RIPOTA PANORAMA
MSARIFU wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation (BMF), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka taasisi hiyo kuendelea kuboresha mifumo yake ya afya ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
Taarifa iliyotolewa na juzi na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zanzibar, Charles Hilary ilieleza kuwa Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo Januari 18, mwaka huu alipokutana na uongozi na wafanyakazi wa BMF katika Ikulu ya Zanzibar ambako aliwapongeza kwa utendaji kazi wao kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Dk, Mwinyi aliutaka uongozi wa BMF kuangalia kwa upana jinsi ya kukamilisha miundombinu ya vifaa tiba pamoja na kuimarisha mifumo ya mawasiliano itakayotoa huduma bora kwa walengwa na pia kuboresha utendaji kwa kuongeza nguvukazi za ajira ili kutanua wigo kwenye tasnia hiyo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake na taasisi hiyo ili kuimarisha huduma bora za afya.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliutaka uongozi na wafanyakazi wa BMF kuanzisha Bima ya Afya kwa lengo la kwenda sambamba na mahitaji ya wananchi.
Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliwatunuku vyeti, tunzo na fedha taslimu wafanyakazi wa taasisi hiyo waliofanya vizuri kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMF, Balozi Tuvako Manongi alisema bodi imeendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi mbalimbali, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, wadau wa maendeleo wakiwemo wafadhili kutoka Sekta za Umma na binafsi pamoja na wachangiaji binafsi ili kupata rasilimali fedha.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BMF, Dk. Ellen Senkoro alisema taasisi hiyo inakusudia kutekeleza vipaumbele vyake vinne ikiwemo kuufanyia tathmini mpango mkakati wa taasisi hiyo uliopo ili kuongeza ubunifu na wigo wa kuanzisha miradi mipya baada ya mikongwe iliyopo kukamilika kwa asilimia 50.
BMF aliasisiwa na aliyekuwa Rais wa Awamu wa Tatu, Hayati Benjamin Mkapa na inabeba maono na sifa za viongozi bora wa Tanzania na Bara la Afrika.
MATUKIO KATIKA PICHA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI , DK HUSSEIN ALI MWINYI ALIPOKUTANA NA VIONGOZI NA WAFANYAKAZI WA TAASISI YA BENJAMIN MKAPA FOUNDATION