RIPOTA PANORAMA
ASHURA Samweli, mkazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambaye alipigwa risasi mkononi na mzazi mwenzie akiwa mjamzito, amemtaja mmoja wa vigogo wa Jeshi la Polisi kuhusika katika sakata hilo.
Akizungumza jana na mwandishi wa Tanzania PANORAMA Blog nyumbani kwake Mbezi Beach, Ashura alisema Septemba mwaka jana, akiwa nyumbani kwake alishambuliwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzie aliyemtaja kwa jina la Riziki Mahambi lakini hakuripoti tukio hilo polisi mara moja kutokana na ushawishi alioupata kutoka kwa mzazi mwenzie huyo.
Alisema baada kupigwa risasi mzazi mwenzie alimshawishi asilifikishe suala hilo polisi lakini baadaye alilifikishwa kwa afisa wa juu wa polisi mwenye cheo cha Kamishna anayemtaja kwa jina moja la Msangi akiamini kuwa anaweza kumsaidia kutokana na wadhfa wake, lakini polisi huyo baada ya kukutana na mzazi mwenzie alimgeuka.
“Nilikwenda kwa Kamishna Msangi akanihoji kuhusu tukio zima nami nikamuelezea kisha aliniahidi kunisaidia, alisema atatuma watu wakamkamate Riziki na kufanya taratibu nyingine za kisheria. Lakini baada ya siku kadhaa nilisikia Riziki alikamatwa na kupelekwa kwa Kamishna Msangi, sijui walizungumza nini.
“Sasa hivi nikimpigia simu hayuko kama alivyokuwa mwanzo mara aniambie eti hata mimi nina makosa naweza kushtakiwa kwa kuwa nilikuwa na mahusiano na mume wa mtu, yaani sielewi hata anachonieleza ni kitu gani, kupigwa risasi na kutembea na mume wa mtu vina uhusiano gani?”
Akizungumzia tukio la kupigwa kwake risasi lilivyotokea alisema mzazi mwenzie, Mahambi ni Mfanyakazi wa Kampuni ya Emirates Shipping Line Agency na kwamba walifahamiana na kuanza uhusiano wakiwa katika harakati za kazi.
“Tulijuana kwenye mambo yetu ya kazi na ndipo Riziki akaanza kunifuatilia nami nikajikuta nimenasa katika mtego wake, wakati huo nilikuwa na mtu wangu lakini kwa kuwa Riziki alionesha kunipenda sana na kunishawishi kwa vitu vingi nilijikuta nikikubali kuwa mpenzi wake.
“Nikaachana na mtu wangu na kujiweka rasmi kwa Riziki, mapenzi yetu yalianza kwa amani na furaha sana mpaka tukafanikiwa kupata mtoto wa kwanza, hakukuwa na shida yoyote kati yetu kila mmoja alionesha mapenzi ya dhati kwa mwenzie.
“Tulipanga mipango mingi ya kimaendeleo na jinsi ya kuikuza familia yetu ndipo nikaruhusu kubeba ujauzito mwingine ambao hivi sasa una miezi sita lakini upepo ulianza kubadilika mwishoni mwa mwaka jana kwani katika hali isiyoeleweka Riziki alianza visirani na ugomvi wa mara kwa mara bila sababu za msingi.
“Mwezi wa tisa mwaka jana tukiwa tumekaa ndani ulitokea ugomvi usiokuwa na kichwa wala miguu, Riziki alikuja akionekana kuwa na jambo lake kichwani kwani alipofika tu aliniuliza mahali alipo mdogo wangu aitwae Magna, nikamwambia Magna hayupo amesafiri, papo hapo akachukua simu akampigia Magna akamuuliza yuko wapi, sijui Magna alimjibu kitu gani lakini ghafla alinigeukia na kusema unaona dada yako anavyoendelea kunidanganya?
“Baada ya kusema maneno hayo akakata ile simu aliyokuwa akiongea na Magna kisha akatoa bastola akaniambia usiponiambia ukweli nakupigia risasi nakuua, mimi nikajua utani, nikamwambia nipige, nikashangaa kweli amenifyatukia risasi mkononi na mkono ulikuwa jirani kabisa na tumbo, yaani kama ingepotea njia kidogo tu ingenitoa utumbo.”

Alisema baada ya Riziki kumpiga risasi alianza kujigamba kuwa ana pesa nyingi hawezi kukamatwa wala kufungwa na mtu yeyote hapa nchini lakini muda mfupi baadaye alitulia na kuonekana ameingiwa na hofu.
Ashura alisema alianza kubembelezwa na Riziki asiende kuripoti tukio hilo polisi huku akimkumbusha kuwa wao ni wazazi na kama atakwenda kuripoti polisi na ikatokea akafungwa watoto wao watateseka.
“Kama mzazi aliponieleza maneno hayo na ukizingatia ukweli kwamba nimezaa naye na nina ujauzito mwingine wa miezi sita nikaingiwa na huruma na kukubalina na alichonieleza, akanichukua na kunipeleka kwenye hospitali moja iliyopo Mbezi Salasala akampatia pesa daktari tuliyemkuta ndipo nikatibiwa bila PF3,” alisema.
Hata hivyo, alisema huduma aliyoipata kwenye hospitali hiyo haikuwa nzuri kwani jeraha lake halikushonwa kitaalamu na baada ya siku mbili mkono ulianza kuvimba na kutoa harufu kali ukionyesha kuanza kuoza.
“Ikabidi nihame hospitali, nikaenda kutibiwa hospitali nyingine hadi jeraha likarudi katika hali yake ya kawaida, lakini mpaka sasa vidole viwili havifanyi kazi na kipindi wingu likiwa zito angani maumivu ya mkono huwa makali sana,” alisema.
Alipotafutwa Mahambi kwa kufikiwa ofisini kwake kuzungumzia tuhuma za mzazi mwenzie, aliwafungia mlango ndania ya ofisi yake waandishi wa Tanzania PANORAMA Blog kisha akaanza kuongea na simu kwa muda mrefu na aliporejea alisema yeye kwa wadhfa wake kwenye Kampuni ya Emirates Shipping Line Agency ana kazi nyingi hivyo suala hilo amemkabidhi Kamishana wa Polisi aloyemtaja kwa jina moja la Msangi kuwa ndiye msemaji wake na amekwishawasiliana naye ameelekeza waandishi hao wazuiwe hadi atakapofika kuwachukua, jambo ambalo waandishi wa PANORAMA waliliafiki na kuomba viti waketi ili wamsubiri Kamishna Msangi.
Mahambi baada ya kuona waandishi hao wanaomba viti waketi kumsubiri Kamisha Msangi alitoka nje tena akaanza kuongea na simu kwa takribani saa zima na aliporejea alisikika akisema ‘wapo wamekaa wanapiga story tu hata wasiwasi hawana, nadhani siyo waandishi ni nyoka hawa.’
Waandishi wa Tanzania PANORAMA Blog waliendelea kuketi ofisini kwa Mahambi zilizopo Ofisi za Emirates Shipping Line Agency, jengo la IT Plaza, ghorofa ya kumi wakimsuburi Kamishna Msangi ambaye hata hivyo hakutokea na baada ya hapo waandishi walisimama na kumshukuru Mahambi kwa ukaribisho wake, wakaondoka wakimuacha amesimama akiwaangalia.
Tanzania PANORAMA Blog imemtafuta Kamishna Msangi kwa simu yake ya kiganjani na kumuuliza kuhusu suala hilo lakini alikanusha kumfahamu Ashura na Mahambi na alipoambiwa iwapo atapewa uthibisho wa jina lake kutajwa kwenye sakata hilo alianza kufoka huku akihoji anayemuuliza anamuuliza kama nani.
Alipoambiwa anayemuuliza ni mwandishi wa habari anayetimiza wajibu wake wa kiuanahabari, Kamishna Msangi aliiomba Tanzania PANORAMA Blog kwenda ofisini kwake kuliongelea suala hilo badala ya kuongea kwenye simu.
USIKOSE KUSOMA TANZANIA PANORAMA BLOG KESHO KUJUA MWENDELEZO WA SAKATA HILI.