RIPOTA MAALUMU – Ikungi
VIONGOZI wa Serikali, watendaji na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Wilaya ya Ikungi wamefanya ziara ya pamoja katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kuhamasisha kilimo pamoja na wazazi kupeleka watoto wa shule.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mwenezi CCM wa Wilaya ya Ikungi, Nassoro Henku kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa viongozi hao, jana walifanya ziara katika Kata za Lighwa na Mang’onyi ambako walisikiliza na kutatua kero za viongozi wa halmashauri za vijiji vilivyo katika kata hizo na hayo yalienda sambamba na kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ikungi, Mika Tano Likapakapa ambaye alikuwa kwenye timu ya viongozi waliofanya ziara kwenye kata hizo, alivitumia vikao vyote vilivyofanyika kuwahimiza viongozi wa CCM na Serikali wa ngazi za kata na vijiji kushirikiana kutekeleza Ilani ya CCM, kuondoa mitafaruku baina yao na kufanya kazi kwa moyo mmoja.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi, Ali Mwanga aliitumia ziara hiyo kuwahimiza madiwani kwenda kwa wananchi kuwahamasisha kuwapeleka watoto wao shule.
Mwanga aliwataka madiwani kuwahimiza wazazi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na elimu ya Sekondari kuwapeleka shule kabla mwezi Januari haujaisha bila kujali kama wana sare za shule au hawana kwa sababu hakuna mwanafunzi atakayekataliwa shuleni kwa kukosa sare.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungu, Jerry Muro baada ya kusikiliza kero za wananchi wa vijijini mbalimbali ambako viongozi hao walifika, alimwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi kuwaelekeza watendaji wa idara ya kilimo kuwasimamia maafisa ugani wanaopaswa kufikisha mbegu kwa wakulima na hasa wa maeneo yaliyo pembezoni mwa wilaya hiyo.
Alisema kazi ya kufikisha mbegu kwa wananchi inapaswa kutekelezwa kwa uhakika kwa sababu maafisa ugani wana pikipiki walizopewa kuwarahisishia utekelezaji wa majukumu yao na kwa upande mwingine kuwaondolea wananchi usumbufu wa kutembea mwendo mrefu kufuata mbegu.
Aidha, Muro aliwataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kusoma taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi katika vijiji vyote vya wilaya hiyo kabla ya kumalizika kwa mwezi Januari.
Wakati huo huo, Muro aliwaarika wananchi wa Wilaya ya Ikungi kuhudhuria mkutano maalumu ambao Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba atazungumza na kutoa fursa kwa wananchi kueleza kero zao.
Alisema mkutano huo unaotarajiwa kufanyika leo, Januari 19, 2023 kuanzia saa nne asubuhi katika Kata ya Puma, Serukamba ataambatana na viongozi wa Kamati ya Usalama ya Mkoa, viongozi wa taasisi na mashirika yote ya Serikali yaliyopo Mkoa wa Singida.
Baadhi ya wananchi waliozungumza wakati wa ziara hiyo waliomba kupelekewa huduma za ugani hususan mbegu na mbolea katika maeneo yao ili waweze kuwahi mvua zilizoanza kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ikungi.
Ombi jingine lililotolewa na wananchi wengi ni viongozi wa vijiji na vitongoji kusoma taarifa za maendeleo za maeneo yao ikiwemo taarifa za mapato na matumizi ya vijiji vyao ili wananchi waweze kujua kazi zinazofanywa na Serikali yao.
Katika ziara hiyo ambayo pia ilijumuisha vikao vya ndani vya kiutendaji baina ya wajumbe wa halmashauri za vijiji na uongozi wa CCM kuanzia tawi hadi kata, wananchi walipata nafasi ya kupewa taarifa ya utendaji kazi na miradi inayotekelezwa katika wilaya na haswa Kata za Lighwa na Mang’onyi ikiwemo kazi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan tangu alipoingia madarakani
MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA WAKATI WA ZIARA YA VIONGOZI, WATENDAJI WA SERIKALI NA CCM WA WILAYA YA IKUNGI