Friday, April 25, 2025
spot_img

POLISI ‘WAMWITA’ MWANAMKE ALIYESHAMBULIWA NA KUJERUHIWA KWA RISASI

RIPOTA PANORAMA

JESHI la Polisi limesema Ashura Samweli, Mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam anayedai kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi na mzazi mwenzie aende kwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kufikisha malalamiko yake.

Hayo yamesemwa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) David Misime alipokuwa akitoa kauli ya jeshi hilo kuhusu jina la Kamishna wa Polisi aliyetajwa kwa jina moja la Msangi kuhusika kwenye sakata hilo.

Ashura anadai Septemba mwaka jana akiwa nyumbani kwake, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mkononi na mzazi mwenzie anayemtaja kwa jina la Riziki Mahambi ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Emirates Shipping Line Agency lakini hakuripoti mara moja tukio hilo polisi baada ya kushawishiwa na mzazi mwenzie huyo.

Katika mahojiano aliyoyafanya na Tanzania PANORAMA Blog, Ashura alieleza kuwa baadaye alifikisha malalamiko yake kwa Kamishna Msangi ambaye alimwita Mahambi ofisini kwake Dar es Salaam na kumuhoji naye akakiri kutenda tukio hilo kisha Kamishna Msangi akamtaka Ashura aondoke ili yeye abaki na Mahambi akimshughulikia.

Pamoja na mambo mengine, Ashura alisema baadaye alipata taarifa kuwa Mahambi anaendelea na shughuli zake kama kawaida na alipowasiliana na Kamishna Msangi alimbadilikia kwa kumweleza aachane na suala hilo kwa sababu linaweza kumgeukia yeye kwani alikuwa akitembea na mume wa mtu.

Jeraha alilopata Ashura Samweli baada ya kushambuliwa kwa risasi na mzazi mwenzie Riziki Mahambi

Kamishna Msangi ambaye jana alitafutwa na Tanzania PANORAMA Blog kwa simu na kukanusha kuwafahamu Ashura na Mahambi, lakini alipobanwa aliitaka Tanzania PANORAMA Blog kwenda ofisini kwake kwa ajili ya kulizungumzia suala hilo, uchunguzi mdogo kwenye usajili wa namba yake ya simu ya mkononi umeonyesha kuwa imesajiliwa kwa jina la Hassan Msangi na taarifa zaidi zimeonyesha ana cheo cha Kamishna Msaidizi na si Kamishna kama ambavyo imekuwa ikielezwa.

SACP Misime, ameiambia Tanzania PANORAMA Blog kuwa kinachoelezwa na Ashura kinaonyesha kilichotendeka ni uhalifu na kwamba jambo baya linaloonekana kwenye maelezo ya Ashura ni jinsi tukio lilivyotokea; inaonyesha nia ya kutaka kuficha uhalifu.

“Kinachozungumziwa ni uhalifu unaoonyesha ulitokea mwaka jana jijini Dar es Salaam. Jambo baya ambalo linaonekana kwa jinsi tukio hilo lilivyotokea, inaonyesha dhahiri ni kutaka kuficha uhalifu na mhalifu aliyetenda uhalifu huo kuanzia siku aliyotenda kosa hilo na mengine yakaendelea kama alivyoeleza mtendewa.

“Jeshi la Polisi lingependa kumwelekeza afike kwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu Dar es Salaam atasikilizwa na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zitachukuliwa,” amesema SACP Misime.

Ashura Samweli

Kauli hiyo ya SAPC Misime ilikuwa ikijibu maswali ya Tanzania PANORAMA Blog ambayo ilimuuliza hivi; Ashura Samweli, anamtuhumu Kamishna Msaidizi Hassan Msangi kuwa alimfikishia malalamiko yake ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi na mzazi mwenzie na Kamishna Msaidizi huyo akaahidi kumsaidia ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kisheria lakini baada ya kukutana na anayetuhumiwa alimgeuka kwa maelezo kuwa hata yeye mlalamikaji ana makosa hivyo suala hilo la kushambuliwa kwa risasi aliache. Naomba kujua;

Mosi; Kamishna Msaidizi wa Polisi ana mamlaka ya kusikiliza malalamiko ya watu kushambuliana kwa risasi ya kuyatolea maamuzi?

Pili; Kwa mujibu wa taratibu za Jeshi la Polisi, Kamishna Msaidizi huyo alipaswa kuchukua au kufanya nini baada ya kufikishiwa malalamiko au madai hayo?

Tatu; Iwapo kuna taratibu za kiutendaji katika Jeshi la Polisi ambazo Kamishna Msaidizi huyo hakuzizingatia, kuzifuata au alizikiuka; sheria, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi zinaelekeza nini?

USIKOSE KUFUATILIA MKASA HUU HAPA TANZANIA PANORAMA BLOG KESHO.

Nyingine Zinazohusiana na Hii

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Tufuatilie

0FansLike
3,913FollowersFollow
0SubscribersSubscribe
- Advertisement -spot_img

Habari Nyingine Mpya