwenye Bandari ya Dar es Salaam imendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka; kutoka tani milioni 5.57 mwaka 2019/20 hadi tani milioni 7.80 zilizohudumiwa mwaka 2021/22.
“Mwaka 2019/20 Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani 1,393,893, mwaka 2020/21 tani 1,141,445 na mwaka 2021/22 tani 2,036,748 ya shehena za nchi ya Zambia na kwa nchi ya D. R Congo, shehena yake iliyohudumiwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam kwa mwaka 2019/20 ni tani 1,890,732, mwaka 2020/21 tani 1,986,503 na mwaka 2021/2022 ni tani 2,956,368.
“Shehena ya Burundi iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam kwa mwaka 2019/20 ni tani 477,788, mwaka 2020/21 tani 504,274 na mwaka 2021/22 ni tani 493,078. Rwanda kwa mwaka 2019/20 shehena iliyohudumiwa ni tani 1,252,338, mwaka 2020/21 ni tani 1,293,534 na kwa mwaka 2021/22 ni tani 1,487,277 huku Malawi shehena yake iliyohudumiwa kwa mwaka 2019/20 ni tani 376,054, mwaka 2020/21 tani 407,849 na mwaka 2021/22 ni tani 470,475.
“Uganda shehena yale ilikuwa tani 140,269 kwa mwaka 2019/20, tani 191,282 kwa mwaka 2020/21 na tani 209,975 kwa mwaka 2021/22 na kwa nchi za Msumbuji, Sudan, Kenya, Comoro, Angola na Zibwabwe shehena za nchi hizo zilizohudumiwa kwa mwaka 2019/20 ni tani 35,169, mwaka 2020/21 tani 54,703 na mwaka 2021/22 ni tani 147,574,” imesomeka taarifa hiyo.

Kuhusu kushiriki kwenye maonyesho ya biashara katika masoko ya usafiri, Mbossa ameeleza kuwa TPA imeshiriki na kufanya maonyesho ya shughuli za Bandari kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi ambapo Julai hadi Agosti, 2022 ilishiriki maonyesho yaliyofanyika nchini Malawi, Mwezi Septemba, 2022 ilishiriki maonyesho yaliyofanyika nchini Zambia na Septemba hadi Oktoba ilishiriki mashindano yaliyofanyika nchini Burundi.
“TPA pia iliratibu ziara ya wafanyabiashara kutoka Zimtrade ya Zimbabwe na ziara nyingine za wafanyabishara kutoka D. R Congo, Zambia na Rwanda. Ziara hizo zilifanyika kati ya mwezi Oktoba na Novemba, 2022 na aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TPA alishiriki kwenye shughuli za maonyesho ya Migodi ya Madini nchini D. R Congo kwa mwaliko wa Waziri wa D. R Congo mwenye dhamana ya Madini.
“Madini na mahitaji ya migodi D. R Congo ni sehemu kubwa ya shehena inayopita katika Bandari za ukanda wa Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika,” amesema.
Mbossa amezungumzia pia kupanga na kufanya ukaguzi wa njia kila nusu mwaka kwa kueleza kuwa TPA inafanya kaguzi za njia kwa mfumo wa shoroba za usafirishaji unaofahamika kwa kimombo; transport corridors unaohusisha kuchunguza aina ya kiwango cha shehena inayosafirishwa, njia za usafirishaji, changamoto na ushindani uliopo katika Bandari za Tanzania na nchi jirani ili kubuni mikakati ya kuzifanya Bandari za Tanzania kuwa shindani kieneo.
Aidha, Mbossa ameeleza kuwa ukaguzi hufanyika kila robo mwaka kwa kuandaa madodoso maalumu ya kibiashara na mara nyingi huhusisha wadau wote wa Sekta ya Uchukuzi kwenye shoroba husika na kwamba hivi sasa TPA inaendelea na ukaguzi wa shoroba za Dar es Salaam, Kati, Kaskazini na Mtwara ambao utakamilika Machi 2023.
Amesema taarifa za ukaguzi huo hutumiwa na ngazi za maamuzi kutekeleza mikakati ya kushika soko kubwa.
Jambo jingine alilozungumzia Mbossa kwenye taarifa yake hiyo ni ofisi na wakala wa kutangaza biashara katika nchi za Rwanda, Zambia na Burundi kutekeleza shughuli zilizokusudiwa ambapo amesema utendaji wa ofisi za kimasoko kama zilivyo idara nyingine za TPA huongozwa na taratibu za utendaji kazi.

Amesema taratibu za utendaji kazi kimasoko nje ya nchi tayari zimekwishatengenezwa tangu Novemba mwaka jana na hivi sasa zipo kwenye hatua za mapitio kabla ya kuidhinishwa kutumiwa na mamlaka husika ili ziweze kuhuisha mfumo wa taratibu za utendaji kazi katika ofisi hizo kabla ya mwisho wa mwaka 2023.
Mbossa amesema taratibu za utendaji kazi zilizotengenezwa zinaonyesha muundo wa kazi za kila ofisi ya kimasoko nje ya nchi na jinsi ya kutekeleza wajibu wake haraka ndani ya muundo wa kitaasisi katika utoaji huduma kwa wateja.
Taarifa ya Mbossa imezidi kueleza kuwa mpango wa uendeshaji wa ofisi za kimasoko umeainishwa kwenye mpangomkakati wa nne wa TPA na kwamba utafiti wa kimasoko ni sehemu ya utekelezaji wa mpangomkakati ambao ni endelevu.
“Hata hivyo, kazi nyingi za mpango huo ni za kiintelejensia zinazohusisha pamoja na mambo mengine, mbinu za kimasoko ambazo hazipaswi kujulikana au kuigwa na washindani wa Bandari za Tanzania. Kazi hizi hufanywa kila robo mwaka kulingana na mpango kazi wa mwaka husika. Kwa mfano, kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 kazi hizi zimepangwa kufanyika kati ya Machi na Aprili, 2023,” ameeleza Mbossa katika taarifa yake hiyo kwa Tanzania PANORAMA Blog.
Mbossa ameelezea pia ufuatiliaji wa tathmini ili kuhakikisha malengo ya TPA yanafikiwa ambapo amesisitiza kuwa kazi hiyo hufanywa kupitia mpango kazi uliopangwa kwenye mpango na bajeti wa kila mwaka husika.