RIPOTA PANORAMA
MUFTI na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dk. Abubakar Zubeir bin Ally ameunda tume ya maboresho ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), yenye wajumbe saba.
Taarifa kwa umma iliyotolewa jana na BAKWATA na kusaini na Mufti na Sheikh Mkuu Dk. Ally imeeleza kuwa tume hiyo ameiunda kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Baraza Kuu la BAKWATA, kipengele 84:17.
Taarifa inawataja wajumbe walioteuliwa kuwa ni Sheikh Issa Issa ambaye ni mwenyekiti na katibu wa tume ni Alhaji Omar Ege. Wajumbe wengine ni Alhaji Nuhu Mruma, Daudi Nasibu, Iddi Kamazima, Mohamed Nyengi na Qussim Jeizan.
Wajumbe wa tume watafanya kazi kwa kufuata hadidu saba ambazo zinatajwa kwenye taarifa hiyo kuwa ni kuhakiki madeni ya BAKWATA na kushauri namna ya kuyalipa, kufanya uchunguzi wa mali za BAKWATA ambazo zinamilikiwa na watu wengine kinyume cha taratibu na kuchukua hatua za kutatua na kufanya tathimini ya changamoto za mifumo ya utawala inayoikabili BAKWATA na kushauri namna bora ya kufanya maboresho.
Nyingine ni uchunguzi wa mikoa au wilaya yenye migogoro mikubwa ya uongozi au mali na kuchukua hatua kuitatua, kuibua na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa BAKWATA na masuala mengine muhimu ambayo tume itaona yanafaa kufanyiwa kazi.