CHARLES MULLINDA
TAIFA lina kiu ya Katiba Mpya ambayo sasa kuna kila dalili kuwa, Rais Samia Suluhu Hassan atatanzua mtanziko wa upatikanaji wake.
Dalili kuwa Rais Samia atatanzua mtanziko wa upatikanaji wa Katiba Mpya ni za muda mrefu. Zilianza kuonekana wazi Juni 28, 2021 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam; Ilikuwa siku yake ya 100 tangu alipoingia madarakani aliposema suala la Katiba Mpya lisubiri ajenge uchumi ulioathiriwa na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Nimepata kuandika huko nyuma kuhusu Rais Samia kuwa na nia ya kutanzua mtanziko wa upatikanaji wa Katiba Mpya na changamoto zitakazomkabili katika nia yake hiyo; leo hapa ninarejea kuandika nilichokiandika zaidi ya miaka miwili iliyopita huku nikikijazia nyama nyama ili kuzipa nguvu hoja ninazozingumzia kwenye makala haya.
Januari 3, mwaka huu alipokuwa akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Ikulu, Dar es Salaam Rais Samia alisema Serikali imedhamiria kukwamua mchakato wa Katiba Mpya ambao ulikwama mwaka 2014.
Kauli hiyo ya Rais Samia iliondoa kauli yake ya awali ya 2021 aliposema suala la Katiba Mpya lisubiri kwanza, alipokuwa akijibu sauti zilizokuwa zikimshinikiza wakati huo kurejesha mchakato huo.
Wakati huo, ujumbe wake wa kuwataka waliokuwa wakishinikiza kurejeshwa kwa mchakato huo kuwa na subira ulikuwa ni kuwataka wampe nafasi ya kupambana na vihunzi viwili ambavyo mosi; ilikuwa changamoto ya kuporomoka kwa uchumi na pili kuongoza na kusimamia vita ya kutokomeza janga hatari la Corona.
Kauli ya Rais kutaka subira ulivuta hisia za watu wengi wakiwemo wanasiasa na wanazuoni walioohoji subira isiyokuwa na mipaka wakiwa na shaka kuwa inaweza kuwa na maana ya kutokuwepo kwa mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wasiosukumwa na matamanio ya kukidhi kiu za kisiasa waliitafasiri kuwa; ili kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya uliobaki ambao ni kura ya maoni na pengine katika kura ya maoni pakahitajika maboresho zaidi endapo hapatakuwa na matokeo chanya kwenye hatua ya kwanza, basi patahitajika kuitishwa Bunge Maalumu la Katiba ili kufanya maboresho kabla ya kupiga kura ya pili. Na ili kukamilisha hayo inahitajika kuwepo fedha nyingi na za kutosha.
Kura ya maoni ni sharti iende na elimu ya mpiga kura hivyo ili kufanikisha hilo patahitajika nakala nyingi za Katiba kutosheleza mahitaji ya wananchi kuielewa Katiba na pengine njia nyingine za kutoa habari zitapaswa kutumika kufikisha ujumbe kwenye maeneo yasiyoweza kufikika na kwa wale ambao hawawezi kusoma wenyewe, njia mbadala ni budi zitumike ili kuwawezesha kuijua Katiba inayopendekezwa.
Kura ya maoni haina tofauti na uchaguzi mkuu na pengine inaweza ikawa zaidi ya uchaguzi mkuu kwa sababu mtoa elimu ya mpiga kura anakuwa Serikali; tofauti na uchaguzi mkuu ambapo vyama vya siasa vinakuwa na wajibu wa kutoa elimu ya mpiga kura kwa kunadi ilani zao.
Kwa sababu hiyo, kama Serikali haina ziada ya kutosha kumudu kugharamia mahitaji ya kura ya maoni, tafsiri yake ndiyo hiyo ya kusubiri hali ya uchumi itengemae.
Haina shaka kuwa sasa amefanikiwa kuruka vihunzi hivyo viwili vya kutengemaa kwa uchumi ya kuongoza kwa mafanikio mapambano dhidi ya janga la Corona. Hata hivyo, Rais Samia ambaye amekuwa akitizamwa na wanasiasa wa upinzani na hata wale wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni mwenyekiti wake wa Taifa kuwa mtu sahihi atakayewezesha kumalizika kwa mchakato huo, atalazimika kupambana na kihunzi kingine cha maridhiano ya pamoja kwa makundi yaliyosusia Bunge Maalumu la Katiba ili kuwa na msimamo wa pamoja.
Maridhiano ya pamoja katika suala la Katiba Mpya siyo jambo jepesi ikizingatiwa kuwa haijawahi kutokea duniani wakati wa kutunga Katiba kuwa na kauli moja kwa mambo yote ya msingi kwa sababu ya maono na mahitaji tofauti hasa yale ya kisiasa na kijamii ambayo ndio hubadilika badilika.
Ni kweli tayari yapo maridhiano ya kisiasa yaliyokwishafikiwa wakati huu wa utawala wake ambayo yametoa nuru ya kustawi tena kwa kile kinachoitwa demokrasia ya vyama vingi lakini anapolielekeza Taifa kwenye mchakato wa Katiba Mpya, upo uwezekano wa kurejea kwenye yaliyotokea mwaka 2014 wakati Bunge la Katiba lilipomeguka kwa sababu ajenda za wanasiasa wa Tanzania wanaodai sana Katiba Mpya zinafahamika.
Hivi sasa anapoelekea kutekeleza azma yake ya kulipatia Taifa Katiba Mpya, Rais Samia atalazimika kuchanga karata zake vizuri ili Taifa lisonge mbele na ajenda ya Katiba iwe ni historia ya rejea.
Amebeba mabegani matumaini ya wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo ya siasa ambao waliweka turufu yao kwake ya kuipatiaTanzania Katiba Mpya. Wapo wanasiasa wanaoheshimika na wanaharakati ambao wamekuwa wakipigia chapuo kupatikana kwa Katiba Mpya waliopata kuonyesha tumaini hilo kwake.
Kila mwenye matumaini ana ajenda yake. Hivyo ndivyo ilivyo kwa wanasiasa walioonyesha matumaini makubwa kwa Rais Samia ambao kwa sababu ya kuwa na kiu isiyomithilika ya kupata Katiba Mpya, alipowataka kuwa na subira walihoji subira isiyokuwa na ukomo huku tamaa ya waziwazi ya kutaka awe muwazi kwa kuelezea ni lini hali ya uchumi utatengemaa ili suala la Katiba lichukue mkondo wake wakiiweka mbele.
Hao ni pamoja na Prof. Ibrahim Lipumba, Zitto Kabwe, James Mbatia, Freeman Mbowe na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alikwenda mbali zaidi kwa kueleza kuwa ni wakati sasa kwa watawala kutanzua mtanziko wa upatikanaji wa Katiba Mpya huku akiunga mkono kauli ya Rais Samia ya kutaka apewe muda wa kutosha kabla ya kuanza kazi hiyo.
Jaji Warioba, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume iliyokusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya, mbali ya kuunga mkono kauli ya Rais Samia ya kutaka apewe muda, kwa tahadhali kubwa na kwa kuchagua maneno alieleza pia changamoto zilizopo katika kukamilisha mchakato huo. Kwa maneno yake mwenyewe, alisema;
āRais ameomba muda ni kweli lakini muda gani? Nadhani ni juu ya viongozi kukubaliana ni lini hasa mchakato wa Katiba Mpya utaendelezwa. Tunaweza kufanya kwamba tuvumilie mpaka mwaka 2024 wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tuunganishe. Wakati wananchi wanapiga kura, wapige na kura ya maoni.
āHaya yakifanyika Taifa litatulia. Mimi sioni hili kama ni tatizo naona ni rahisi kabisa. Ifike mahali tufanye uamuzi, tukifanya uamuzi nchi itatulia.ā
Alieleza zaidi kuwa Katiba iliyopendezwa inapaswa kufanyiwa marekebsho madogo ambayo hayahitaji kuitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba, kauli inayoipa uzito changamoto ya wapi panapaswa kuwa mwendelezo wa ukamilishaji wa mchakato huo pasipo kuibua malumbano au minyukano kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii na hasa wanasiasa na wanaharakati; mambo ambayo Rais Samia anapaswa kuyatarajia na kujipanga kukabiliana nayo.
Mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya ulianza rasmi mwaka 2010 baada ya Rais wa Awamu wa Nne, Jakaya Kikwete kutangaza dhamira ya Serikali aliyokuwa akiiongoza ya kuanzisha mchakato huo.
Hatua hiyo ya Rais Mstaafu Kikwete ilifuatiwa na kuanza rasmi kwa mchakato huo mwaka 2011 ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011, sura namba 83/2012 na baadaye Sheria ya Kura ya Maoni namba 11/2013.
Baada ya kutungwa kwa sheria hizo, Rais Kikwete aliuunda Tume ya Katiba na kumteua Jaji Warioba kuwa Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya iliyohakikiwa na mabaraza ya Katiba kabla ya kupatikana kwa Rasimu ya Katiba Mpya.
Rasimu hiyo ilipelekwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo mwenyekiti wake alikuwa marehemu Samuel John Sitta na makamu wake alikuwa Rais Samia. Hata hivyo, mchakato wa uandishi wa Katiba hiyo ulikumbwa na misukosuko baada ya waliokuwa wajumbe kutoka baadhi ya vyama vya siasa vya upinzani kususia vikao vya Bunge hilo na kundoka.
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliosalia ambao walitoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe wa kundi la 210 ambao hawakutokana na vyama vya siasa waliendelea na mchakato hadi ilipopatikana Katiba iliyopendekezwa kwa kura iliyokidhi theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.
Katiba hiyo iliyopendekezwa ilipitisha na kukubaliana na maudhui kwenye Rasimu ya Katiba kama vile Tume Huru ya Uchaguzi, mgombea binafsi, ruhusa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais mahakamani na kura za rais ziwe zaidi ya asilimia 50 ili kutangazwa kuwa mshindi.
Sehemu ambazo zilifanyiwa marekebisho tofauti na maono yaliyobainishwa kwenye rasimu ya Katiba ni pamoja na pendekezo la kuwepo kwa Serikali tatu, kuondoa kabisa madaraka ya Rais na baadhi mengineyo ambayo Bunge la Katiba halikuona mantiki yake hivyo liliboresha kwa kuondoa kutokubaliana na maudhui ya Rasimu ya Katiba baada ya mivutano na minyukano mikali kwenye kamati na hata ndani ya Bunge lenyewe.
Katiba iliyopendekezwa iliwasilishwa rasmi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tazania na yule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini kuliibuka kelele kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na wanaharakati kuwa Katiba iliyopendekezwa haina muafaka wa maridhiano kwa sababu baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba walisusa kupiga kura kuthibitisha Katiba inayopendekezwa.
Haina shaka Rais Samia anaujua msimamo wa wanasiasa waliogoma kupiga kura kuthibitisha Katiba inayopendekezwa na kama msimamo wao huo haujabadilika, atakabiliwa na mtihani wa kutumia ushawishi wake kuwalainisha.
Mbali na Rais Samia, kama Taifa tunapoelekea kurejea kwenye mchakato wa Katiba Mpya inatupasa kurejea sababu mbalimbali za kutopiga kura zilizoainishwa wakati wa kukabidhi Katiba ambazo ni pamoja na kauli za vitisho kwa baadhi ya viongozi wa Serikali waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, mivutano ya kiitikadi katika mijadala ndani ya kamati na bungeni na pengine lililo kubwa zaidi ni mtizamo wa kisheria juu ya mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba kuichambua Rasimu ya Katiba na kuacha baadhi ya mambo yaliyopendekezwa, kana kwamba halikuwa na utashi huo uliotokana na Sheria, sura namba 83.
Taifa lirejee kwenye mchakato wa Katiba Mpya likitambua kuwa tafsiri ya sheria tajwa hapo juu ipo wazi na pengine inakwenda mbali zaidi, mwaka 2011 wakati wabunge wa Bunge la Tanzania walipokuwa wanapitisha sheria na 83 kwa umoja wao wakijumuisha wabunge kutoka chama tawala na vyama vya upinzani vilivyokuwepo wakati huo, Chadema, CUF, ACT Wazalendo, NCCR mageuzi na UDP, kwa kauli moja walipitisha sheria hiyo na tafisiri yake juu ya mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba kufanyia kazi Rasimu ya Katiba kama litakavyoona inafaa.
Ni jambo lililo wazi kuwa Watanzania wanataka kupata Katiba Mpya kwa namna ambayo itawakilisha matakwa ya walio wengi bila kujali kama wanasiasa watakuwa sehemu ya mchakato huo ingawa ndiyo huwawakilisha wananchi katika vyombo vya maamuzi kama vile Bunge, Baraza la Wawakilishi na mabaraza ya halmashauri, lakini Watanzania wote wana haki sawa bila kujali itikadi zao au nafasi zao katika jamii.
Watanzania ni budi tutambue kuwa Katiba bora inapaswa kufuata misingi ya haki na uhuru wa mtu mmoja mmoja wakati wa kuiandika badala ya kuwa na Katiba ya kutimiza malengo ya upande mmoja katika jamii.
Jambo la kuzingatia ni kwamba dhamira ya kupata Katiba Mpya haipaswi kuwa na utashi wa mabadiliko ya uongozi wa nchi kwani rekodi zilizopo duniani kuhusu dhamira ya upatikanaji wa Katiba kwa namna hiyo zinaonyesha kuwa huangamiza Taifa.
Kwa hulka ya kibinadamu ni jambo lisilowezekana kwa watu wote kuwa na uelewa unaofanana au kukubaliana katika kila jambo na hiyo ndiyo siri ya michakato ya Katiba duniani kutumia mfumo wa Bunge la Katiba kwa uwakilishi wa uwiano na utashi wa dhamira iliyo chanya.
Hata hivyo, bado huwa kuna sehemu ya watu katika jamii ambao huwa na maoni tofauti au kinzani ambao nao inapaswa wapewe haki ya kusikilizwa kwa staha na mwisho utashi wa walio wengi hutawala kwa maslahi ya wote.
Watanzania tunapokabiliana na upepo wa hitaji la Katiba Mpya tunapaswa kuogozwa na alama ya Taifa katika hitaji hilo na hasa bendera ya Taifa yenye rangi zaidi ya tatu lakini kati ya rangi hizo hakuna rangi nyekundu ingawa uhuru wa Tanzania ulipitia kwenye harakati za kumtoa mkoloni.
Wazee wetu wakumbuke na vijana wetu wafundishwe kuwa katika harakati hizo adui aliyekuwepo aliwaunganisha Watanzania wote kuwa kitu kimoja lakini hapakuwa na umwagaji wa damu.
Utamaduni huu ndiyo uendelezwa katika hili la Katiba Mpya licha ya kuwepo misukosuko ya hapa na pale inayojitokeza kwa wanaoshinikiza upatikanaji wa Katiba Mpya ambao wakirejea kwenye ushuhuda huo utawaongoza kudai Katiba Mpya kwa hoja na staha.
Katiba ya sasa ya Tanzania ilitungwa mwaka 1977 na imepata kufanyiwa marekebisho mara 14. Nyuma yake ipo Katiba ya mwaka 1961 iliyofuatiwa na ya mwaka 1962, kisha 1964 na baadaye 1965. Mwaka 1984 kulikuwa na mabadiliko makubwa ya katiba ambayo ndiyo yapo hadi leo.