Thursday, July 17, 2025
spot_img

SERUKAMBA AZINDUA UPANDAJI MITI MIL 1.5 IKUNGI

RIPOTA MAALUMU

Ikungi, Singida

MKUU wa Mkoa (RC) wa Singida, Peter Serukamba amezindua kampeni ya upandaji miti millioni moja na nusu pamoja na utunzaji mazingira katika Wilaya ya Ikungi iliyopo Mkoa wa Singida.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ukungi kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa uzinduzi huo ulifanyika jana katika Kijiji cha Utaho kilichopo eneo la mpakani mwa Wilaya ya Ikungi na Singida Mjini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, RC Serukamba aliambatana na Sekretariat ya Mkoa wa Singida iliyoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Mwalimu Dorothy Mwaluko pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, RC Serukamba aliwataka wakazi wa maeneo hayo kupanda miti kama sehemu ya utamaduni wa kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

RC Serukamba alizielekeza halmashauri zote za Mkoa wa Singida kutunga sheria ndogo zitakazowabana watu wenye nia ovu na mazingira ili wananchi wote washiriki kikamilifu utunzaji wa mazingira; aidha aliwaagiza wakuu wa wilaya kusimamia kazi hiyo.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ikungi, Jerry Muro akipanda mti wakati wa uzinduzi wa upandaji miti milioni moja na nusu katika Wilaya ya Ikungi jana.

Agizo jingine alilotoa RC Serukamba ni marufuku ya uchomaji mkaa hovyo na aliinyooshea kidole Kata ya Isuna kuwa na wachomaji mkaa kiholela wengi aliotaka wathibitiwe na viongozi wa eneo hilo.

Awali akimkaribisha RC Serukamba, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ikungi, Jerry Muro alisema eneo lake la utawala analolisimamia limetekeleza kikamilifu agizo la Serikali Kuu la kupanda miti na kutunza mazingira.

DC Muro alisema tayari miti 50,000 imekwishapandwa katika maeneo mbalimbali ya umma, binafsi na pembezoni mwa barabara kuu za Singida kwenda Dodoma na ile ya Singida kwenda Manyara kupitia Babati.

Alisema kazi ya utekeleza wa maagizo ya Serikali Kuu ya kupanda miti ya kutunza mazingira ni endelevu kwa mwaka mzima na kwamba viongozi wa vitongoji, vijiji, kata na wilaya wanapaswa kujiwekea utaratibu maalumu wa kuratibu kazi ya upandaji na ukuzaji miti.

Naye Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu aliwapongeza viongozi wa wilaya na halmashauri kwa kuanza utekelezaji wa maazimio ya Bunge ya upandaji miti na utunzaji mazingira na kusisitiza kuwa Wilaya ya Ikungi lazima iwe mstari wa mbele kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kupanda na kulinda miti.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ali Juma Mwanga alisema maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Serukamba kwa halmashauri kutunga sheria ndogo za usimamizi wa mazingira yatazingatiwa kwa uzito unaostahili.

MATUKIO KATIKA PICHA UZINDUZI WA UPANDAJI MITI MILIONI MOJA NA NUSU WILAYANI IKUNGI

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya